Mara wamsubiri Mbowe

Maandalizi ya jukwaa kwa ajili ya mkutano wa hadhara wa Chadema utakaofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Mukendo mjini Musoma leo Jumapili Januari 22, 2023.  Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Viongozi na  wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mara wamejiandaa kumpokea Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe na viongozi wengine wa kitaifa tayari kwa mikutano ya hadhara itakayofanyika mjini Musoma leo Jumapili Januari 22, 2023 na Mjini Tarime kesho.


Musoma. Viongozi na  wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mara wamejiandaa kumpokea Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe na viongozi wengine wa kitaifa tayari kwa mikutano ya hadhara itakayofanyika mjini Musoma leo Jumapili Januari 22, 2023 na Mjini Tarime kesho.

Mkutano huo utakaofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Mukendo utakuwa ni wa pili kwa chama hicho kikuu cha upinzani baada ya ule wa uzinduzi uliofanyika jijini Mwanza jana Jumamosi.

Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami ameiambia Mwananchi kuwa mkutano huo pia utahudhuriwa na viongozi na wana Chadema kutoka mikoa ya Simiyu na Shinyanga ambayo kwa pamoja na Mara inaunda kanda hiyo ya Serengeti.

"Awali, tulipanga kufanya mkutano mmoja tu wa uzinduzi mjini Musoma kwa Kanda ya Serengeti, lakini tumelazimika kuongeza mwingine utakaofanyika mjini Tarime kesho Januari 23, 2023 kutokana na maombi pia hamasa ya wanachama," amesema Mnyawami.

Amesema kabla ya kufika Musoma mjini mapokezi rasmi yatafanyika eneo la Stendi ya Bweri, Mbowe pamoja na viongozi wengine atakaoambatana nao watasimama kusalimiana na wananchi katika vituo maalum vya Ramadi, Bunda, Kyabakari na Makutano Ziroziro na tayari taratibu zote za kisheria ikiwemo kutoa taarifa Jeshi la Polisi kwa ajili ya ulinzi na usalama imekamilika.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mara, Lucas Ngoto amesema maandalizi ya mikutano yote miwili yamekamilika huku maombi ya kutaka viongozi hao wa kitaifa kufika kila jimbo la uchaguzi yakiwa mengi kutokana na hamasa ya mikutano baada ya kukosekana kwa takribani miaka saba tangu ilipozuiwa mwaka 2016.

"Kutokana na ratiba kuwa ngumu, uongozi wa chama utaandaa ratiba ya mikutano kila jimbo itakayoshirikisha viongozi wa kikanda na kitaifa kwa siku zijazo kukidhi kiu ya wananchi wenye hamu ya kuwasikiliza viongozi wao," amesema Ngoto

Ameongoza; "Tunawasihi wanachama na wananchi wa mikoa ya Mara, Simiyu na Shinyanga inayounda kanda ya Serengeti kukubali tufanye mikutano miwili ya Musoma na Tarime mjini kama sehemu ya uzinduzi ya mikutano katika kila kona ya kanda yetu siku zijazo,"

Katibu mstaafu wa Chadema Mkoa wa Mara, Chacha Heche amesema mikutano ya mjini Musoma na mjini Tarime inasubiriwa kwa hamu kutokana na wananchi kukosa fursa ya kuwasikiliza viongozi wao kwa kipindi kirefu mikutano ilipozuiwa.

"Kwa mtazamo wa kawaida, hii mikutano ya uzinduzi ni sehemu ya sherehe ya kuondolewa kwa zuio la shughuli za kisiasa iliyotunyima haki ya kikatiba na kisheria ya kufanya siasa," amesema Heche.

Mwanasiasa huyo amelinganisha mikutano hiyo ya uzinduzi na sherehe ya kumpokea nyumbani ndugu yao aliyetoka kifungoni inayochanganyika na machozi ya furaha na huzuni kwa pamoja.

Amesema hitimisho la sherehe za kutoka kifungo haramu cha shughuli za siasa itakuwa wakati wa mapokezi ya viongozi na makada wa Chadema waliokimbilia ughaibuni kwa madai ya usalama baada ya kuhisi tishio la maisha na usalama wao wakiwemo Makamu Mwenyekiti (Bara), Tindu Lissu, wabunge wa zamani, Godbless Lema na Ezekiah Wenje na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Kanda ya Victoria, Ansbert Ngurumo.

Kada wa Chadema mjini Musoma, Abdullah Maulidi amesema kurejea kwa mikutano ya hadhara ni fursa kwa wanamageuzi wote bila kujali itikadi zao kusukuma ajenda ya Katiba Mpya itakayounda taasisi imara za kuongoza Taifa.