Mbowe atoa tumaini jipya Tanzania

Muktasari:

Wakati jana Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiadhimisha miaka 30 tangu kipate usajili wa kudumu Januari 21, 1993, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe anasema safari hiyo ni ndefu iliyojaa kila furaha na huzuni, lakini anaamini Watanzania watafika kwenye nchi waitakayo.

Wakati jana Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiadhimisha miaka 30 tangu kipate usajili wa kudumu Januari 21, 1993, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe anasema safari hiyo ni ndefu iliyojaa kila furaha na huzuni, lakini anaamini Watanzania watafika kwenye nchi waitakayo.

Katika mahojiano yake na Mwananchi, Mbowe anaeleza safari waliyopitia, mafanikio na matarajio yao kwa siku zijazo.

Mwananchi: Mnajivunia nini tangu mlivyoanzishwa?

Mbowe: Katika mazingira magumu na kandamizi, tumeweza kujenga “Chama Imani” kwa mamilioni ya Watanzania, wakati fursa za ajira, mali, kandarasi, madaraka, ‘kulindwa’zikiwa ndiyo mvuto wa washindani wetu, mvuto kwa Chadema umekuwa sera zetu, imani yetu ya kujenga kada inayoamini katika haki, uhuru wa watu, ustawi wa wote, demokrasia na utawala wa sheria.

Pamoja misukosuko mingi inayochagizwa na mashambulizi kutoka kwa washindani wetu tumeendelea kukua na kuieneza imani ya Chadema ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.

Chama chetu kimejengeka hatua kwa hatua bila kusinyaa kuanzia uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi wa 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015.

“Idadi ya Madiwani 1994 - 42, 2000 - 72, 2005- 102, 2010- 578, 2015 - 1,108

2020 - 85 huku idadi ya Wabunge

1995- 4, 2000- 5, 2005- 11, 2010- 49, 2015- 73,2020- 1”

Chaguzi za Serikali za Mitaa za mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ulivurugwa kiasi cha kuwa Uchafuzi badala ya Uchaguzi na sisi kama Chama hatuyatambui matokeo ya uchaguzi ule na ndicho kilichokua msingi Mkuu wa hitajiko la Agenda za Maridhiano kati ya CCM na Chadema ili kutanzua vikwazo vingi vinavyokabili demokrasia, uhuru, haki na maendeleo ya watu.

Mpaka 2020 tulishiriki kikamilifu katika kuimarisha Bunge na kulifanya kuwa na uwezo wa kuiwajibisha Serikali na kuisimamia katika nyakati tofauti.

Itakumbukwa kuwa tuliongoza halmashauri za majiji, miji na wilaya kiufanisi na kutekeleza sehemu ya sera zetu.Kwa mfano Halmashauri ya Wilaya ya Karatu ilikuwa ya kwanza kufuta kodi ya kichwa iliyokuwa inawatesa na kuwanyanyasa sana wananchi, baada ya hatua hiyo mwaka 2000, Serikali Kuu iliamua kuifuta kodi hiyo nchi nzima.

Huwezi kusahau tulivyoongoza kambi rasmi ya upinzani bungeni kati ya mwaka 2010-2020 na kufanikisha kusukuma ajenda za kitaifa, ikiwemo Katiba Mpya ambayo mchakato wake bado tunaendelea nao hadi itakapopatikana.

Mwananchi: Ni nyakati gani zilikuwa ngumu kwenu?

Mbowe: Kimsingi tumepoteza watu wetu waliouwawa kwa nyakati tofauti kwa kipindi chote hicho na idadi yao ni kubwa, lakini wameacha alama ya kufa wakipigania demokrasia ya Tanzania.

Wapo ambao walifungwa, kuteswa na hata kuumizwa kwa risasi na mabomu kwa nyakati tofauti na wapo waliofilisiwa mali zao na biashara zao kuharibiwa na watawala kwa nyakati tofauti kwa kipindi chote hicho.

Katika Serikali ya awamu ya tano hali ilikuwa mbaya zaidi, kwa sababu ya mateso makubwa ambayo wanachama na viongozi waliyapitia kutoka katika vyombo vya dola na hata kupelekea baadhi ya viongozi na wanachama wetu kuikimbia nchi na familia zao wakihofia usalama wao, huku wakiziacha mali zao na biashara zikiteketea au kuharibika.

Tumeishi kwa kuwindwa mara zote, kukamatwa, kubambikiwa kesi mbalimbali na hivyo mahabusu na magereza kuwa sehemu ya maisha yetu, lakini hatukukata tamaa wala kurudi nyuma.

Tumeishi kwa kubaguliwa kwa sababu za kiitikadi kwenye ajira Serikalini na maeneo mbalimbali ya huduma za kijamii.

Mikakati michafu ya kununua wanachama na viongozi wetu ilishamiri na kuota mizizi katika Serikali ya awamu ya tano na kutokana na mateso na fedheha walizokuwa wanapitia viongozi wengi walilazimika kujiunga na watawala ili kusalimisha maisha yao na mali zao.”

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa nyakati tofauti imetumika kukihujumu chama chetu kwa nia ya kukidhoofisha ili kuua kabisa ustawi wa demokrasia ya vyama vingi nchini .

Mwananchi: Mnaendesha vipi chama bila ruzuku ya Serikali baada ya kuigomea mwaka 2020?

Mbowe: Chama chetu kimekuwa kikiendeshwa kwa michango kutoka kwa wanachama na viongozi, ada za uanachama na hivyo ndivyo tumekijenga chama ambacho watu wake wanaishi kwa kujitolea.

“Ruzuku ilikuwa sehemu kidogo sana katika kuendesha chama na ndiyo maana hata kipindi hiki ambacho haipo tumeendelea kukijenga na kuendesha chama.

Leo tunaanza uzinduzi wa mikutano ya hadhara bila kusubiri ruzuku na tutaendelea mbele kuhamasisha wanachama waendelee kujisajili kidijitali na walipie ada za mwaka ili kukiwezesha kuendelea kujiendesha kwa ufanisi zaidi.

Mwananchi: Nini siri ya kuwekeza zaidi kwa vijana?

Mbowe: Mara zote tumeendelea kuwekeza kwa vijana, kwani wao ndio Taifa linawategemea na ndiyo nguvu kazi yake.

Kwa upande wa vijana wa vyuo vikuu, huko nyuma tulikuwa tunawafuata mmoja mmoja, lakini sasa tumewaundia taasisi yao kwenye vyuo vyote nchini inaitwa CHASO (Chadema Students Organisation), hiki ni chombo kinachoendelea kuwaandaa viongozi wa leo na wajao.

Kimsingi viongozi wengi wa vijana waliopo leo walipitia kwenye taasisi hiyo.

Mwananchi: Mliathirika vipi na zuio la mikutano ya hadhara?

Mbowe: Lilituathiri chama na Taifa, tulipata hasara kubwa kuliko faida, tulinyimwa haki ya kukusanyika iliyotolewa na Katiba ya nchi na sheria ya vyama vya siasa, tulishindwa kuwafikia watu wetu moja kwa moja na kuwaeleza kuhusu sera zetu na kuvutia wanachama wapya.

“Zuio hili lilikuwa linabomoa umoja wa kitaifa ambao ulijengwa kwa gharama kubwa na muda mrefu. Kwa mfano kumtaka kiongozi wa kitaifa wa chama akahutubie kwenye jimbo lake au kata yake tu aliyochaguliwa kama Mbunge au diwani, ni Jambo la hatari kwa umoja wetu.

Hili lilisababisha viongozi wajifungie kwenye maeneo yao tu ama walikozaliwa au wanakoishi...Kamwe tusithubutu kufanya jaribio kama hili tena, kwani tunaweza kuligawa Taifa vipande vipande.

Demokrasia ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi. Penye demokrasia iliyodumaa na uchumi hudumaa na badala yake rushwa na ufisadi hutamalaki.

Hofu kubwa imetanda nchini kutokana na vitisho na hivyo kuwafanya wanachama wetu kuogopa kujitambulisha kuwa ni wanachama wa vyama vya upinzani.

Mwananchi: Nini mafanikio ya Chadema digital?

Mbowe: Mafanikio ni makubwa na tunaendelea kuimarisha mfumo huo, kwani kwa kipindi chote ambacho tulizuiwa kufanya mikutano tuliendelea kukutana na wanachama wetu kwa njia ya kidijitali na tulihamishia mikutano ya hadhara kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Tutaendelea kukiendesha chama kwa njia hii, kwani ndiko ulimwengu uliko kwa sasa na siku zijazo.

Mfano, sasa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wametangaza hatua waliyofikia ya kuwa na sarafu ya kidijitali.

Ndio tunaelekea kwenye uchumi wa kidijitali, ndiyo maana ni muhimu kuimarisha mfumo huu.

Mwananchi: Nini uwekezaji wenu?

Mbowe: Uwekezaji wetu mkubwa na muhimu kuliko wote, ni mtaji wa wanachama wetu tulionao na tutaendelea kuwashawishi Watanzania kwa sera mbadala ili waendelee kujiunga kwa wingi, kwani huu ndio mtaji wa chama cha siasa.

Chadema tunaendelea kuwekeza kwenye Chadema digital, lakini mazingira ya kuwekeza kama chama cha siasa cha upinzani nchini sio rafiki hata kidogo.

Tunaendelea na madai ya kupata Katiba mpya ambayo itaweka sawa uwanja wa kufanya siasa na uwekezaji kwa vyama vyote bila ubaguzi na uonevu wa mifumo na sheria zetu.