Mjema atamani CCM kuwa na kasi ya Supersonic

Katibu wa Itikadi Siasa na Uenezi wa CCM, Sophia Mjema.

Muktasari:

  • Katibu wa Itikadi Siasa na Uenezi wa CCM, Sophia Mjema ametuma salama kwa watendaji wa chama kuwa lazima watatue kero za watu kwa kasi.

Dodoma. Katibu wa Itikadi Siasa na Uenezi wa CCM, Sophia Mjema ametuma salama kwa watendaji wa chama kuwa lazima watatue kero za watu kwa kasi ipitayo ile ya sauti (supersonic).

Mjema ametoa kauli hiyo leo Jumanne Januari 24, 2023 wakati akisalimia wanachama wa CCM Mkoa wa Dodoma wakati wa mapokezi ya Sekretarieti mpya ya chama hicho.

Januari 14, 2023 Halmashauri Kuu ya CCM iliwathibitisha Sekretarieti mpya kwa chama hicho ambayo ipo chini ya Katibu Mkuu, Daniel Chongolo huku Sophia Mjema akichukua nafasi ya aliyekuwa Katibu wa Itikadi Siasa na Uenezi Shaka Hamdu Shaka.

"Kuanzia tutaanza kutoa elimu kwa wanachama wetu ili wakijue chama chao vema, lakini nawaambia watendaji wote kuwa mnatakiwa kutatua kero siyo kusubiri Sekretarieti ije kutatua kero za watu," amesema Mjema.

Amesema kero zote lazima zipatiwe ufumbuzi na wananchi wapate imani Kwa chama chao kuwa kinawasikiliza kwenye matatizo yao.

Mwenezi huyo amesema atatumia uzoefu wake wa miaka 18 ndani ya chama ili kukifanya CCM kuwa Super Sonic huku akiahidi kutowaangusha wanawake.