Mtifuano mpya makada wa Chadema Chanika

Mwenyekiti Chadema Kata ya Chanika,Ibrahim Omary akizungumza wakati alipowavua uanachama wanachama sita. Picha na Pamela Chilongola

Muktasari:

  • Sintofahamu imeibuka baina ya makada wa Chama cha Chadema Kata ya Chanika baada ya kuwapo kwa mvutano wa uhalali wa uanachama wa makada sita wa chama hicho wanaodaiwa kufukuzwa kutokana na kukiuka mienendo ya chama.

Dar es Salaam. Sintofahamu imeibuka baina ya makada wa Chama cha Chadema Kata ya Chanika baada ya kuwapo kwa mvutano wa uhalali wa uanachama wa makada sita wa chama hicho wanaodaiwa kufukuzwa kutokana na kukiuka mienendo ya chama.

Hayo yameelezwa leo Jumapili Oktoba 22, 2023 na Mwenyekiti wa Chadema Kata hiyo, Ibrahim Omary huku akisema maamuzi hayo yamebarikiwa na kikao kikao cha kamati tendaji kilichofanyika jana Oktoba 21, 2023.

Omary amesema makosa mengine yaliyosababisha wanachama hao kuvuliwa uanachama ikiwemo kukihujumu chama hicho Kwa kupinga maazimio na misimamo ya chama nje ya vikao halali na kuunda kamati tendaji ya kata na kufanya vikao huku wakijua ni kinyume cha katiba.

"Kutoa siri za chama kwa washindani wetu wa kisiasa wamekuwa wakiwaeleza watu wengine mambo yanayoendelea kwenye chama cheti,"amesema na kuongeza:

"Kuanzia leo Oktoba 23 mwaka huu wanachama Hawa hawatarihusiwa kujihusisha na kazi za chama wala kutumia nembo ya chama cha Chadema mahalo popote kwani Kwa kufanya hivyo watakuwa wanakiuka sheria za nchi",amesema Omary

Wakati Omary akiutaja uamuzi huo upande makada hao sita waliodaiwa kuvuliwa uanachama ambao ni Charles Sangiwa, Paul Kigonti, Augustine Mkello, Seif Haji, Ally Kakwaya  na Frenk Mwambepo wamepinga maamuzi hayo huku wakidai kutoyatambua.

"Sisi bado wanachama tupo ofisini tunaendelea na zoezi la kuwasajili wanachama wapya kidigitali ambapo zoezi litaanza saa 10 jioni eneo la Nguvu Kazi," amesema Charles Sangiwa, mmoja wa wanachama waliodaiwa kufukuzwa.

Naye Paul Kigonti amesema yeye bado ni mwanachama wa Chadema na ni Katibu wa kata ya Chanika hivyo anadai waliowafukuza uanachama siyo viongozi halali.