Ndingo aanika matano atakayoanza nayo Mbarali

Mgombea ubunge wa Mbarali (CCM), Bahati Ndingo akisaliamiana na wananchi wa Kata ya Lugelele baada ya kuwasilia eneo kwa ajili ya kufanya mkutano wa hadhara wa kampeni za jimbo hilo. Picha na Bakari Kiango
Mbarali. Mgombea wa ubunge wa Mbarali mkoani Mbeya kwa tiketi ya CCM, Bahati Ndingo amesema endapo atafanikiwa kushinda nafasi hiyo ataanza kuyasimamia mambo matano ikiwemo suala la migogoro ya ardhi ili wananchi wa Mbarali walime kwa ufanisi na kujiletea maendeleo.
Mengine ni upatikanaji wa umeme wa uhakika na gharama nafuu kulingana na maeneo husika, barabara za mitaa na maji ambayo bado ni changamoto katika jimbo hilo.
Ndingo alieleza hayo jana akiwa katika vijiji vya Kaniago, Lugelele na Iwanje katika mwendelezo wa kampeni za kuwania ubunge wa jimbo hilo iliyoachwa wazi na Francis Mtega aliyefariki dunia Julai Mosi, mwaka huu baada ya kugongwa na trekta dogo (Power Tiller) shambani kwake.
Akizungumza na wananchi hao, Ndingo amesema endapo atashinda kiti hicho anataka suala la migogoro ya ardhi lipatiwe ufumbuzi wa kudumu ili wananchi wa Mbarali wanufaike na rasilimali hiyo na kukuza na uchumi wao.
"Bado kuna tatizo la umeme kukatika mara kwa mara Mbarali na vijana wengi wamejiajiri kupitia saluni na mashine kusaga na kukoboa, sasa hali hii inawapata wakati mgumu katika utekelezaji wa majukumu hasa kujipatia kipato.
"Hata hivyo, Serikali inafanya marekebisho katika njia ya umeme mkubwa wa kuingilia Mbarali, sasa tutaihimiza Serikali iangalie namna ya kutekeleza jambo hilo kwa awamu ili wananchi kupata huduma na kupunguziwa mgao wa muda mrefu," amesema Ndingo.
Ndingo pia amesema atahakikisha anashughulikia bei za umeme wilayani humo hasa vijijini, akisema kuna baadhi ya maeneo yanachanganya watu washindwa kufahamu gharama halisi wanayotakiwa kuilipa ili kupata huduma hizo.
"Nikipata fursa ya kuwa mbunge wenu nitahakikisha Serikali inakuja kutoa ufafanuzi kuhusu sintofahamu hii kwa wananchi wa Mbarali.Nataka mpate neema changomoto zenu, naomba Septemba 19 msiniangushe nipelekeni nikachape kazi," amesema Ndingo.
Kuhusu changamoto ya maji, Ndingo aliyekuwa mbunge wa viti maalumu, kabla ya kujiuzulu na kuwani nafasi hiyo hivi sasa, amesema Serikali imefanya juhudi kubwa za ikiwemo kupeleka miradi wilayani Mbarali lakini ataongeza nguvu zaidi ili kuondokana na tatizo hilo.
"Kazi ninaiweza nipeni kura wananchi wa Mbarali nitapeleka changamoto zenu maeneo husika. Kata ya Lugelele kijiji cha Kanioga. Nipe ridhaa tuchape kazi," amesisitiza.
Kabla ya kumaliza hotuba yake Mkazi Lugelele Catherine Omar alimtaka mbunge huyo kuwahakikishia kuwa endapo akifanikiwa kuibuka mshindi katika mchakato atakuwa akiwatembelea katika maeneo na sio kuwatelekeza.
"Tunaomba ukipata ubunge utukumbuke tu lakini huwe unatutembelea hapa kwetu, maana kuna mmoja alikuwa mbunge lakini hakuwa na utaratibu wa kutumbelea kusikikiliza kero zetu.Hapa tuna shida ya vivuko kwenda Rujewa tunaomba utusaidie Catherine.
Akijibu changamoto hizo, Ndingo amesema "najua changamoto hii, kwa sababu na watoto wanapata shida kuzunguka kwenda Rujewa ambapo ni kilomita moja lakini wanatumia mwendo mrefu hadi kufika huko hasa kipindi cha masika.
"Huduma nyingi zinapatikana makao makuu ya Rujewa lakini mtakuta mnazunguka wakati wa masika, nipeni kura zenu ili nikaongeze nguvu kulisuka jambo hili. Nipe ridhaa nikaongeze nguvu zaidi ya kuisukuma Serikali iboreshe miundombinu ya Kanioga ikiwemo Kivuko," amesema Ndingo.
Katika mikutano hiyo ya hadhara Ndingo aliambatana na mbunge wa Momba Conchesta Sichwale aliyesema
"Katika heshima na kuweka historia hakikisheni Bahati amepita, mpeni dhamana Bahati uzuri kina mama hatujawahi kushindwa.
"Mama atafanya kila liwezekanalo, kina mama wanafanya kazi kwa juhudi kubwa sana, naomba muwe mabalozi kwa kumtafutia kura katika vijiji vya jirani," amesema Sichwale.