NIKWAMBIE MAMA: Tuna maisha ya samaki mkubwa kumla mdogo

Muktasari:

  • Nakusalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kazi iendelee!

Awali ya yote nakupa pole kwa kazi nzito ya kuliongoza Taifa letu.
Natambua kuwa kuwaongoza wabongo ni zaidi ya kurusha ndege iliyosheheni milipuko! Wabongo wanaweza kukushangilia na dakika hiyohiyo wakakubadilikia. Inataka kichwa ngumu sana kuwapika kwenye chungu kimoja, ndiyo maana hata daktari wa vichaa huwa na sura mbili (ya nyumbani na ya kazini).

Lakini pia nashukuru kupata nafasi ya kukufikia na kukueleza yale yasiyo na bahati ya kukufikia mezani pako. Nafahamu kwamba mengi yapo kwenye kina ambacho urefu wa kata ya kuchotea haujatimu kufika kwenye kina chake.

Naamini yote unayoletewa mezani ni matone ukilinganisha na makombe yaliyofunikwa kutupisha wanaharamu. Nina mengi yasiyoweza kutosha kwenye msahafu mmoja, hata hivyo, nitaheshimu muda na majukumu yako mazito. Aus sio mama nikwambie au?

Kama kawaida kwa sisi waswahili, kilio huwa ni jadi yetu, tukikosa tunalia njaa na tukipata tunalia kuvimbiwa. Ili kukuelewesha haya ninayoelekea kukwambia, leo nitasimamia “uswahilini” ambako ndiko pekee unakoweza kupata picha ya ujumla ya wananchi wako.

Maana uswahilini nako kuna mabosi wanaokula bata mzinga (japokuwa ni kwa uwiano wa mmoja kwa makapera mia moja). Nasikia uwiano wa kule ushuani ni mabosi kumi kwa kapera mmoja.

Uzuri wa mabosi wa huku ni vile wanavyodhani kuwa wao ndio wanaomfuatia Mungu kwa ukubwa. Siku ukijikwaa na kukosakosa kumwaga bia yake utasikia:

“Unanijua mimi nani?” Ni bora kule ushuani ambako unaweza kumwogopa kila mtu kwa kutojua nani ni nani. Unaweza ukajichanganya kumtusi mtu anayetunza funguo za riziki ikala kwako. Ndiyo maana nasema uswahilini tunapata picha ya ujumla.

Nina hamu sana kukutembeza mtaani kwetu (kama kweli kuna mtaa) ujionee hali halisi, lakini naogopa wenzangu wanaweza kudhani wameshukiwa na Masiha.

Watakubebesha mizigo ya shida ushindwe kufanya kazi zako. Huyu atakwambia tumbo linamuuma, yule atakulalamikia kijumbe kamdhulumu, mwingine atajaribu kukupa “ubuyu” eti jirani yake anakula maini mwezi mzima japo hana kazi!

Pamoja na kwamba matatizo ya Watanzania wote yanakuhusu kwa kuwa ni kiongozi wao, lakini mengine hayakuhusu moja kwa moja. Iweje mtu aje kukulalamikia njaa badala ya kula na kumaliza tatizo lake?

Au tuseme ni sawa na muota moto anayeacha kuondoa kidole kinachoungua kwenye kuni akisubiri zimamoto? Usije ukaacha kusikiliza yangu maana ni ya msingi kati ya walio wengi.

Huku tunaishi kama samaki, mdogo kuwa chakula cha mkubwa. Pamoja na nchi yetu kuongozwa na sheria na katiba, kwetu hakuna msamiati huo.
Huku saa ya mkubwa ndiyo inayosema ukweli daima. Na ndio chimbo lao la uhakika kwa kuwa kwao ni fursa nzuri ya kuchumia utumbo wao. Ukiwauliza wanafanya hivyo kwa mamlaka gani watakwambia “Unanijua mimi ni nani?”

Kwa bahati mbaya asilimia kubwa ya wakazi wa huku wamerithi mitaji ya masikini. Hawana elimu wala mtaji fedha, bali wanategemea nguvu zao kuutafuta ugali wa siku wanayoiishi.

Maisha yao hayana tofauti na mfumo wa ujima, japo haya yanahusisha sarafu chache: Mmoja atakwenda sokoni kununua fungu sita za bamia, atauza mafungu matano apate hela ya mkaa na unga robo. Fungu moja atalipika mlenda watoto wale, siku imeisha.

Tatizo linaanza pale wakubwa wanapoona kuwa kumbe maisha yanawezekana hata kwa mtindo huu. Watakuja kuwapanga masikini hao kando ya barabara kwa utaratibu wa kulipia shilingi mia tano kwa kila meza.

Atakayeshindwa kulipia atanyang’anywa bidhaa zake wenye nguvu wakale. Muathirika akienda kulalamika atapigwa faini kwa kufanya biashara mahala pasipo rasmi, na kwa kuchafua mazingira.

Ukiwa na bahati ya kumpata bosi mmoja kati ya wanaofanya ubadhirifu huo atakwambia “kama kusingekuwa na wadhambi, wachungaji wa kondoo za bwana wangelifanya kazi gani?”

Masikini mimi kwa mawazo yangu hawa hawafanani na wanaojifananisha nao, bali wanafanana na mganga anayekuroga ili akuuzie tiba. Ni sawa na wale wanaosaini mauziano ya viwanja vya mabondeni, kisha kuwafukuza wahamiaji.

Inasikitisha sana. Kama ningeulizwa mchanganuo wangu ningeuweka hivi; Kwa kuwa mataifa mengi yaliyokuwa masikini wa kutupwa kama India yalipata maendeleo kidogo kidogo kwa muda mrefu, hawa masikini wangeweza kuendelea kulipia hizo mia tano tano katika muda fulani.

Mamlaka za mitaa zingesimamia fedha hizo kwa ujenzi wa masoko rasmi na kuwahamishia huko. Ziwape elimu ya ujasiriamali na wasajiliwe kuwa walipa kodi rasmi.

Mama nimeamua kukwambia maneno haya kwa sababu mimi nawaogopa. Nikijaribu kuwapa mchanganuo huo bila shaka watanipoteza kwa kuitia mchanga keki yao, maana wanachoonekana kukiendesha ni kuhalalisha makosa ili wapite humohumo kudai mlungula na fadhila.

Kumbe wangesimamia haki kusingekuwa na mazoezi ya kupindua meza wa wachuuzi na kupora makarai ya wachemsha mihogo bila huruma.

Leo nisikuchoshe maana najua una majukumu mazito ya kuliongoza Taifa hili. Ila naomba usinichoke kwa sababu watu wetu wanabadilika kama vinyonga, ukimgusa kwenye hili anajificha kwenye jingine. Lakini maadamu nimepata uchochoro wa kukufikia moja kwa moja, naamini mbio zao zitaishia ukingoni.
Mama mimi narudi zangu mtaani kwa walalahoi wenzangu, lakini nitakuja tena Jumatano ijayo kukwambia mazito zaidi na hata majina ya wahusika nitakupatia.