Operesheni +255 Katiba Mpya yahitimishwa, mikutano zaidi ya 100

Muktasari:

  • Operesheni +255 Katiba Mpya ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Magharibi yenye mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora iliyozinduliwa Mei 17, 2023 imehitimishwa leo Jumatatu, Mei 29, 2023 huku mikutano zaidi ya 100 ikiwa imefanyika.

Tabora. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimehitimisha Operesheni +255 Katiba Mpya Kanda ya Magharibi kwa kufanya mikutano ya hadhara zaidi ya 100 katika kata za majimbo 25 ya mikoa hiyo ya Kigoma, Tabora na Katavi.

 Operesheni hiyo iliyofanyika kwa siku 14 kuanzia Mei 17, 2023 ilianzia mkoani Kigoma kisha Katavi na kuhitimishwa leo Jumatatu, Mei 29, 2023 wilayani Igunga mkoani Tabora ambapo ilihudhuriwa na mamia ya wakazi wa wilaya hiyo.

Katika operesheni hiyo, kulikuwa na timu mbili ambapo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alikuwa na Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar, Salum Mwalimu na timu ya pili ilikuwa na Makamu Mwenyekiti-Bara, Tundu Lissu pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika.

Timu hizo zilikuwa zikifika mkoa mmoja, wanafanya mkutano wa hadhara wa pamoja kisha wanagawanyika kwa kwenda kwenye kata na majimbo ya mkoa husika.

Akihitimisha operesheni hiyo, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe aliwaeleza wananchi wa Igunga baada kuachiwa kutoka gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam, Machi 4, 2022 alikutana na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu ya jijini humo na kumweleza mbinu za kuwaongoza Watanzania kwa amani.

Mbowe alisema alifikia uamuzi huo baada ya kubaini Serikali iliyoko madarakani imekosa uhalali wa wananchi hivyo kuwaongoza inahitaji mkakati maalum ambao ni pamoja na kutafuta maridhiano.

Mwanasiasa huyo mkongwe alisema miongoni mwa mambo aliyoteta na Rais Samia ni pamoja na umuhimu wa kufumua Katiba iliyopo na kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya huku akidai anaamini mchakato huo utakamilika kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025.

"Huwezi kuongoza nchi hii kwa amani kwa kufikiria kuwa nchi hii ni CCM pekee ambayo imekosa uhalali mbele ya wananchi kwa hiyo akitaka kuongoza kwa amani aruhusu mawazo kinzani na ndicho alichokifanya," alisema Mbowe

Mbowe alisema Katiba Mpya inayodaiwa na chama hicho siyo mali ya upinzani bali itakuwa na manufaa kwa watanzania wote bila kujali itikadi zao na kuwataka kuuungana na chama hicho kuhakikisha lengo hilo linafikiwa.

"Tumezunguka katika hii mikoa mitatu, timu yangu na timu ya Makamu Mwenyekiti, Tundu Lissu tumebaini changamoto kadhaa ikiwemo miundombinu, utitiri wa kodi, migogoro ya ardhi, hifadhi, uraia, wananchi kutosomewa mapato na matumizi na rushwa katika miradi inayotekelezwa haya yote yatamalizwa na Katiba Mpya," alisema

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema Katiba Mpya itasaidia kutatua changamoto za muungano ikiwemo kufumua muungano wa sasa kutoka muundo wa sierikali mbili hadi tatu ambazo ni Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

"Muungano wa sasa unaikandamiza Zanzibar kwani Tanganyika kuwa wakati inanufaika na muungano wakati Zanzibar hainufaiki. Tunataka Katiba Mpya ili muungano utunufaishe wote, hilo litafanikishwa na Katiba Mpya," alisema Mwalimu

Kwa upande wake, Operesheni Kamanda wa +255 Katiba Mpya wilaya ya Nzega, Secilia Kwayu alimueleza Mbowe miongoni mwa changamoto zilizopo katika wilaya hiyo ni pamoja na eneo la wananchi kutwaliwa na mwekezaji bila kuwalipa fidia huku akimtaka kufikisha kilio chao kwa Rais Samia.

Viongozi hao wa Chadema baada ya kuhitimisha Operesheni +255 Katiba Mpya Kanda ya Magharibi watapumzika kwa mwezi mmoja kisha kuendelea na Operesheni hiyo Julai 2023 katika mikoa ya Kanda ya Victoria inayojumuisha mkoa wa Mwanza, Geita na Kagera.