Rais Samia akutana na Mbowe, Kinana Ikulu Dar

Rais wa Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (kulia) na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana Ikulu jijini Dar es Salaam leo Jumamosi  Desemba 31, 2022.

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan ameufunga mwaka 2022 kwa kukutana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amepokea taarifa ya maendeleo ya mazungumzo ya mchakato wa maridhiano ya kisiasa kati ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Rais Samia amepokea taarifa hiyo kutoka kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana leo Jumamosi Desemba 31, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam.

Hii si mara ya kwanza kwa viongozi wa vyama hivyo kukutana tangu uanze mwaka 2022, ingawa ilikuwa nadra kwa Serikali za awamu zilizopita.

Rais Samia kwa mara ya kwanza, alikutana na Mbowe Machi 4, 2022, Ikulu ya Dar es Salaam saa chache baada ya kuachiwa huru kutoka gerezani alikokaa kwa takriban miezi tisa kwa tuhuma za ugaidi.

Hata hivyo, kikao chao hicho kilifungua milango ya vikao vingine baina ya viongozi wa vyama hivyo vilivyoendelea mara kadhaa, kuyasaka maridhiano ya kisiasa.

Rais wa Samia Suluhu Hassan akiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (kulia) na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana mara baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya mazungumzo ya mchakato wa maridhiano ya kisiasa, Ikulu jijini Dar es Salaam leo Jumamosi  Desemba 31, 2022.

Tume ya watu 10 kutoka Chadema iliundwa, kadhalika idadi kama hiyo kutoka CCM na zilikutana Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma kuanza mazungumzo hayo.

Hatua hiyo ilichukuliwa kama ukurasa mpya na chanya kwa siasa za Tanzania.



Angalau sasa, vyama mbalimbali ikiwemo Chadema vimeonekana vikifanya shughuli za kisiasa mikoani, ikiwa ni dalili ya uwanja huru wa kisiasa tofauti na miama mitano iliyopita.