Prime
Rais Samia anavyoteswa na ‘jini’ la demokrasia Tanzania

Rais Samia Suluhu Hassan
Nianze kwa kumnukuu Rais wa Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, katika kitabu chake “Mzee Rukhsa; Safari ya Maisha Yangu”, ameandika kuwa demokrasia ni jini, ukishalitoa kwenye chupa huwezi kulirejesha.
Nukuu hiyo naitumia kujadili hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan juzi (Septemba 11, 2023), kwenye Mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa na wadau wa demokrasia, Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere.
Hotuba ya Rais Samia, kwa kuitafsiri kuanzia hisia, uso na maneno aliyotumia, ndio Waingereza huita kupumua (breathing fire), kwa maana alizingumza akiwa mwenye ghadhabu.
Rais Samia, hakuwa yule wa Januari 3, 2023, alipoondoa marufuku ya mikutano ya hadhara kwa vyama siasa. Siku hiyo, alizungumza akitabasamu, mithili ya mama anayewanasihi watoto wake.
“Kama waungwana, kama wastaarabu, Watanzania wenye sifa ndani ya dunia hii, niwaombe sana ndugu zangu, ruhusa hii tunaitoa twendeni tukafanye siasa za kistaarabu. Siasa za kujenga, zilizopevuka, sio za kubomoa. Hapa tulipofika tusirudi nyuma,” Rais Samia, Januari 3, 2023.
“Uhuru maoni una ukomo wake, sio tu kisheria hata kibinadamu. Mtu mwenye wazazi, aliyelelewa na kupitishwa kwenye dini, kuna maneno hawezi kutamka,” Rais Samia, Septemba 11, 2023. “Mtu anatukana mpaka unajiuliza, kinywa hichohicho ndicho anapitishia chakula?”
Nukuu za tarehe mbili tofauti, zinamwonesha Rais Samia wa kabla na baada. Kabla, alitoa nasaha kwa imani mithili ya mama anayewapa hamasa wanaye anaowaamini. Baada, ni mlezi aliyechoshwa na vitendo vya watoto aliokutana nao ukubwani.
Hotuba ya Rais Samia juzi, inatoa picha kuwa amekuwa akijizuia mno kutoa kauli kuhusu sakata la bandari ambalo bado halijapoa, vilevile harakati za Katiba. Dhahiri, lugha ambazo hutumika humkwaza, ndio sababu alisema: “Hawana cha kuzungumza ndio maana wanatukana.”
Pengine sasa, anatamani kurudisha tarehe nyuma ili awaze upya kuhusu kuruhusu mikutano ya vyama vya siasa. Bahati mbaya, kwa mzunguko wa kawaida wa sayari, hakuna namna tarehe zinaweza kurudi nyuma.
Kisichopaswa kusahaulika ni kuwa uamuzi wa kuruhusu mikutano ya kisiasa ulikuwa moja ya uamuzi wa busara kufanywa na Rais Samia. Mikutano ya kisiasa ni haki kikatiba na kisheria. Kifungo kilikuwa batili. Ruhusa ilikuwa kurejesha haki. Rais Samia hapaswi kujilaumu kutenda haki.
Demokrasia ni jini
Taifa linaloongozwa kidemokrasia ni bora kwa sababu linatoa taswira kuwa wananchi wote wana haki sawa katika kuchagua viongozi wao. Taifa la kidemokrasia, huonesha kuwa serikali inawajibika kwa wananchi.
Tafsiri hiyo inakuonesha kwamba wananchi ndio mabosi. Serikali, kuanzia rais, mawaziri, wabunge na watumishi wengine wote serikalini ni wafanyakazi wa wananchi. Mwananchi anayeuvaa ubosi na akakosa uungwana, unadhani atatumia lugha gani?
Ikiwa mwajiri wa msaidizi wa nyumbani, aliyekosa uungwana, anaweza kumfanya mfanyakazi wake ajione anaishi jehanamu, vipi huyohuyo akauvaa ubosi mbele ya rais wa nchi yake? Atatumia lugha gani?
Mfumo wa demokrasia ni mchezo wa kushindania madaraka au mashindano ya kisiasa. Chama kinachoongoza dola na vinavyomezea mate dola ni wapinzani. Je, unaweza kutumia lugha gani dhidi ya mpinzani wako?
Anayemezea mate dola, siku zote atatamani aliyeshikilia dola akosee ili iwe faida kwake kisiasa. Akipata fursa ya kumfanya kiongozi aliye madarakani apungukiwe ushawishi, hadhi au hata heshima, ataitumia kikamilifu.
Ufafanuzi, ama uuweke upande wa faida au hasara, hayo ndio matunda ya demokrasia. Rais, pamoja na mamlaka, hadhi, vilevile ukuu wa kikatiba alionao, mbele ya wa wanasiasa wanaomezea mate dola, humwona ni mshindani wao.
Ni kweli nchi inaongozwa kikatiba na rais ndiye mlinzi mkuu wa Katiba. Kwa mantiki hiyo, rais ndiye mkuu wa dola kwa kipindi chake cha kiapo. Hivyo, rais ni mlezi wa taifa, ila sio baba au mama wa raia mmoja-mmoja.
Kama alivyosema Mwinyi, demokrasia ni jini. Ukishairuhusu inakuwa vigumu kuidhibiti. Na kwa kuwa rais hahusiki na malezi ya mtu mmoja-mmoja, jukumu lake linabaki moja tu; kulea, kulinda na kuliunganisha taifa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.
Kwa vile rais hahusiki na malezi ya raia mmoja-mmoja, maana yake anawajibika kulea na kulinda taifa la watu waliopitia malezi na ukuaji wa tofauti. Na hiyo ni moja ya gharama za urais katika nchi ya kidemokrasia.
Wito wa juu kabisa kwa rais kwenye nchi ya kidemokrasia ni yeye kuwa mvumilivu kuliko wapinzani wake. Aoneshe ukomavu na ustahimilivu zaidi ya wengine. Adhihirishe kiwango cha juu cha uungwana wa kisiasa. Awe na kifua kipana cha kupokea na kusamehe.
Rais katika nchi ya kidemokrasia, anapaswa kuwa na kauli thabiti. Anaposema anaruhusu mikutano, hapaswi baada ya muda akereke na kuifuta. Hiyo itadhihirisha woga wake. Rais anatakiwa kuwa na ngozi ngumu, yenye kumwezesha kupokea mishale pasipo sumu kupenya kwenye moyo na ini.
Hotuba ya Rais Samia, inampambanua kuwa mwenye matamanio hadi ya malezi ya Watanzania. Jinsi alivyokuzwa kimaadili, akapitishwa madrasa kusoma dini, akafunzwa ustaraabu wa kuishi na jinsi ya kudumisha uhusiano wa kijamii, anatamani iwe hivyo kwa kila Mtanzania.
Hiyo ndio sababu anashangazwa na anaowasema wanatukana. Tena, inaonekana wanamuumiza. Bahati mbaya, Tanzania ni taifa mchanyato (diverse). Ni mchanganyiko kuanzia jamii za makabila, dini tofauti, madhehebu mbalimbali, wapagani hadi chimbuko la vizazi.
Pamoja na nadharia kuwa Watanzania ni watu wema ila si wakati wote ustaarabu wako unaweza kufanana na wa mwingine. Yupo aliyekuzwa kufokeana na yeyote bila kujali umri. Mwingine alilelewa kwa kuendekezwa hata alipotukana wazazi wake.
Tanzania ni moja; watu wanaua wengine. Matukio ya ubakaji hayajakauka. Watoto wanapiga wazazi wao. Walemavu wa ngozi wanauawa na kukatwa viungo. Ujambazi wa kutumia silaha upo. Rushwa na ufisadi vimeweka makazi ya kudumu. Matendo yote hayo yanafanywa na Watanzania.
Tafsiri kuwa Watanzania ni watu wema haina maana kuwa wote ni watenda mema. Ndio maana sheria zimetungwa, mamlaka za ulinzi, usalama na utoaji haki zimewekwa. Kuna vituo vya polisi hadi magereza.
Najaribu kumkumbusha Rais Samia kuwa hulka hadi za uovu zimo Tanzania, sembuse zile za kupishana na kukoseana adabu. Anachopaswa ni kujielekeza katika kuongoza nchi kwa kuacha mifumo ifanye kazi. Kama ni sheria, ichukue mkondo wake.
Urais ni wajibu mgumu kwenye nchi ya kidemokrasia. Unatakiwa uwaelewe wote, wanaokupenda na wanaokuchukia. Wanaokusifia na wanaokukosoa. Wanaokupamba na wanaokuponda.
Halafu sasa, hupaswi kuwapendelea wanaokupenda au kuwabagua wanaokuchukia. Ule msemo ukubwa ni jalala unakubalika zaidi kwa rais wa nchi ya kidemokrasia. Rais Samia atambue kwamba yeye ni jalala.
Elimu kutoka Marekani
Machi 12, 2017, Rapa wa Marekani, Cordozar Calvin Broadus, Jr ‘Snoop Dogg’, alitoa wimbo unaoitwa Lavender (Nightfall Remix) ambao maudhui yake ni kutetea jamii ya Wamarekani weusi dhidi ya Serikali ya Marekani.
Snoop Dogg anaimba kuwa polisi wa Marekani na serikali yote ni adui wa Wamarekani weusi. Wimbo unatoa ahadi kuwa wote wenye kuwakandamiza Wamarekani weusi, usiku ukifika ndiyo itakuwa tamati yao kwa sababu wanastahili pigo la bunduki.
Katika video ya wimbo huo, kipande cha mwishoni kinachoonesha usiku umefika kwa ajili ya kutimia kwa hukumu ya bunduki, yupo mtu amevalishwa wajihi na sura ambavyo vinamfanya afanane na kibonzo cha Rais wa 45 wa Marekani, Donald Trump. Wakati huo, Trump alikuwa hajafikisha hata miezi miwili madarakani.
Ndani ya video hiyo, huyo mtu aliyetengenezwa kufanana na kibonzo cha Trump, anatambulishwa kwa jina “Ronald Klump”, badala ya Donald Trump, kisha anashikiwa bastola na Snoop, kuonesha kuwa tayari muda wake umefika.
Video ya wimbo huo ilitoka Machi 12, siku tatu baadaye, yaani Machi 15, 2017, Trump aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kupitia akaunti yake rasmi ya @realDonaldTrump kumshambulia Snoop.
Trump aliandika: “Unaweza kufikiri mayowe yangekuwaje kama Snoop Dogg, aliyeshindwa kisanii na kila kitu, angedhamiria kumlenga na bunduki Rais Obama? Muda wa jela.”
Tafsiri ni kuwa Trump anaamini kuwa Snoop angemfanyia kitendo hicho cha kumdhihaki kwa bunduki mtangulizi wake, Barack Obama, vilio vingekuwa vingi, hivyo akaahidi kumtupa jela mwanamuziki huyo.
Maneno hayo ya Trump kwenye Twitter dhidi ya Snoop, ndiyo ambayo yaliamsha hisia kali kutoka kwa wanamuziki wa Rap Marekani, waliomshambulia Rais wao kuwa anatakiwa kumwacha mkongwe huyo wa Rap.
Uhuru wa kujieleza kwa Marekani upo juu mno, kwa hiyo kitendo cha Trump kumjibu Snoop kwa kitisho, kilisababisha wanamuziki wengine wa Rap wamshambulie kwa lugha isiyo na staha wala angalizo kuwa huyo ni rais wao.
Wanamuziki wa Rap, Shad Gregory Moss ‘Bow Wow’ na Clifford Joseph Harris Jr ‘T.I’, waliongoza kundi kubwa la jamii ya muziki wao kumshambulia Trump bila staha wala hofu.
Kilichomtesa Trump ni kutotambua kuwa taifa lao limeshapiga hatua kubwa mno katika uhuru wa maoni. Marekani, rais pamoja na kupewa ulinzi mkubwa, maisha yenye hadhi ya juu kabisa na kadhalika, lakini anatambulika kuwa ni mtumishi wa watu.
Tanzania bado inahangaika na akina Nay Wamitego na Roma Mkatoliki kwa nyimbo zao za ukosoaji. Waachwe watu wakosoe. Wanaotukana, sheria za jinai zichukue mkondo wake.
Wanaotumia lugha mbaya, Watanzania sio wajinga, lakini mwisho wa siku siasa za kistaarabu zitawale.