Prime
Simulizi ya saa 24 kabla ya kifo cha Sokoine
Imepita miaka 40 tangu aliyekuwa Waziri Mkuu, hayati Edward Sokoine alipofariki kwa ajali ya gari mkoani Morogoro wakati akitoka mkoani Dodoma kuelekea Dar es Salaam.
Sokoine alifariki Aprili 12, 1984 baada ya gari lake kugongwa na gari lingine katika eneo la Dakawa, Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro.
Sokoine anatajwa kuwa miongoni mwa viongozi walioonyesha uwezo wa hali ya juu kwa kutatua kero za wananchi na kutafuta suluhu kwa mambo magumu yaliyoikabili nchi.
Mapema wiki hii, kitabu cha “Edward Moringe Sokoine, Maisha na Uongozi Wake” kilizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Kitabu hicho cha tawasifu ya maisha yake, kimeandikwa na Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua).
Makala haya yanachambua maisha ya kiongozi huyu kama yalivyosimuliwa kwenye kitabu hiki, ikiwemo uongozi wake, haiba yake, uamuzi alioufanya na hata kifo chake kilivyotokea na kusababisha majonzi kwa Watanzania.
Kifo chake
Kitabu hicho kinaeleza mazingira ya kifo cha Sokoine siku moja kabla ya ajali aliyoipata, kikisema alikataa usafiri wa ndege aliokuwa anaupendelea.
“Aprili 11, 1984, siku moja kabla ya kifo chake, mlinzi na mpambe wake Sokoine, Amaan Abihudi Luila, alimweleza Waziri Mkuu kuwa ilikuwapo ndege ya kumrudisha Dar es Salaam kama alikuwa anapendelea usafiri huo.
“Sokoine, baada ya kuelezwa kuwa ndege hiyo ilikuwa na uwezo wa kubeba watu saba, aliuliza kama angepanda ndege hiyo, wasaidizi wake ambao alikuwa amekwenda nao Dodoma wangerudi vipi Dar es Salaam?
“Alisisitiza kuwa angetaka timu yake irudi pamoja Dar es Salaam kama ilivyokuwa imekwenda Dodoma. Ilikuwa kawaida ya Sokoine kuwatetea wasaidizi wake na siku hiyo utetezi ulihusu maofisa wake wengine watano ambao alisafiri nao kwa njia ya barabara kwenda Dodoma kutoka Dar es Salaam, Aprili 8, 1984.”
Kitabu hicho kinaeleza kuwa ilikuwa Aprili na ilikuwa nyakati za masika, hivyo mvua ilinyesha usiku kucha Dodoma, kuanzia saa 4 usiku, ikiwa imeambatana na ngurumo za radi, kama ilivyokuwa kwa nchi nzima.
“Mvua ile ilikuwa bado inaendelea kunyesha wakati safari ya Waziri Mkuu inaelekea Dar es Salaam. Sokoine hakujali hayo. Pamoja na mvua hiyo kubwa, saa 2 kamili za asubuhi, msafara wake uliingia kwenye lango kuu la nyuma la ofisi yake mjini Dodoma.”
Kitabu hicho kinaeleza kuwa pamoja na mvua iliyokuwa ikinyesha, Sokoine alikwenda ofisini katika jengo la Old Boma, eneo la Uzunguni, karibu na Dodoma Hotel, kama ofisi yake.
Kitabu hicho kinasimulia kwamba kama ilivyokuwa kawaida yake, baada ya kuingia ofisini kwake, alikagua majalada na kufanya mashauriano na wasaidizi wake. Saa 4:30 asubuhi, alitoka nje ya jengo la ofisi yake na kumkuta mmoja wa wasaidizi wake, Horace Kolimba (sasa marehemu), kwa masihara, alimkaribisha aingie kwenye gari lake ili wasafiri kwa pamoja kurudi Dar es Salaam.
“Kwa heshima, Kolimba akamjibu Sokoine kuwa yeye angesafiri baadaye jioni kwa ndege. Hayo ndiyo yalikuwa maneno ya mwisho ya Sokoine kwa msaidizi wake yeyote, kwa sababu baada ya hapo msafara ulitimka kuelekea Dar es Salaam.
“Lakini kabla ya kuanza safari yake kuelekea Dar es Salaam, Sokoine alikutana pia na Mawaziri wa Nchi (watatu) katika Ofisi ya Waziri Mkuu - Paul Kimiti, Gertrude Mongella na Anne Makinda.
Alifanya kikao cha mapitio ya kazi za Serikali na Bunge kwa siku nne alizokuwa Dodoma. Sokoine aliwapitisha mawaziri hao kwenye muhtasari wa mambo muhimu aliyotaka yafanyike baada ya Bunge.”
Pia, alikutana na watu mbalimbali, ikiwa pamoja na kufanya karamu na wabunge mkoani humo.
Ufafanuzi wa Mwanga kuhusu yaliyotokea katika safari ya kwenda Da es Salaam hautofautiani na ule wa Chiledi, ambaye kama alivyo Mwanga alikuwa ni mtu wa lazima kuwapo katika kila msafara wa safari za Wazi Mkuu.
Safari yaishia Wami
Kwa mujibu wa aliyekuwa mwandishi wa Soikoine, Accadoga Chiledi, mwendo wa magari yaliyoandamana katika msafara wa kiongozi huyo ulikuwa wa kawaida, kati ya kilomita 110 na 130 kwa saa kwa sehemu zilizonyooka.
“Chiledi alikaa katika gari lake la kawaida mbele ya lile la Waziri Mkuu. Gari lililotangulia, la kusafisha njia, lilikuwa la Jeshi la Polisi, aina ya Peugeot 504, likifuatiwa na gari la maofi wa usalama, na la tatu lilikuwa ni la Waziri Mkuu, Mercedes Benz. Baada ya gari la Waziri Mkuu likafuata gari jingine la maofisa wa usalama, baadaye gari la wasaidizi wengine, akiwamo Mwanga.
Chiledi anaongeza, “Hata hivyo, dakika tano baada ya kuvuka Mto Wami, kiasi cha kama kilomita 40 hivi kutoka Morogoro, nilisikia kishindo kikubwa kikitokea nyuma yetu, kishindo cha mgongano wa vyuma.
“Gari la Waziri Mkuu lilikuwa limegongana na gari aina ya Toyota Landcruiser la kubeba mizigo. Sokoine hakuchukua muda.
“Alipoteza maisha muda mfupi tu baadaye kutokana na majeraha makubwa ambayo alikuwa ameyapata ya kichwani na kifuani.”
Aanza na Katiba mpya
Sokoine aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu siku nane tu baada ya vyama vya TANU na ASP kuunganishwa na kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM).
Aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu kwa mara ya kwanza mwaka 1977 na alidumu hadi mwaka 1980, akajiuzulu na baadaye aliteuliwa tena mwaka 1983 hadi alipofariki mwaka 1984.
Kuunganishwa kwa vyama hivyo kulienda sambamba na mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambayo ndiyo inaendelea kutumika nchini hadi sasa.
Katiba hiyo iliyopitishwa Aprili 26, 1977, siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, pia ilichukua nafasi ya Katiba ya Muda ya Tanzania ya mwaka 1965.
Kitabu hicho kinaeleza kuwa uongozi wa Sokoine ulijitokeza katika usimamizi wake wa kupitishwa kwa Katiba hiyo.
“Katiba hiyo kimsingi ndiyo iliyoimarisha kwa vitendo mfumo na nadharia ya Chama Kushika Hatamu za Uongozi wa nchi, na nafasi ya CCM katika maisha ya Watanzania.
“Katiba hiyo ya 1977 pia ndiyo iliyoondoa utata wa kuwapo kwa vyama viwili vya siasa. Kwa mara ya kwanza tangu Muungano, nchi sasa ilikuwa kweli na chama kimoja cha siasa kufuatia kuungana kwa vyama vya TANU na ASP miezi miwili kabla ya kupitishwa kwa Katiba mpya ya mwaka 1977. Aidha, hatua ya kuunganisha vyama hivyo iliimarisha Muungano,” kinaeleza kitabu hicho.
Vita vya Idd Amin
Mafanikio mengine ya Sokoine yanayotajwa katika kitabu hicho ni uongozi na usimamizi wake wa vita dhidi ya Idi Amin vya kukomboa sehemu ya Tanzania iliyovamiwa na mtawala huyo wa Uganda.
“Sokoine alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Vita wakati huo. Vita vinahitaji mchango wa watu wengi na hakuna shaka kuwa watu wengi nchini walichangia mafanikio ya Tanzania katika ushindi huo.
“Hata hivyo, ushindi huo usingepatikana bila uongozi thabiti wa Sokoine katika vita hivyo. Nyerere alitambua mchango wa Sokoine katika barua ambayo alimwandikia Waziri Mkuu akimkubalia ajiuzulu Uwaziri Mkuu mwishoni mwa mwaka 1980.
“Baada ya kummiminia sifa nyingi za uongozi, Nyerere alimwambia Sokoine, ‘Ni lazima nitaje, kwa namna ya pekee, kazi uliyoifanya katika kuendesha na kuratibu juhudi za taifa letu wakati tulipolazimishwa kuingia vitani; binafsi ulitoa mchango mkubwa katika ushindi wetu wa mwisho na mchango wako ni lazima utambuliwe hadharani’.”
Vita dhidi ya uhujumu uchumi
Sokoine pia aliingia madarakani kwa nyakati zote mbili wakati Tanzania inapitia kipindi kigumu kiuchumi. Baada ya kupitishwa Sheria ya Uhujumu uchumi, ukamataji ulianza hata kama ilikuwa katika mazingira ya siri.
Kamatakamata ilikwenda kwa kasi sana na Hamad Rashid ananukuliwa kwenye kitabu hicho akisema katika kipindi kifupi, watu wapatao 3,000 walikuwa wametiwa ndani, mali nyingi za mamilioni ya fedha zilikamatwa na vyombo vya Serikali na nyingine hata kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
Akimwelezea Sokoine katika mkutano wa uzinduzi wa kitabu chake Septemba 30, 2024, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba anasema Sokoine alisimamia uanzishwaji na utekelezaji wa Sheria ya Uhujumu uchumi ambayo kwa maoni yake aliona kuwa inaweza kuleta shida.
“Alisema kesi za uhujumu ya uchumi zisikilizwe katika Mahakama maalumu, halafu ushahidi wa kusikia uchukuliwe, kesi zisikilizwe faragha na kusiwe na dhamana,” anasema.
Hata hivyo, Jaji Warioba anasema alipinga sheria hiyo akisema inakiuka utawala bora na haki za binadamu.
“Nikamwambia, mimi kwa kuwa ni Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu, siwezi kusimamia sheria ambayo siiamini. Kwa hiyo nikamwambia Mheshimiwa Waziri Mkuu, mimi nitakaa pembeni,” anasema.
Hata hivyo, alisema Sokoine hakupenda msimamo wake. “Akaniambia wewe umekuwa mstari wa mbele kupambana na rushwa, unataka kuacha kazi kwa jambo dogo hili?
“Nikamwambia hapana, sheria zozote zinazotekelezwa kwa operesheni zinakuja kuleta madhara makubwa baadaye na kwa sheria hii, italeta madhara na inavunja utawala bora na inaingilia haki za binadamu,” anasema Jaji Warioba.
Anaendelea kusimulia kuwa Sokoine alimchukua hadi Msasani kwa Mwalimu Julius Nyerere kutaka ushauri.
“Mwalimu akaamua nusunusu, akasema nendeni mkaondoe hiyo ya kesi kusikilizwa faragha na hiyo ya hearsay evidence (ushahidi wa kusikia), lakini utaratibu maalumu ubaki na dhamana isiruhusiwe na akasema hakuna mtu ku-resign (kujiuzulu) hapa,” anasema.
Anasema sheria hiyo ilipitishwa Aprili 1983 na Nyerere aliisaini haraka haraka.
“Yaleyale niliyokuwa naogopa yakaanza kutokea, kwa sababu utekelezaji wake ulikuwa na vurugu kubwa. Watu walianza kukamatwa kwa taratibu mbaya, mali za watu zilichukuliwa na malalamiko ya wananchi yalikuwa mengi sana,” anasema.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Jaji Warioba, baadhi ya watendaji wa Serikali waliosimamia operesheni ya uhujumu uchumi walikwenda kinyume na maelekezo, jambo lililomsikitisha Sokoine.
Kwa mujibu wa kitabu hicho, Sokoine hakuwa na ugomvi na ubepari na mabepari kwa sababu aliweka tofauti kati ya mabepari “waaminifu” ambao kazi yao ilikuwa kushiriki katika uzalishaji na shughuli halali, na walanguzi na wahujumu uchumi waliojipatia mali kwa njia za ulanguzi na uhujumu uchumi.
“Wakati ule wa vita dhidi ya uhujumu uchumi, Sokoine alitamka hadharani kuwa chama na Serikali havikuwachukia matajiri, bali kuwa kilichotakiwa ni watu kutajirika kwa njia halali za uzalishaji mali.
Katika moja ya kauli zake, Sokoine alitoa changamoto za matatizo akisema: “Watuambie nani katika Tanzania amenyang'anywa ardhi yake, mifugo yake na kadhalika.”
Ilikuwa vigumu kwa Sokoine, kwa hakika, kutokuamini katika miliki binafsi ya mali kwa kuzingatia kuwa, licha ya kukadiriwa kuwa na ng'ombe kati ya 500 na 600, pia alimiliki maeneo makubwa ya ardhi.
Katika kitabu hicho, Profesa wa Sheria, Issa Shivji, mmoja wa wasomi na wachambuzi hodari wa mambo nchini, anasema kuwa Sokoine hakuwa na ugomvi kuhusu ubepari kwa maana ya ubepari au kuhusu mabepari kama tabaka ndani ya jamii.