Ujio wa Kamala ni ishara ya kukua kwa demokrasia

Robert Mugabe, Rais wa zamani wa Zimbabwe, kupitia kitabu chake “Julius Nyerere, Asante Sana” ameacha ujumbe unaoweza kuutafsiri kama wosia kwa Afrika. Maudhui ya kitabu ni kueleza kinagaubaga mchango wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwa ukombozi wa Zimbabwe na bara la Afrika. Katika kitabu hicho, Mugabe aliandika kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa na maono ya mbali kuhusu ukombozi.

Aliwaonyesha wanaharakati waliokuwa wanapigania uhuru wa nchi za Afrika kuwa wangeweza kupata marafiki wa kuwaunga mkono hata nje ya bara hili.

Mugabe amesimulia kwenye kitabu kuwa Mwalimu Nyerere alitumia uhusiano wake mzuri na China kuwaunganisha wanaharakati wa ukombozi Afrika na taifa hilo la Mashariki. Kisha Afrika yote ikawa rafiki wa China.

“Baadaye nikaja kugundua kuwa China ni rafiki mzuri sana. Magharibi watajifanya rafiki, watataka manufaa, Magharibi wataadhibu lakini tazama Mashariki, ni rafiki ambaye anajiona yupo sawa nawe,” aliandika Mugabe.


Baada ya muhtasari

Leo, Tanzania inampokea Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris. Mwanamke wa kwanza kushika ofisi namba mbili Marekani, anazuru taifa linaloongozwa na mwanamke wa kwanza kuongoza ofisi namba moja.

Kamala, mbali ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya juu zaidi Marekani, vilevile ameweka rekodi ya kuwa Mmarekani wa kwanza mwenye asili ya Afrika kuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo. Sasa, ofisi za juu zaidi Marekani zimewahi kushikwa na watu weusi, Rais wa 44, Barack Obama na Kamala.

Ziara ya Kamala Tanzania ina tafsiri nyingi anuwai. Ya kwanza kufunguka kwa anga la kimataifa. Rais Samia amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuishawishi dunia kwamba sasa Tanzania haiendeshwi kidikteta na ni sehemu salama zaidi.

Mtazamo wa jumuiya za kimataifa, kipindi cha uongozi wa Rais wa Tano, Dk John Magufuli, ni kuwa nchi ilikuwa kwenye makucha ya uongozi wa kiimla. Shughuli za kisiasa zilifungiwa, demokrasia ikawekwa korokoroni. Uhusiano wa kidiplomasia ukadorora.

Kamala anakuja nchini kipindi ambacho mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa imefunguliwa. Mchakato wa mabadiliko ya sheria nyingi kandamizi ukiendelea. Miongoni mwa sheria kandamizi ni ya takwimu na huduma za vyombo vya habari. Pili, ni kuendelea alipoishia Rais mstaafu, Jakaya Kikwete. Tanzania kabla ya Magufuli ilikuwa kwenye uhusiano mwema na jumuiya za kimataifa. Tangu wakati wa Mwalimu Nyerere, ukastawi zaidi kipindi cha Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa na Kikwete.

Mkapa akiwa Rais, aliyekuwa Rais wa Marekani, Bill Clinton, alitembelea Tanzania. Wakati wa Kikwete, marais wawili wa Marekani waliokuwa madarakani, George W. Bush na Obama, walizuru Tanzania kikazi.

Kipindi cha Magufuli, ndicho ambacho hakuna kiongozi yeyote wa juu wa Marekani, aliyetembelea Tanzania. Rekodi hiyo ni sawa na ile ambayo iliwekwa na Rais wa Pili, Ali Hassan Mwinyi, kati ya mwaka 1985 mpaka 1995.

Wakati wa Nyerere, pamoja na ziara yake ya kihistoria Marekani, alipokutana na Rais wa 35 wa nchi hiyo, John Kennedy, White House, Julai 15, 1963, vilevile kipindi cha uongozi wake, alipokea mawaziri wa mambo ya nje wawili, waliofika Ikulu, Dar es Salaam.

Henry Kissinger ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, aliyeweka rekodi ya kuwa kiongozi wa juu wa kwanza wa nchi hiyo kufanya ziara Tanzania. Kipindi cha Nyerere, Kissinger alifanya ziara Tanzania mara tatu ndani ya mwaka mmoja (1976).

Cyrus Vance ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani wa pili, kufanya ziara Tanzania. Ilikuwa Aprili 13 mpaka 16, 1978. Baada ya hapo ilipita miaka 18, alipofanya ziara Tanzania, Madeleine Albright, Agosti 18, 1996.

Albright alizuru Tanzania mara ya pili, Oktoba 21, 1999, alipokuja kwa ajili ya kumwakilisha Bill Clinton kwenye shughuli ya mazishi ya Mwalimu Nyerere, ambaye alifariki dunia Oktoba 14, 1999, London, UK.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Condoleezza Rice, alitembelea Tanzania mwaka 2008, alipoongozana na Rais Bush, vilevile mwaka 2011, Hillary Clinton, alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa mwisho wa nchi hiyo kuzuru Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa muktadha huo, ujio wa Kamala ni kipimo kuwa uhusiano wa Tanzania na Marekani umerejea kwenye hali yake ya kawaida. Kipindi cha Magufuli, uhusiano ulikuwa na sintofahamu kiasi ambacho Marekani ilikata misaada kutoka mfuko wa changamoto za malengo ya milenia, vilevile kumpiga marufuku aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda, kutembelea nchi hiyo.


Air Force Two Tanzania

Ujio wa Kamala, unakwenda kufungua ukurasa mpya kwa ndege ya Makamu wa Rais wa Marekani, Air Force Two, kutua Tanzania. Ndege ya Rais wa Marekani, Air Force One, imeshatua Tanzania mara tatu. Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), mara mbili. Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), mara moja.

Kwa mantiki hiyo, Air Force Two, itakapotua JNIA, Dar es Salaam, leo, itaweka rekodi kwa Makamu wa Rais wa Marekani aliye ofisini kutua Tanzania kwa mara ya kwanza. Marais na mawaziri wa Marekani walishafanya ziara Tanzania. Hii ni mara ya kwanza kwa Makamu wa Rais. Kamala anatarajiwa kufanya ziara ya siku mbili, keshokutwa (Machi 31), atapaa kwenda Zambia kabla ya kurejea Marekani, Aprili Mosi. Kwa mantiki hiyo, Air Force Two itaegeshwa JNIA kwa takriban saa 48. Hili si jambo dogo.

Moja ya agenda za ziara ya Kamala Afrika ni kuhamasisha uongozi wa wanawake. Bila shaka, imeipendeza Marekani kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais wa nchi hiyo, kuitembelea Tanzania kwa sababu inaongozwa na mwanamke, Rais Samia.

Kwa mantiki hiyo, wanawake kupitia ngano yao ya “jeshi kubwa”, wana kila sababu ya kutambia ujio wa Kamala. Nchi yao inaongozwa na mwanamke na mgeni wake, inawezekana ndiye binadamu mwenye jinsia ya kike aliye na ushawishi mkubwa kuliko yeyote duniani hivi sasa.


Tafsiri ya Kamala Afrika

Zama za taifa moja kutawala nchi nyingine kijeshi zimepitwa na wakati. Anguko la Dola za Papa (Papal States), Karne ya 19 na sehemu kubwa ya dunia kujipatia uhuru Karne ya 20, ziliibua zama mpya za utawala wa hiari (co-opt) badala ya coerce (shuruti). Hizi ni zama za teknolojia ya habari. Ubabe wa kidola unapaswa kuundwa na mamlaka ya laini (soft power), kwamba nchi yenyewe inavutiwa kukimbilia upande fulani kwa sababu za kimasilahi. Kivutio cha soft power kinaweza kuwa utamaduni, misingi ya kisiasa na sera za kimataifa.

Kiwanda cha muziki na maisha ya Hollywood, kwa miaka mingi, yalifanya utamaduni wa Marekani, kujenga athari kubwa duniani. Vivyo hivyo, sera zake za mambo ya nje na mifumo yao ya kidemokrasia, vimekuwa kielelezo cha ustaarabu wa kidunia. Hiyo ndio soft power.

Eneo la sera za mambo ya nje, hugusa pia jinsi ambavyo taifa hilo hushirikiana na mataifa mengine madogo. Hata sasa, zipo nchi zinajiona si lolote mbele ya Marekani. Kauli ya Marekani ndio msimamo wao.

Hayo ni matokeo ya soft power. Mwishoni mwa Karne ya 20, China ilianza kupenyeza ushawishi wa mamlaka laini Afrika. Hadi kufikia sasa, mataifa mengi Afrika, maendeleo yao ya miundombinu na biashara, kwa kiasi kikubwa yanategemea taifa hilo kubwa la Mashariki.

Waafrika wanavaa kutoka China, wanajenga reli za standard gauge, madaraja na barabara kupitia utaalamu na wataalamu wa nchi hiyo. Malighafi nyingi zinatoka China. Umefikia wakati mbao zinatoka Afrika zinapelekwa China, kisha Waafrika wananunua samani za ndani, milango na madirisha kwa bei kubwa kutoka China.

Ukirejea nadharia ya “hegemony”, yaani dola moja kuwa kiranja wa dunia, maana yake utawala wa China Afrika, unaifanya Marekani kupoteza turufu yake ya kiushawishi. Taratibu, ile jeuri yao ya kujiita “the super power”, inaondoka.

Mchuano wa kuwa dola kiongozi duniani kwa sasa upo China na Marekani. Ndio sababu, ziara ya Kamala Afrika, moja kwa moja imekuwa ikichambuliwa kama sehemu ya jitihada za Marekani kujiimarisha Afrika na kupunguza msuli wa China kwenye bara hili.

Desemba mwaka jana, Rais wa Marekani, Joe Biden alialika mataifa 49 ya Afrika katika kongamano la ushirikiano wa Marekani na Afrika (US-Africa Leaders Summit). Lilikuwa kongamano la siku tatu, lililohusu demokrasia, ushirikiano wa kibiashara, usalama wa chakula na athari za Covid-19. Agenda nyingine ya siri ilikuwa ushawishi wa China kwa Afrika.

Ipo hoja ya baadhi ya nchi za Afrika kuelemewa na mzigo wa madeni kutoka China, yenye masharti magumu. Marekani inataka kuyasaidia mataifa hayo dhidi ya China. Ghana na Zambia, zimekuwa kwenye wakati mgumu wa kiuchumi na madeni, ziara ya Kamala kwa nchi hizo, inaelezwa ni kujadili jinsi ya kuzinusuru na China.

Tanzania, yenyewe inaelezwa kuwa imepata ugeni wa Kamala kwa sababu ya mkazo wa uongozi wa mwanamke na uungaji mkono wa Marekani, kwa jinsi Rais Samia, alivyoibadili nchi kwenye uelekeo wa kidikteta hadi kidemokrasia.