Ujumbe wa Sugu kwa Rais Samia, Polisi

Muktasari:

Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Jospeh Mbilinyi maarufu Sugu amempongeza Rais Samia kwa uamuzi wa kuruhusu mikutano ya hadhara huku akisema uamuzi huo pamoja na mengine yanaoendelea kufanyiwa kazi ni lazima yapelekwe bungeni na kupitishwa kuwa sheria.




Musoma. Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Jospeh Mbilinyi maarufu Sugu amempongeza Rais Samia kwa uamuzi wa kuruhusu mikutano ya hadhara huku akisema uamuzi huo pamoja na mengine yanaoendelea kufanyiwa kazi ni lazima yapelekwe bungeni na kupitishwa kuwa sheria.

Sugu ameyasema hayo leo Jumapili Januari 22, 2023, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Shule ya Msingi Mukendo mjini Musoma, Mkoa wa Mara.

Amesema endapo mambo hayo yasipopelekwa bungeni na kupitishwa kuwa sheria upo uwezekano wa mambo yaliyotokea katika kipindi cha miaka saba iliyopita kujirudia.

"Tumeteseka sana, tumekamatwa na kupelekwa magerezani, wafanyabiashara wamelia sasa ili haya yasijirudie lazima haya mambo yaende bungeni na kuwa sheria rasmi," amesema

Kuhusu mikutano ya hadhara, Sugu amesema baada ya mikutano hiyo kuruhusiwa wapo baadhi ya watu waliowabeza kuwa hawana hoja zozote na kusema wanazo hoja nyingi na hoja ya kwanza ni kupunguzwa kwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kutoka asilimia 18 hadi asilimia 10.

Amesema kodi hiyo ikipunguzwa watu wengi watalipa kodi kwa hiari na Serikali kupata mapato zaidi kuliko sasa ambapo kodi hiyo inalipwa na watu wachache huku wengi wakikwepa.

Amesema hoja nyingine ni umiliki wa ardhi ambapo kutokana na kuwa sheria ya Tanzania inatamka kuwa ardhi ya Tanzania inamilikiwa na Rais watanzania wengi wameshindwa kutoka katika umasikini pamoja na kuwa wanamiliki ardhi.

"Tunataka katiba itamke rasmi ardhi inamilikiwa na mtu binafsi na hii itasaidia mmiliki wa ardhi kuitumia kwaajili ya uwekezaji tofauti na sasa kwani wengi wanashindwa kutumia ardhi hiyo kwaajili ya maendeleo yao kwani muda wowote wana weza kunyang'anywa ardhi yao.

Ametolea mfano wa wakulika wa mpunga Mbarali ambao waliwekeza kwa kufungua viwanda kupitia mikopo waliyopata kutoka taasisi za fedha lakini hivi sasa wanatakiwa kuondoka bila kujali gharama walizotumia na namna watakavyo rejesha mikopo yao.

Sugu pia amelipongeza jeshi la polisi kwa utendaji wao wa kazi na kusema tangu jana Jumapili, mkoani Mwanza polisi wamekuwa vizuri hadi leo Musoma na kuongeza watahakikisha wanapigania maslahi ya askari.

"Tunasema we need police service na sio police force, polisi nyie ni washikaji zetu hapa katikati tuliacha kuwatetea kutokana na kukabana na ninyi ila kuanzia sasa maslahi yenu ni moja ya ajenda zetu kwenye majukwaa,” amesema

Katika hatua nyingine Sugu ametumia mkutano huo kukumbushia enzi zake za usanii kwa kuimba na kuwapagawisha watu waliohudhuria mkutano huo.

Amesema kipindi cha nyuma aliamua kusitisha kuimba akiwa jukwaani kwa masuala ya kisiasa kwa maelezo hakuwa na furaha kutokana na mambo yaliyokuwa yakiendelea ikiwepo kuzuiliwa kwa mikutano ya hadhara.

"We need to celebrate niga hapa kati tumepitia magumu sana, kwasasa nitakuwa napiga nondo na kuchana lazima tusherehekee" amesema.