UVCCM Arusha wamvaa Gambo, wadai wamechoshwa na kauli zake

Katibu wa UVCCM Mkoa wa Arusha, Ibrahim Kijanga akizungumza na waandishi wa habari.

Muktasari:

  • Umoja wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha, wamewataka viongozi wa juu wa chama hicho kumchukulia hatua kali za kinidhamu Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo kwa madai ya kutoa kauli mbaya za kudhihaki taasisi hiyo na Rais Samia Suluhu.

Arusha. Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha (UVCCM), wamemvaa vikali Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo wakimtaka kuacha kauli walizodai ni chafu na dhihaka pamoja na kejeli dhidi ya chama hicho.

Zaidi wamewataka viongozi wa juu wa chama hicho kumchukulia hatua kali za kinidhamu kwa madai ya kutoa kauli mbaya za kuwatukana na kuwadhalilisha wateule wa Rais kwani zina mrengo wa kumdhalilisha Rais Samia Suluhu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumanne Septemba 19, Katibu wa UVCCM Mkoa wa Arusha, Ibrahim Kijanga alisema kuwa Mbunge huyo wa tiketi ya CCM amekuwa akitoa kauli mbaya za kukidhihaki chama hicho na viongozi wake, lakini hachukuliwi hatua zozote hali inayomtia jeuri na kiburi.

“Amekuwa na dhihaka siku zote na baada ya kuchafua watu bila kusemeshwa akaanza kudhihaki viongozi wa chama bila hatua zozote lakini sasa amefikia anatoa kauli chafu za kumtukana na kumdhalilisha Rais kuwa eti wanaomwakilisha kazi yao ni kuimba mapambio," amesema na kuongeza.

"Hii siyo sawa na hatuwezi kunyamaza tena hivyo tunaomba chama waone mwisho umefika wa huyu mtu na wamchukulie hatua za kinidhamu na tunaamini wao ni wasikivu watatekeleza,” amesema.

Kauli hiyo imekuja baada ya hivi karibuni Gambo akiwa kwenye mkutano wa wakuu wa shule jijini Arusha, amesema kuwa yeye kama mbunge anafaa kuwasemea wananchi na hayuko kwenye nafasi hiyo kwa ajili ya kumfurahisha mtu wala kiongozi yoyote.

“Unajua kazi ya mbunge ni kufurahisha wananchi waliomchagua lakini viongozi wale wateuliwa inatakiwa wamfurahishe aliyewateua, kwa hiyo kila mtu ana jukumu lake hapa" amesema Gambo na kuongeza.

"Hivyo mbuge ukiacha tena kazi ya kuwatumikia wananchi na akaenda tena kuimba mapambio itakuwa hakuna maana ya kuwa na bunge tukufu,” amesema Gambo katika mkutano huo uliofanyika Septemba 16.

Kijanga alisema kuwa wao kama vijana wana jukumu kubwa la kulinda chama na viongozi wake hivyo kitendo cha Gambo kutoa maneno yaliyojaa dhihaka wamechoka kunyamaza.

“Tumefedheheka na kama akiendelea tutachukua hatua zaidi maana maneno yale yamejaa dhihaka kwa Rais aliyeteua watu hao na kuridhika nao tena akumbuke na yeye aliwahi kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa kumbe hakuja kufanya kazi ya Rais bali kuimba mapambio, hii ni dhihaka kubwa sana kwa Rais wetu,” amesema.