UWT kushughulika na viongozi wazembe

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania( UWT), Mary Chatanda

Muktasari:

  • Umoja wa Wanawake Nchini (UWT) ukimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, umeanza utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais Samia wakati akifungua mkutano wa uchaguzi wa umoja huo Novemba 28, 2022. 

Dodoma Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa wanawake (UWT), Mary Chatanda amesema umoja huo utapendekeza hatua za kuchukua kwa viongozi wote wanawake watakaoonyesha utovu wa maadili, uzembe na hujuma.

 Aliyasema hayo leo Desemba 09, 2022 wakati wa kongamano la UWT la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wa juu wa UWT kwa kuchaguliwa kwao kushika nafasi hizo za uongozi.

Chatanda amesema pamoja na kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika nyanja za uongozi, watahamasisha uwajibikaji kwa weledi ili kumsaidia Rais Samia kwenye uongozi wake.

Amesema UWT haitasita kukemea maovu kwa wanawake ambao watakaonyesha uzembe na kutowajibika kikamilifu wakati wa kutekeleza majukumu yao.

“Na hata ikibidi kupendekeza hatua za kuchukuliwa endapo tutaona na kuthibitisha vitendo vyovyote ambavyo vinakusudia uzembe, kukosa maadili na hujuma kwa kiongozi yoyote dhidi ya mwanamke kwa kiongozi yoyote wa awamu ya sita,”amesema Chatanda.

Amesema wanataka wanawake wote nchini kuonyesha kiwango cha juu cha uwajibikaji katika nafasi walizo nazo ndani ya chama na Serikali kuliko wakati wowote hapa nchini.

Amesema umoja huo utatekeleza maagizo yote ya Rais Samia aliyoyatoa katika mkutano wa uchaguzi wa umoja huo ikiwa ni pamoja na kushiriki kwa vitendo katika mapambano ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuongeza idadi ya wanachama wapya.

Pia Chatanda amesema kuwa wamoja, kuvunja makundi na kujenga chama chao kwasababu uchaguzi ndani ya chama hicho umekwisha.

Naye Makamu Mwenyekiti wa UWT, Zainab Shomari amesema wakati wanaomba kura lengo lao lilikuwa ni kuimarisha jumuiya hiyo upya kiuchumi, kisiasa na kimaendeleo.

Amesema ni matumaini yake kuwa viongozi wa jumuiya hiyo watawatumia wakuu wa mikoa kama fursa ya kuwezesha umoja huo uweze kujitegemea kiuchumi.

“Tutumie fursa hizi ziweze kutunufaisha, tushirikiane na Serikali na viongozi wetu ili tuweze kuondokana na ombaomba lakini pia kuwapunguzia wabunge wetu mzigo wasiwe tena ATMs,”amesema.

Amesema hawatoweza kuimarisha jumuiya hiyo kisiasa bila kuwashika vizuri watendaji wao na ili jumuiya hiyo imara itasimamia maslahi na haki za watendaji wao.