VIDEO: Bavicha wamvaa Tulia

Muktasari:

  • Baraza la vijana Chadema (Bavicha) limemtaka Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson kujiuzulu kufuatia kauli aliyoitoa hivi karibuni wakati akizungumza na vijana wa hamasa Wilaya ya Mbeya Mjini.

  


Dar es Salaam. Baraza la vijana Chadema (Bavicha) limemtaka Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson kujiuzulu kufuatia kauli aliyoitoa hivi karibuni wakati akizungumza na vijana wa hamasa Wilaya ya Mbeya Mjini.

Oktoba 3 mwaka huu katika mitandao ya kijamii ilionekana video yenye sekunde 58 ikimuonyesha Dk Tulia akiwaonya vijana hao kutoungana na mtu yoyote anaemsema vibaya Rais Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Katika video hiyo ilisikika akisema "Rais Samia ni Rais wa nchi na Mwenyekiti wa chama chetu, asitokee mtu yoyote ndani au nje ya chama akamkosoa shughulikeni nae na nyookeni nae"

Katika video nyingine yenye dakika moja na sekunde 35, Dk Tulia ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini, amesikika akisema “Shughulikeni nao kwa kujibu hoja na kama kuna shida elekeeni Sabasaba zilipo ofisi za CCM”.

Chadema wamvaa Tulia

“Jamani mwenyekiti wa chama kule kwenye mtaa wangu kuna shida moja, mbili tatu tunajaribu kuwaelewesha lakini mwenyekiti kule ni mtihani, kama kijana jana nimepitapita mtaani vijana wanakusema vibaya kuna changamoto pale,”

Akizungumza na wanahabari leo Jumatano Oktoba  5,2022 Mwenyekiti  wa Bavicha, John Pambalu amesema baraza hilo linasikitishwa na kauli hiyo kwani inahamasisha vurugu, na mtu ambaye ni Spika wa bunge.

Pambalu amesema wakati kauli hiyo ikitolewa Rais Samia na Jeshi la Polisi wamekaa kimya, badala ya kuchukua hatua wakati Taifa likiendelea kushuhudia hayo yakitokea.

“Kwa kuwa chama chetu kinaamini uhuru na haki, kwa kuwa Dk Tulia ni mwanasheria na kauli aliyosema inaligawa Taifa tunamtaka ajiuzulu,”amesema.