VIDEO: Ujumbe wa Lissu watikisa msiba kiongozi Chadema

Sunday March 01 2020
Lissu pic

Waombolezaji wakiwa wamekusanyika nyumbani kwa aliyekuwa kiongozi wa Chadema marehemu, Alex Joas. wakati wa mazishi yaliofanyika Manyoni jana. Picha na Habel Chidawali

Manyoni. Viongozi wa Chadema jana walitumia mazishi ya aliyekuwa katibu wa chama hicho jimbo la Manyoni Mashariki, Alex Joas kukemea matukio ya utekaji na mauaji huku ujumbe wa Tundu Lissu kuhusu matukio hayo ukiibua shangwe kwenye msiba huo.

Mazishi hayo yalihudhuriwa na viongozi wa chama hicho akiwamo mwenyekiti wa Kanda ya Kati, Lazaro Nyalandu na mwenzake wa Kaskazini, Godbless Lema na naibu katibu mkuu, Benson Kigaira.

Joas ambaye ni mkazi wa Majengo mjini Manyoni mkoani Singida, mwili wake ulikutwa umepigwa na kitu chenye ncha kali Februari 25, alizikwa jana mjini Manyoni katika makaburi ya Kaloleni.

Majonzi, shangwe

Akisoma ujumbe wa Lissu ambaye ni makamu mwenyekiti wa chama hicho, katibu wa Chadema Kanda ya Kati, Gwamaka Mbugi alisoma barua hiyo ambayo Lissu amemwandikia Nyalandu akimuomba aisome katika msiba huo.

Katika barua yake, Lissu amegusia matukio mengi ya wanachama wa Chadema kuuawa na watu aliowaita wasiojulikana. Aliwataja waliokumbwa na mikasa hiyo orodha ambayo ilikuwa na jina la aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo.

Advertisement

Mawazo alifariki dunia Novemba 14, 2015 wakati madaktari wa Hospitali ya Geita wakijaribu kuokoa maisha yake baada ya kushambuliwa na kundi la watu waliokuwa na silaha za jadi.

Waombolezaji walilipuka kwa shangwe na kusahau majonzi kwa muda baada ya Mbugi kusoma tukio la Lissu kushambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017.

Katika ujumbe huo, Lissu aliwataka wanachama wa Chadema kutokata tamaa licha ya maumivu na machungu wanayopitia.

Neno la Lema

Lema ambaye ni mbunge wa Arusha Mjini, aliwataka wananchi kutolipiza kisasi kwa mauaji ya Joas.

Lema ambaye ni waziri kivuli wa mambo ya ndani, alisema hofu yake ni kutokana na mlolongo wa matukio ya mauaji ya kuchinjwa, huku akiwataka wanasiasa wa vyama vyote kuungana kuwatafuta wauaji ambao mwisho ni kugombanisha wananchi.

“Sipendi muwe wanyonge, sitaki kuwazima hisia zenu, lakini nasema mlolongo wa mauaji ya watu 14 tena kwa kuchinjana, hii inaweza isiwe siasa za Chadema bali ni uzembe wa vyombo vya dola,” alisema.

Alimtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene kuwafukuza kamanda wa polisi mkoa wa Singida, OCD wa Manyoni na watu wote wa usalama mkoa kwa kuwa wameshindwa kazi.

Lema alimuomba Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), Daniel Mtuka kupiga kelele hata ikibidi kupoteza ubunge ili kuwasemea watu wake kwani wanaendelea kuisha kwa kuchinjwa.

Naye Mtuka alisema mauaji ya kinyama yamevuka viwango na kwamba, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro aingilie kati kuwasaidia wananchi wa Manyoni kwa kuwa kifo cha Joas ni cha saba

Naye mwenyekiti wa CCM wilaya ya Manyoni, Jumanne Mahanda alilaaani tukio hilo akitaka vyombo vya dola kuwasaka na kuwatia mbaroni wahusika.

Advertisement