Wajumbe Mkutano mkuu wafunguka changamoto mikoani

Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar), Dk Hussein Mwinyi ambaye ni Rais wa Zanzibar wakisikiliza maoni na changamoto zilizokuwa zikitolewa na wajumbe wa mkutano mkuu, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Licha ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutoa taarifa ya Serikali ya utekelezaji wa ilani ya CCM, wajumbe wa mkutano huo wamefunguka changamoto zikiwemo ubovu wa barabara, umeme na maji.

Dodoma. Licha ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutoa taarifa ya Serikali ya utekelezaji wa ilani ya CCM, wajumbe wa mkutano huo wamefunguka changamoto sugu kwenye Mikoa yao ambazo wanataka zifanyiwe marekebisho.

Changamoto hizo zimetolewa leo Desemba 8, 2022 na wajumbe wa mkutano huo kwenye mjadala baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fursa ya wajumbe kuchangia kuhusu muhtasari wa taarifa hiyo na kueleza changamoto zao.

Akizungumza katika mkutano huo, mjumbe wa kutoka Mkoa wa Kaskazini Pemba, Ramadhani Issa Kipaya amemuomba Rais wa Zanzibar Ally Hassan Mwinyi kutupia jicho Bandari kongwe ya Wete.


“Tunapenda kumuomba kutengeneza upya bandari ya Wete ambayo ni bandari Kongwe inapaswa kutengenezwa upya ili iwasaidie wananchi wanaokwenda kutafuta rizki maeneo mbalimbali,” amesema.

Kwa upande wake mjumbe wa NEC wa mkoa wa huo, Sophia Mzirai ameeleza changamoto ya upatikanaji wa fedha za uwezeshaji wananchi kiuchumi Sh114 bilioni ambazo Serikali imetenga kwaajili ya wanawake Zanzibar, vijana na watu wenye ulemavu kutokana na masharti magumu.

Sophia amesema kumekuwa na tabia ya wanufaika kutembelewa na kuidhinishiwa mkopo mkubwa, lakini siku ya kupewa mkopo huo hupata kidogo hali ambayo haiwanufaishi kwenye biashara na kusababisha kutorejesha mkopo huo.

Wakati wajumbe hao wakitaja hayo mjumbe kutoka Mkoani Songwe, Fatma Hussein amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kukamilisha ahadi ya ujenzi wa barabara kutoka Mbalizi hadi Mkwajuni na ya Kamsamba hadi Mlowo.

Fatma amesema barabara hiyo imeahidiwa na Marais watatu kuhusu utekelezaji wake lakini hakuna utekelezaji.

“Barabara hizi mbili ziliahidiwa na marais watatu, hayati Rais Mkapa (Benjamin) aliahidi, Kikwete (Jakaya) aliahidi, Hayati (John) Magufuli aliahidi na hata wewe ulipokuja Songwe 2020 kwenye Kampeni uliahidi, barabara hizi zimeshafanyiwa upembuzi yakinifu na tenda imetangazwa,” amesema.

Mjumbe kutoka mkoani Shinyanga, Sharifu Samwel ameiomba Serikali kutekeleza ahadi ya ujenzi wa barabara kutoka Korandoto kwenda Kishapu kwa kiwango cha lami ya km35 hadi 40.

Kuhusu uhaba wa maji, Dk Emmanuel Nuhas kutoka Mkoa wa Manyara amesema mkoa huo una uhaba wa maji hususan katika Wilaya za mbulu, Babati, Hanan’g na Simanjiro chini ya asilimia 50.


Naye Mjumbe kutoka Mkoa wa Kusini Unguja, Shaban Hassan Haji amesema Kusini mwa Mkoa huo kuna miundombinu ya maji chakavu inayosababisha upungufu wa maji.

Kuhusu ukosefu wa umeme mjumbe Joseph Kasheku kutoka Geita amesema mkandarasi ambaye alitakiwa kuanza kazi ya kusambaza umeme Oktoba, 2022 bado hajaanza kazi hiyo.

Wakati Geita wakilia na miundombinu Ally Kamtande Katibu wa siasa na uenezi Wilaya ya Temeke amesema changamoto ya Mkoa wa Dar es salaam ni kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Kamtande amesema ili kusaidia utatuzi wa changamoto hiyo ni muhimu kufufuliwa kwa miradi ya kuzalisha umeme ya kinyerezi 1, 2 na 3 ili kumaliza changamoto hiyo.