Prime
HADITHI: Mwiba mdogo-4
ILIPOISHIA
“Mmh! Sawa, nina imani wewe ulikuwa mtu wake wa karibu sana, hivyo hakuwahi kukuficha siri zake?”
Endelea
“Unataka kusema nini mkuu?”
“Mchungaji alishakueleza juu ya kuwa na ugomvi na mtu?”
“Mmh! Sikuwahi kusikia kuhusu ugomvi na mtu, siku zote alikuwa mtu wa kusamehe, aliamini msamaha ndiyo njia ya kuwa huru kiakili na kiroho.”
“Inawezekana kuna kitu unakijua juu ya kukwaruzana na mtu au kiongozi wa kanisa lolote. Hebu tueleze ni nani hata kama mkwaruzano ulikuwa mdogo.”
“Mmh! Hakuna, sijawahi. Baba Mchungaji alikuwa rafiki wa wote hata wasio Wakristu au madhehebu tofauti. Kwa kweli alikuwa kiigizo chema kwetu tulio chini yake tumefaidika na mengi sana.”
“Kifo chake kinaonekana cha kisasi, hata muuaji anajinasibu bado wanne, kama kuna siri unaijua niambie, najiuliza nani anafuata.”
“He! Kasema hivyo, Mungu wangu huenda ni mimi nafuata,” Mchungaji Lusajo alisema kwa woga.
“Ili tudhibiti vifo vingine, basi tueleze unachokijua juu ya Mchungaji Samwel.”
“Mkuu, sijui chochote, hata nikifa nitakufa bila kujua sababu ya kifo changu.”
“Nina imani mna siri kubwa, mkikaa kimya nitawasaidia vipi? Hebu iseme siri hiyo aliyokwambia bosi wako ili tuweze kuzuia hao wanne wa kufa.”
“Kwa kweli juu ya kifo chake sijui, huenda siri hiyo anaijua mwenyewe. Siwezi kusema kila siri yake lazima mimi niijue, siri ina maana kubwa sana kwa mtu, kuna siri huwezi kumwambia hata mama yako, baba yako, mkeo, rafiki yako bali atanena na Mungu wake ambaye ndiye msiri mkuu, huwezi kuitangaza siri yako uikute kwa kiumbe chochote.
“Siku zote atunzaye siri huwa sawa na aliyemeza moto, huwezi kuitunza kwa vile inakuchoma ndani kwa ndani, ili kuwa salama lazima uitoe hata kwa kuisema kwa sauti ukiwa peke yako na si kuitunza moyoni.”
Kama mwenye siri hawezi kutunza moyoni mwake na kukueleza wewe ili atue mzigo, wewe utawezaje kuivumilia?”
“Hivyo vipo vya kuelezwa na vingine huwezi kuelezwa, kwa vile msiri wa kweli ni bwana Mungu wako.”
“Kwa hiyo zaidi yako, nani mwingine mtu wa karibu yake?”
“Mtu mwingine wa karibu ni Mchungaji Mwakasanga wa ZIZI KUU LA BWANA na...na... mfanya biashara moja mkubwa.”
“Anaitwa nani?”
“Anaitwaaaa na...nakumbuka jina moja anaitwaa Balize.”
“Anakaa wapi?”
“Mikocheni B, nyuma ya Shopper’s Plaza.”
“Atakuwa George Balize yule tajiri wakala wa spare mwenye maduka Tanzania nzima?”
“Ndiye huyohuyo.”
“Ooh! Kuna umuhimu wa kuwataarifu wawe makini kabla ya kukutana nao ili wapate ulinzi.”
“Hao mtawapa ulinzi, mimi je?” Mchungaji msaidizi aliingiwa wasiwasi wa kuuawa kama mchungaji wake.
“Wewe kuanzia leo nitaweka ulinzi nyumbani kwako na kanisani.”
“Mmh! Sawa.”
“Umenitajia watatu, sasa huyo wa nne atakuwa nani?”
“Kwa kweli sijui, pia kuna watu maarufu wengi hata wenye vyeo vikubwa serikalini ni marafiki zake wakubwa hata kwenye hafla za kiserikali hualikwa hata kusoma dua kabla ya shughuli kufanyika.”
Kauli ile ilizidi kumweka mkuu wa upelelezi Shila kwenye wakati mgumu na kuona ugumu wa kazi yake kutokana na marehemu kuwa na marafiki wengi. Wakiwa katikati ya mazungumzo, simu ya mkononi ya Shila iliita, alipoiangalia ilikuwa ngeni, tena imepigwa kwenye kibanda.
Kabla ya kuipokea, kwanza alishusha pumzi na kuona kabisa ile simu haikuwa na usalama.
Alimwomba Mungu kimoyomoyo isiwe mbaya, kwani aliamini atazidi kuchanganyikiwa.
Alianza kuona dalili za Operesheni Rwanda kujirudia na kuamini siku zote kesi kama ile huwa ya kisasi ambayo husumbua sana kwa vile muuaji hujipanga sana na kuhakikisha kila anachokipanga kinakwenda vilevile. Alizipandisha pumzi na kuzishusha, kisha alipokea.
Wakati huo Mchungaji msaidizi wa kanisa la Chemchem ya Bwana macho yake yalicheza kwenye uso wa Shila na kuiona hofu kubwa baada ya kuitazama ile simu, kisha kuona jinsi alivyotulia akiwaza kabla ya kuipokea na kumfanya awe na maswali simu ile ina nini?
Mkuu Shila alipokea simu kwa sauti ya chini kidogo.
“Haloo.”
“Haloo, mkuu mbona umeingiwa ubaridi mapema wakati ndo kunakucha.”
“Nani wewe au mtoto wa marehemu?”
“Ndiyo mimi baba yangu,” sauti ya upande wa pili ilijibu kwa upole.
“Haya niambie mwanangu unasemaje?” Ilibidi awe mpole ili kupata huruma.
“Baba hesabu yetu imeongezeka.”
“Mungu wangu, umeua tena?” Shila aliuliza kwa mshtuko.
“Sijaua, natimiza hesabu yangu.”
“Kwa nini unaua mwanangu, kama kuna kosa kwa nini usije ofisini ili watu hao tuwakamate?”
“Baba, siku zote raha ya kisasi akutoae jicho nawe mtoe jicho, hata dini inasema kisasi ni haki. Kwa uwezo wao wa kifedha, nina imani huu umaskini wangu mtanikamata na kunifunga kwa kutengenezewa kesi ya kichwa. Tena mimi nachukua mtu mmoja mmoja wao wamenichukulia wote. Sitaki wenzangu wawe kama mimi kuwachukulia wazazi wao wote.
“Sitachukua uhai wa mtu asiye na hatia, mama yangu amekufa katika mateso mazito kwa ajili yao, baba yangu amekufa akivuja damu kama chujio la nazi. Nashukuru Mungu nimelipa kisasi cha baba yangu, bado cha mama yangu kinaendelea cha mateso mazito.”
“Kwani walikufanya nini mwanangu?”
“Ni historia ndefu, huu si wakati wake kwa vile nimekuahidi nikimalizana nao nitakuja mwenyewe kujisalimisha wala usisumbuke mzee wangu, nina imani una kazi nzito ya kumtafuta mwanamke albino aliyetekwa Mlimani City.”
“Wewe umejuaje?”
“Baba, mengi tutazungumza baadaye, huu si muda wake muhimu jua tu nimebakiza watatu.”
“Umemuua nani?”
“Nimemuua mzee George...”
“George Balize.”
“Swadakta baba! Utakuwa mtabiri kama Sheikh Yahya Hussein, ndiye huyohuyo nina imani anayefuata sasa utamjua.”
“Umemuua George Balize, umefanya mauaji wapi, binti naomba ujisalimishe nikikutia mkononi utafia gerezani.”
“Nimemuulia mlangoni kwake kwa kisu kama alichomuulia baba yangu kwa kuugeuza mwili wake kama chujio la nazi, risasi nilitumia kwa walinzi waliojipendekeza kwa kuwavunja miguu. Sikutaka kuwaua kwa vile ile kesi ilikuwa haiwahusu. Naapa sitatoa uhai wa mtu asiyenihusu.
“Nakuapia hawa mashetani watakufa kwa mateso kama alivyokufa mama yangu na baba yangu wakati wao wakifurahia utajiri wa damu na uhai wa watu.”
“Naapa nikikutia mikononi utajuta kuzaliwa.”
“Sina vita na wewe, ugomvi huu haukuhusu, umekuwa mtu mwema sana kwangu, umenisaidia mengi, hivyo hii vita iache mzee wangu. Hawa watu hawafai kuendelea kuishi, sema tu nina hofu na Mungu kila mmoja ningemuua kwa kumchoma moto na kubakia majivu. Hujui kiasi gani nimeumizwa na mashetani hawa halafu leo wengine wanakimbilia kwenye ucha Mungu? Sitamuacha mtu, hata mtu akifa nitamfukua na kumuua tena kwa kisasi vilevile,” sauti ya upande wa pili ilizunguza kwa uchungu mkubwa.
“Sasa...”
“Mzee wangu nipo kwenye kibanda cha simu kuna watu wapo nje wanasubiri huduma bai...,” simu ilikatwa upande wa pili.
“Kazi ipo,” Mkuu Shila alisema huku akishusha pumzi na kufuta jasho kwa kitambaa.
“Mzee unataka kuniambia mzee Balize naye amefariki?” Aliuliza Mchungaji Lusajo, macho yamemtoka pima.
“Ndiyo.”
“He! Kwa hiyo nafuata mimi?” Mchungaji Lusajo alipagawa.
Kabla ya kuendelea kuzungumza Shila aliwajulisha polisi tukio la mauaji Mikocheni B nyuma ya Shopper’s Plaza. Aliwataka vijana wake wafike eneo la tukio kufanya uchunguzi huenda wakaambulia kitu chochote. Kisha alimgeukia mchungaji aliyeonekana amepagawa kwa taarifa za mtu waliyekuwa wakimzungumzia muda mfupi baada ya kifo cha bosi wake.
“Kwa hiyo unajua siri ya mauaji haya?” alimuuliza amemkazia macho.
“Nakuapia kwa jina la Yesu Kristu aliye hai, sijui kitu chochote mheshimiwa,” Mchungaji Lusajo aliapa mpaka akalamba mchanga kwa msisitizo.
“Kama unasema kweli huijui siri hii, nina imani haupo kwenye hesabu za muuaji,” ilionyesha wazi alikuwa hamjui vizuri bosi wake na siri ya utajiri wake.
“Baba Mchungaji hana siri yoyote, siku zote amekuwa msafi mbele ya Mungu.”
“Umesema muda si mrefu kuwa siri nyingine anajua mtendaji na Mungu wake pale atakapotubu toba ya kweli isiyo na shahidi.”
“Ni kweli lakini si kwa Mchungaji wangu.”
“Usimuamini mwanadamu hata akiwa mzazi wako, ni kweli na muaminifu ni Muumba ambaye hasemi uongo si kama mwanadamu, ndiyo sababu hutusamehe kutokana na mapungufu kimaumbile.”
“Mmh! Unasema kweli mkuu nakiri nimekengeuka kwa mapenzi ya mwili na si kiroho.”
“Kwa vile kuna tukio lingine zito wacha niwaache niwahi ili nijue nini kinaendelea.”
“Sawa mkuu, nikupe pole nina imani hujala wala kupumzika.”
“Ni kazi tuliichagua hatuna budi kutumikia ninyi mabosi wetu.”
Itaendelea