Prime
MWIBA MDOGO-13
ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA
Hii kesi ningeipeleka polisi mwenye hatia ningekuwa mimi, ningefungwa au kunyongwa. Japo haipendezi nilichokifanya lakini niliamini uamuzi wangu ulikuwa sahihi. ENDELEA...
Niliamua niwe polisi mimi, mahakama mimi, sikuwa na hukumu tofauti na kifo na mnyongaji nilikuwa mwenyewe. Ndiyo maana nilikueleza baba nikifunga hesabu zangu nitajisalimisha mwenyewe bila shuruti.”
“Sawa, najua mpaka kufikia hatua ya wewe mwenyewe kujichukulia sheria mkononi, basi hebu tuanze sasa kwa kujitaja jina lako umezaliwa mwaka gani, nini kiliwasibu wazazi wako mpaka kufikia kulipa kisasi.
“Kuna vitu vingine sivijui japo kuna wakati nilikaa na wewe hukuonyesha tatizo lolote, japokuwa kifo cha mama yako kilikuathiri kwa kiasi kikubwa. Nataka kujua huu ujasiri umeutoa wapi japokuwa alijiunga na jeshi la wananchi.”
“Sawa baba, kupayuka kwangu imenisaidia kupunguza sumu moyoni, sasa nitaweza kuzungumza kwa taratibu,” alisema Diana huku akifuta machozi kwa kitambaa na kupenga mafua membamba, kisha alichukua chupa ya maji na kupiga tarumbeta nusu chumba, alijifuta mdomo na kusema:
“Samahanini ndugu zangu pamoja na baba, moyo wangu umeteseka sana kila nilipowaona kina Mchungaji Samwel na wenzake wakifurahia maisha, aah basi tuanze zoezi letu, niongezeni chupa nyingine mbili za maji.”
“Hakuna tatizo.”
Baada ya kusema vile alipewa dakika mbili za utulivu kwa kupandisha pumzi na kuzishusha na kuwaeleza yupo tayari.
“Nipo tayari tunaweza kuanza.”
“Haya dada yangu, kaa tayari macho kwenye kamera, moja... mbili... tatu anza.....,
“Kwa jina naitwa Zulfa Hanzuruni, japokuwa baba mzee Shila jina ananijua kwa jina la Diana, ni mtoto wa pekee kwa baba yangu mzee Hanzuruni na mama yangu Salma Abedi Ndedefu. Nimezaliwa miaka ishirini na tisa iliyopita katika hospitali ndani ya machimbo ya Tanzanite huko Mirelani.
Mpaka napata akili nilijikuta nipo katika kituo cha kulelea watoto yatima ambako nilikaa kule mpaka nilipofika kidato cha pili ndipo nilipokutana na Fatma ambaye ni mtoto wa baba mzee Shila.”
Kauli ile iliwafanya watazamane kujua kumbe muuaji kapitia mikononi mwa mkuu wao Shila.
“Urafiki wangu na Fatma ulikuwa mkubwa kiasi cha kunigeuza kama ndugu yake na kuweza kunishawishi nihamie kwao kwa baba mzee Shila ambako nilipokelewa kama mzaliwa wa nyumba ile.
“Kutokana na tabia yangu ya upole, heshima na upendo kwa wote ulifanya nipendwe na wazazi wote zaidi ya mtoto wao wa kumzaa, Fatma.
Ajabu Fatma hakuonyesha kuumizwa kwa mimi kupendwa na wazazi wake zaidi na yeye kuongeza mapenzi ili nisijishuku kuwa mimi ni yatima.
Nakumbuka nilipofika kidato cha tatu nikiwa mjini siku hiyo nilitoka peke yangu na dereva wa familia, siku hiyo Fatma alikuwa hajisikii vizuri.
Ilikuwa nadra sana kumkuta mmoja wetu yupo peke yake, mara nyingi tulikuwa pamoja. Ilifikia hatua ya kuitwa mapacha tusiofanana, kwa jinsi tulivyokuwa tukipendana na kuwa karibu muda wote.
Basi siku hiyo nilitoka na dereva kwenda Mlimani City kununua mahitaji muhimu ya nyumbani.
Nikiwa natafuta baadhi ya vitu vya nyumbani, nilikutana na mama mmoja aliyenichangamkia sana kwa kuniita jina si langu. Japo sikuwaeleza kuwa wakati najitambua na kujikuta kituo cha kulelea watoto yatima jina langu nilikuta naitwa Diana John.
Nami niliunganisha hivyohivyo na kuamini Diana ndiyo jina langu na baba yangu anaitwa John. Lakini ajabu siku ile niliitwa jina jingine kabisa eti Zulfa binti Hanzuruni.
“Mama utakuwa umenifananisha, mimi naitwa Diana binti John.”
“Si kweli, wewe unaitwa Zulfa tena Muislamu siyo Mkristu kama ulivyo sasa.”
“Hapana mimi siitwi Zulfa wala siyo Muislamu, mimi Mkristu tena nimebatizwa.”
“Zulfa najua baada ya baba yako kuuawa kinyama na mama yako kupata ugonjwa wa akili hukujulikana upo wapi.”
“Unasema baba yangu aliuawa kinyama na nani?”
Japokuwa niliamini yule mama kanifananisha, lakini kauli ya baba yangu kuuawa ilinishtua. Maisha yangu yote niliyoishi katika kituo kile sikuwahi kujua wazazi wangu wako wapi, wazima au wamekufa. Nilielezwa niliokotwa mtaani nikitembea usiku peke yangu huku nikilia, ndipo wasamaria wema waliponichukua na kunipeleka kituo cha watoto yatima.
Maisha yangu yote sikuwajua wazazi wangu, mimi dini gani, kabila gani, nilichokiangalia kilikuwa uzima. Japokuwa nilijua ananifananisha, lakini alipozungumzia kifo cha baba yangu ambaye nilikuwa simjui na ugonjwa wa mama yangu, niliumia sana.
“Haijulikani ila alikutwa amekufa nyumba ya wageni hapahapa Dar.”
“Hiyo nyumba ya wageni ipo wapi?”
“Manzese.”
Kusikia Manzese nilishtuka kidogo, kwani taarifa zilisema niliokotwa Manzese pamoja na kutangazwa kwenye misikiti yote ya Manzese na vitongoji vya karibu hakuna aliyejitokeza kunijua ndipo kituo kilipochukua jukumu la kunilea na kunisomesha.
“Kwani tulikuwa tunaishi wapi kabla ya kifo cha mtu anayesema baba yangu?”
“Katika machimbo ya Mirelani baba yako alikuwa dereva wa kampuni ya uchimbaji wa Tanzanite.”
“Mbona unanichanganya, ilikuwaje baba yangu kufanya kazi Arusha kufia Dar es Salaam.”
“Kwa kweli sijui chochote zaidi ya kusikia kifo cha baba yako na mama yako kupatwa na ugonjwa wa akili.”
“Kwa hiyo mama yangu yupo wapi?” nilimuuliza huku nikiamini kabisa atakuwa amenifananisha na siyo mtu anayemdhania.
“Mama yako yupo Muhimbili wadi ya wagonjwa wa akili.”
“Anatumia jina gani?”
“Salma Abedi Ndedefu, yaani sema tu kwa sasa ugonjwa umemmaliza mama yako, lakini ukimuona wala haujiulizi mara mbili.”
“Nina imani umenifananisha japo taarifa za watu unaonieleza zinasikitisha na kuumiza, kama nilikuwa binti mdogo nisiyejitambua pia hata sura yangu ilikuwa ya kitoto, huoni utakuwa unanifananisha?”
“Binti hicho kidoti chini ya mdomo na mama yako hivyo hivyo, pia hata uongeaji wako kama mtu anayewafahamu anaweza kukuvamia na kukuita Salma.”
“Unajua duniani wawili wawili, utakuwa unanifananisha, naomba niondoke niwahi nyumbani.”
“Kwani wewe wazazi wako wako wapi?”
“Sina wazazi.”
“Wapo wapi?”
“Sijui.”
“Unaona sasa, Zulfa mtafute mama yako, kama siyo achana naye, lakini moyo wangu unaniambia ni wewe sura yako hajabadilika zaidi ya kukuongezea uzuri kama mama yako.”
“He! Mama yangu anaumwa nini?”
“Pamoja na tatizo la ugonjwa wa akili, madonda yamemtoka mdomoni na kwenye ulimi hata zungumza yake ya shida, japokuwa tangu zamani mama yako si muongeaji sana,” kauli ya tabia ya ukimya ilikuwa kama yangu ilionekana nafanana vitu vingi na mtu niliyeambiwa ni mama yangu na kuwa na shauku ya kumuona.
“Ulishawahi kwenda kumuona mama?”
“Kila nikija Dar lazima niende kumuona, alikuwa shoga yangu mkubwa ndiyo maana nilipokuona tu nikakujua.”
“Kwani wewe unakaa wapi?”
“Arusha.”
“Bado upo mgodini?”
“Hapana tulishaondoka tupo Arusha mjini.”
“Ukienda kumuona anakutambua?”
“Ananitambua vizuri, hata wanangu huniulizia kama hawajambo.”
“Sawa nashukuru nitaenda kumuona.”
“Nina imani mama yako atafurahi sana kukuona mnavyofanana wala mtu haulizi, kwa baba yako umechukua macho na rangi.”
“Nashukuru mama yangu, nitakutafuta.”
Tulipeana namba ya simu na kuagana, nilimalizia kununua mahitaj muhimu na kurudi nyumbani, huku nikijiuliza mimi ni nani. Sikutaka kuisumbua akili yangu, nilipanga kwenda hospitali ya Muhimbili bila kumwambia mtu.
Siku moja Fatma aliwahi kuondoka shule, nami nilitumia nafasi ile kwenda hospitali.
Japokuwa nilikuwa naogopa kwa vile niliwahi kutishwa na watu kuwa wagonjwa wa akili wanaweza kukupiga bila sababu. Nilipitia Super Market na kununua vitu kama vyakula na kunywa kisha nilielekea hospitali.
Nilifika hadi wadi ya wagonjwa wa akili na kuulizia jina la Salma Abedi Ndedefu.
Muuguzi hakupata shida ya kumtafuta kwenye kitabu cha wagonjwa, aliniangalia sana mpaka nikaona aibu.
“Dada mbona unanitazama sana mpaka naona aibu?”
“Salma ni nani yako?”
“Nimeambiwa eti ni mama yangu.”
“Yaani nilivyokuona sikuwa na haja ya kujiuliza mnavyofanana na mama yako utafikiri mapacha,” kauli ile ilinifanya niwe na shauku ya kumuona huyo mama yangu.
Nilielekezwa wadi aliyokuwemo, nilikwenda na kukutana na sura yenye taswira yangu. Sura iliyokuwa mbele yangu ilikuwa kama najiangalia kwenye kioo, mama alinichanulia tabasamu pana.
Unaweza kufuatilia hadithi hii kupitia tovuti ya Mwananchi, pia Mwananchi Digital katika Mtandao wa YouTube.
Itaendelea kesho