Ngumi za ridhaa zirudishe uhalisia

Monday January 11 2021
Ngumi pic
By Imani Makongoro

Timu ya Taifa ya ngumi za ridhaa ni miongoni mwa michezo iliyowahi kutamba na kuiletea nchi sifa kwenye mashindano ya kimataifa.

Miongoni mwa rekodi ambayo timu hiyo iliweka ni ile ya michezo ya Afrika ya 1987 nchini Kenya, ambapo timu hiyo ilitwaa medali moja ya fedha na tatu za shaba.

Kwenye michezo hiyo, Tanzania ilivuna medali saba, tatu za riadha na nne za ngumi, na kuweka historia ya kushinda medali nyingi zaidi kuwahi kutokea kwenye michezo hiyo.

Kabla ya michezo hiyo, Titus Simba aliweka rekodi ya kuwa bondia wa kwanza nchini kushinda medali ya kimataifa.

Simba ambaye sasa ni marehemu alishinda medali ya fedha kwenye michezo ya jumuiya ya madola nchini Scotland mwaka 1970.

Simba aliingia fainali kwenye uzani wa kati na kuchapwa na Muingereza, John Conteh aliyetwaa dhahabu na Simba kutwaa fedha.

Advertisement

Tangu wakati huo hadi mwishoni mwa miaka ya 1990, timu ya taifa ya ngumi imekuwa na historia ya kufanya vizuri kabla ya kuanza kupotea miaka ya 2000 hadi sasa.

1998, kwenye michezo ya Jumuiya ya madola ya Kuala Lumpur, Malaysia, Michael Yombayomba (sasa ni marehemu) aliweka rekodi ya kutwaa medali ya dhahabu, ambayo haijawahi kuvunjwa na bondia mwingine nchini mpaka sasa.

2012 ndiyo ulikuwa wa mwisho kwa mabondia wa ridhaa kufuzu kushiriki Olimpiki, ingawa pia miaka ya hivi karibuni wamekuwa na historia ya kuondolewa mapema kwenye mashindano ya kimataifa.

Mwezi Machi mwaka huu, mabondia wa timu ya taifa watakuwa nchini Morocco kwenye mashindano ya dunia, lakini pia Mwezi Mei watakuwa Ufaransa kwenye mashindano ya kufuzu Olimpiki 2021.

Wakati wadau wa mchezo huo wakisubiri kuona kama timu ya taifa itafanikiwa kupenya na kuruka kihunzi hicho ili kushiriki Olimpiki, kuna jambo ambalo viongozi wa ngumi wanapaswa kujifunza.

Kwa miaka kadhaa sasa ngumi za ridhaa zimekuwa zikichezwa kwenye maeneo ya wazi, hasa Dar es Salaam ambako mara nyingi mchezo huo umekuwa ukifanyika kwenye viwanja wa Tanganyika Pakers, Kawe jijini Dar es Salaam.

Sipingani na uongozi kufanya mashindano kwenye uwanja huo, lakini ukweli ni kwamba wanaondoka kwenye uhalisia wa mchezo wa ngumi hasa za ridhaa.

Ngumi za ridhaa katika mashindano yote makubwa zinachezwa kwenye uwanja wa ndani, utaratibu huo upo kwenye Olimpiki, madola, Afrika na mashindano mengine ya kimataifa.


Kwa Tanzania, ni kweli tuna uhaba wa viwanja vya ndani na kumbi ambazo zinaweza kutumika kwa ajili ya mashindano ni gharama kutumia.

Hivyo kuna uwanja wetu wa taifa wa ndani, japo umechakaa, lakini kwa kipindi hiki ambacho hatujui ni lini Serikali itajenga uwanja mpya kama ilivyoahidi, viongozi wa ngumi za ridhaa (BFT) wangeendelea kuutumia kwa mashindano, tofauti na kufanya mashindano kwenye viwanja vya Tanganyika Pakers.

Uenda wazo la viongozi kupeleka mashindano ya taifa kule lilikuwa ni jema na kutaka kuongeza hamasa ya watazamaji, lakini linapoteza uhalisia wa mchezo wa ngumi za ridhaa.

Ngumi za ridhaa ni mchezo unaopaswa kufanyika kwenye kumbi au viwanja vya ndani, wachezaji wetu wanaposhindana au kujifua kwenye viwanja tofauti, kisha wanakwenda kwenye mashindano ya kimataifa na kutakiwa kucheza kwenye viwanja vya ndani, kwa namna moja au nyingine, lazima itawaathiri tu.

Kama kote duniani kwenye mashindano ya kimataifa ngumi zinapigwa kwenye uwanja wa ndani, basi uhalisia huo ungebaki hadi katika mashindano ya ndani na mazoezi ili kuwajengea mabondia wetu kuzoea mazingira hayo.

Tofauti na akiwa nchini atajifua na kushiriki mashindano kwenye mazingira tofauti, akienda kwenye mashindano ya kimataifa anakutana na mazingira tofauti.

Kingine ambacho BFT inapaswa kujifunza ni utaratibu wa kufanya mashindano ya wazi ya taifa.

Utaratibu huu unatoa fursa kwa bondia yoyote, awe na klabu au la kwenda kushiriki mashindano ya taifa.

Uenda kweli uongozi ukawa na nia ya kutafuta vipaji vipya, lakini vipaji hivyo vingeanza kutafutwa kwenye mashindano ya klabu na timu za wilaya, kisha wakachujana hadi kwenye mikoa na ile krimu timu, ndiyo ikashindanishwa kwenye mashindano ya taifa.

Hii itasaidia kwanza viongozi wa Wilaya na mikoa pia kuwajibika, na si kukaa na kusubiri uchaguzi mkuu ndipo wanaibuka kuwa ni viongozi wa mikoa au wilaya.

Advertisement