Ajali ya Korogwe itupatie funzo la uokoaji

Wiki iliyopita ilimalizika kwa majonzi na vilio. Ni baada ya kutokea moja ya ajali mbaya zilizosababisha vifo vya watu wengi, na wengi wao wakiwa wa ukoo mmoja waliokuwa wanasindikiza msiba.

Tayari ndugu hao 20 wamepoteza maisha huku sita wengine wakiendelea kuupigania uhai wao hospitalini.

Siku ya tukio, watu 18 walipoteza maisha, wanane kati yao wakifia eneo la ajali na waliobaki hospitalini walikopelekwa kwa ajili ya matibabu.

Kutokana na uzito wa janga hilo lililowapata waliokuwa tayari katika msiba, Serikali imelipa gharama za kufanikisha mazishi ya ndugu hao pamoja na watu watatu waliokuwa kwenye lori aina ya Fuso lililogongana uso kwa uso na Coaster waliyokuwa wanasafiria ndugu hao.

Pamoja na huzuni na masikitiko, kuna mengi ya kujifunza kama Taifa hasa linapokuja suala la kukabiliana na ajali.

Kilichoshuhudiwa Korogwe hakina tofauti sana na kilichotokea katika Ziwa Victoria pale ndege ya Shirika la Precision ilipozama baada ya kushindwa kutua Uwanja wa Ndege wa Bukoba. Abiria wengi walipoteza maisha kutokana na waokoaji kuchelewa.

Mkoa wa Tanga nao umekumbana na kilekile. Baada ya ajali, watu wanane ndio waliothibitika kupoteza maisha palepale na 19 waliobaki walikuwa na majeraha tofauti na huenda kama wangepa huduma za dharura kwa wakati, huenda baadhi yao wangeokolewa.

Kwa hali ilivyo, kila halmashauri nchini inahitaji kuwa na idara ya uokoaji itakayokuwa inafanya kazi wakati wote kuwahudumia majeruhi watu wengine waliohusika kwenye ajali mbalimbali.

Idara hii itakayokuwa na watu walio tayari pamoja na vifaa vya uhakika bila kusahau vitendea kazi vinavyostahili wapewe mafunzo stahiki kuwahudumia watu wanaokaribia kupoteza maisha kutokna na ajali za namna tofauti ili kupunguza idadi ya vifo vinavyoweza kuepukika.

Kwenye ajali ya Korogwe kwa mfano, iwapo timu ya madaktari wazoefu ingewahi eneo la tukio au hospitalini walikopelekwa majeruhi na kutoa huduma zinazostahili, wengi wangepona.

Hii ni kwa sababu uokoaji wa majeruhi katika ajali unahitaji utaalamu maalumu ili kuokoa maisha ya majeruhi na vilevile mazingira ya uokoaji yanahitaji usalama.

Mbali na hilo, ni muhimu pia maeneo ya ajali yakapewa kuzuia wizi na udokozi unaoweza kufanyika kama ilivyotokea Korogwe ambako baadhi ya marehemu na majeruhi waliibiwa mali zao badala ya kuokolewa.

Jeshi la Polisi kwa kukitumia kikosi chake cha usalama barabarani hili lilikuwa eneo muhimu kwake kuwahi kulinda usalama wa raia na mali zao, achilia mbali kusaidia uokoaji.

Kutokufanya hivyo mapema kulitoa mwanya kwa vibaka kuiba mali za watu wanaostahili kusaidiwa.

Yanaweza kutolewa maelezo mengi na sababu nyingi kwa nini askari walichelewa kwenda eneo la ajali ila ukweli utabaki kuwa tunahitaji kikosi imara cha uokoaji pindi ajali inapotokea.

Uzoefu tulioupata kwenye ajali kadhaa zilizotokea unatosha kuthibitisha kuwa hatujajipanga vyema kukabiliana na majanga hayo.

Ajali nyingi zinatokea kwenye barabara kuu ikilinganishwa na maeneo mengine hivyo tuweke mpango wa kuyasimamia maeneo hayo kwa kuweka vikosi maalumu vya kushughulika dharura za namna hiyo.

Tukijitosheleza barabarani tuhamie maeneo mengine ikiwamo majini, angani na kwingineko ambako Watanzania wanapoteza maisha kabla ya wakati.