Anachokaje sasa! Si tulikubaliana tunawasisimua mwanzo mwisho

Monday March 22 2021

Mpaka leo hii bado kuna wanaume wenye mitazamo ya ajabu ajabu juu ya wanawake. Nyumbani kuna wababa ambao bado wanaamini mtoto wa kiume anastahili upendeleo zaidi kwenye kupewa elimu kuliko wa kike.

Kwamba mtoto wa kike anastahili kusoma mpaka kiasi fulani hivi kisha inatosha, ‘si ataolewa, sasa unamsomesha sana kwa ajili ya nini, ni kupoteza pesa tu.’ Ukiwa mwanamume wa hivi ndani ya mwaka 2021, maana yake kichwani una matope, sio akili.

Mpaka leo kuna wanaume wanaamini mwanamke ni chombo cha starehe, wanawavua ubinadamu wanawake na kuwachukulia kama kiburudisho tu. Unakwenda baa unakuta mtu anaamua tu kuanza kumshikashika mhudumu bila matakwa yake, kwa nini? Kwa sababu ni mwanamke basi anaweza kuchezewa; ‘Mungu aliwaumba kwa ajili ya kutuburudisha hawa, heshima ya nini?’ ukiwa mwanamume wa hivi kuanzia mwaka 2021, maana yake kichwani umejaza sisimizi, sio akili.

Mpaka leo kuna wanaume wanaamini mwanamke ni mtu wa kufanya mambo ya kawaida, madogo madogo, majukumu mepesi mepesi licha ya ushahidi wa kutosha kuhusu uwezo mkubwa walionao, ukiwa mwanaume wa hivi mwaka 2021, maana yake kichwani umejaza hewa, sio akili.

Lakini kupitia historia iliyoandikwa Tanzania ya kuwa na Rais wa kwanza mwanamke, Samia Suluhu Hassan naamini wanaume wengi wajinga wajinga watabadilisha mitazamo kuhusu wanawake.

Tutaanza kuona uwezo mkubwa wa watoto wetu wa kike ambao tuliudumaza kwa kuwanyima elimu ya kutosha, kupitia atakachokifanya Mama Samia Suluhu na huenda tutachukua hatua.

Advertisement

Wanaume tuliokuwa tunawachukulia wanawake ni wa kufanya mambo mepesi tutaanza kuwapa heshima kwa kujifunza kupitia Rais Samia. Tutaanza kuona kama mwanamke anaweza kuongoza nchi, familia kubwa yenye watu zaidi ya milioni 50, kitu gani kingine atashindwa?

Na pengine kupitia funzo hilo tutaanza kuwashirikisha kwa kiasi kikubwa kwenye mambo muhimu, kuwapa nafasi ambayo tumewanyima kwenye ngazi za familia miaka nenda rudi, kuuweka usawa wa kweli, kwamba wao wanaweza kufanya mambo ambayo sisi tunaweza kuyafanya pia, kwa hiyo tunahitaji nafasi sawa bila kuzingatia jinsia.

Tena hata kama tutabadilika kuanzia sasa itakuwa ni kama tumechelewa kwa sababu mshua, baba yetu, chuma, hayati John Pombe Magufuli alituonyesha hili muda mrefu kipindi cha uhai wake.

Magufuli alituonyesha uhalisia wa mwanamke tangu alipomchagua Rais mama Samia kuwa Makamu wake, alikuwa na uwezo wa kumuweka mwanamume kwa sababu alikuwa na machaguo mengi lakini akasema hapana, nafasi hii anastahili huyu mwanamke sio kwa sababu ni mwanamke, bali kwa sababu ana uwezo wa kuishikilia hiyo nafasi, na hivi sasa tuko karibu kuthibitisha maono ya Magufuli.

Kabla mambo hayajakuwa mengi kina baba badilikeni, Rais Samia alipewa elimu na kulelewa katika malezi ya kuaminishwa kuwa mwanamke anaweza na akapewa nafasi na sasa kwa maamuzi ya Mungu ghafla amekabidhiwa jukumu la kuiendesha nchi.

Ingawa ipo Kikatiba, lakini hakuna aliyekuwa anafikiria hilo litatokea, lakini kwa sababu alikuwa Makamu wa Rais nafasi ya juu kabisa ya uongozi hilo limewezekana.

Tuzinduke kupitia mfano huu, wanawake wanaweza popote walipo kila mmoja kwa nafasi yake, kinachotakiwa ni kuwapa fursa kama wanazopata wanaume.

Sijasema za upendeleo hapana, namaanisha kama ambazo wanaume wanapata, sina shaka na uwezo.

Anti Bettie

Advertisement