Bara la Afrika linavyojivunia kwa lugha ya Kiswahili

Muktasari:

Lugha ni chombo muhimu sana cha mazungumzo kati ya watu katika nyanja mbalimbali za maisha.


Na Shimaa Tarek

Lugha ni chombo muhimu sana cha mazungumzo kati ya watu katika nyanja mbalimbali za maisha.

Duniani kuna lugha kedekede na zote ni matunda ya mila na desturi za jamii husika.

Mojawapo ya lugha naweza kusema muhimu duniani kwa sasa ni lugha adhimu ya Kiswahili yenye asili yake katika upwa wa Afrika Mashariki.

Hata hivyo, wigo wa matumizi ya lugha huo sasa umekua kwa kiwango kikubwa, kwani inatumika sio tu ndani ya Afrika Mashariki bali hata Afrika na mabara mengine duniani.

Hata hivyo kufika huko,haikuwa jambo la bahati nasibu. Ni juhudi za kitambo sana kuanzia kwa waasisi wa Tanzania akiwamo aliyekuwa Rais wa kwanza, Mwalimu Julius Nyerere.

Lakini pia Kiswahili sasa kinatamba kutokana na jitihada za taasisi mbalimba za ndani na nje ya Tanzania. Miongoni mwa jitihada hizo ni harakati ya kimataifa yenye jina la aliyekuwa Rais wa Misri, Gamal Abdel Nasser. Ni harakati iliyozaliwa nchini Misri ikiwa na mapenzi makubwa na lugha ya Kiswahili.

Moja ya mapenzi ya harakati za taasisi hii kwa lugha ya Kiswahili ni kaunzisha ukurasa wa mtandao wa facebook uitwao “Harakati ya Nasser kwa Vijana “

Lengo la ukurasa huo ni kuonesha watu, uhusiano mwema kati ya nchi zote za Kiafrika kupitia nchi ya Misri. Lengo ni lile lile la kuendeleza lugha hii adhimu na tamu kwa bara letu la Afrika.

Misri ni miongoni mwa nchi za kwanza kukipa umuhimu Kiswahili. wanafunzi wengi nchini hapa, wana hamu kujifunza na kujua lugha hii ya bara letu.

Hivi sasa lugha hii hapa Misiri inafundishwa katika vyuo vikuu vinne na wanafunzi wake wakiendelea kueneza lugha hiyo nchini Misri na duniani kote.

Kwa hivyo umuhimu wa lugha ya Kiswahili unaongezeka kila siku barani Afrika na duniani kote. Hivi sasa watu wengi wanaijua lugha ya Kiswahili na wanahangaika kujifunza lugha hiyo.

Aidha, ukubwa wa Kiswahili umezidi kukua hasa baada ya Umoja wa Mataifa, kupitia shirika lake la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), kuitangaza Julai 7 ya kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani.

Tukirudi katika harakati za Nasser kwa vijana, harakati hizi zina lengo la kusisitiza ajenda ya malengo ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063, ambayo yanaeleza umuhimu wa kutoa heshima kubwa kwa waanzilishi wa umoja wa nchi huru za Afrika .

Huu ndio umoja unaokumbukwa kwa jitihada zake za kusaidia kuondoa utumwa, ubaguzi wa rangi na wa kijinsia na ukoloni kwa jumla katika nchi nyingi za bara la Afrika.

Gamal Abd El_Nasser, anazingatiwa kama mmoja wa viongozi muhimu na wa kupigiwa mfano barani Afrika. Anakumbukwa kwa kuunga mkono harakati za ukombozi wa nchi za Kiafrika hadi zikapata uhuru kutoka wavamizi wa kikoloni wa nchi za Ulaya.

Vilevile, harakati ya Nasser kwa vijana kama taasisi inalenga kuimarisha viunganishi vya kihistoria,kukuza uhusiano wa pande mbili kati ya Misri na nchi zote ndugu, kubadilishana uzoefu wa vijana duniani kote na kuimarisha mifano ya mafanikio.

Pia ina lengo la kuunda jukwaa la vijana duniani kote kwa kuongeza kanuni za harakati ya kutofungamana na upande wowote na kutetea mshikamano wa Afro-Asia na Umoja wa Afrika hasa katika vifungu vinavyohusiana na vijana, wanawake, hali ya hewa, elimu, usalama na ujasiriamali. Tunajivunia kuwa harakati kwa sasa imesambaa na kuwa na matawi katika nchi 65.

Mwandishi ni mfasiri wa lugha ya Kiswahili anayeishi Misri anayejihusisha pia na harakati za Nasser kwa vijana