FYATU MFYATUZI: Tumekubali kuwa mateka wa watekaji?
Hapo zamani kaya ikiwa kaya, tulizoea kusikia utekaji na uuaji wa watu kisiasa kwa majirani zetu. Majirani zetu wa kaskazini mashariki walisifika kwa mchezo huu mchafu uliofyatua vigogo wengi wa kisiasa, wakiwamo mawaziri kabla ya wale wa kaskazini magharibi kuchukua ukanda. Ni pale nduli alipompoka madaraka Oboto ambaye naye alimpoka madaraka Kabaka, tena kwa kumtumia nduli huyuhuyu.
Sasa inavyoonekana ni zamu yetu. Zamani tukiitana ndugu. Kila fyatu alikuwa ndugu wa mafyatu wote, zama za mzee Nchonga (RIP sana Nguli). Baadaye alikuja Mzee Ruxa (RIP sana Mwamba) kabla ya kuja kwa mzee Ben Nkapa (RIP sana bro). Baada ya hapo alikuja BoysIIMen, na baadaye Jiwe (RIP). Katika awamu zote tano, mambo ya mafyatu kutekwa na kufyatuliwa na mafyatu wasiojulikana yalianza zama za jiwe. Hapa ndipo ulipo mzizi wa kadhia hii ya ajabu na aibu kwa kaya iliyosifika kwa udugu, upendo, usawa, na mshikamano tena vya kupigiwa mfano.
Pamoja na mazuri yake kivitu, jiwe hakufanikiwa kiutu pamoja na kujiita mtetezi wa mafyatu wanyonge.
Ni bahati mbaya, pamoja na ukali wake, Jiwe aliondoka bila hata kumnyaka mmoja wa wale waliojulikana kama wasiojulikana ingawa walikuwa wakijulikana.
Kama wanaharakati huru ambao hawakuwa huru bali udhuru walijulikana, iweje wauaji wasiojulikana wasijulikane kwa lisrikal lenye kila aina ya wataalamu wa uchunguzi na udukuzi.
Sina haja ya kumlaumu marehemu. Cha mno, historia huwa haina huruma wala upendeleo. Huripoti kitu kama kilivyofanyika au kutokea.
Kwa muktadha huu, sasa najikita kwenye jinai, uchafu, na unyama wa kutekana na kutoana roho kwa mambo ya kidunia kana kwamba kuna atayeishi milele.
Ni kama tumekubali kutekwa na kugeuka mateka wa watekaji wetu. Je, hawa ni nani, wanatoka wapi, kwa nini wanaua mafyatu hovyo, wanatumwa, wanajituma, na nani anawalea hawa maafriti nduli wakubwa? Je, vyombo vyetu vya uhasama, sorry, usalama, navyo viko wapi?
Ndata wetu ambao mara nyingi wamejionyesha kushabikia na kutumiwa na chata fulani nao wako wapi? Je, tutaendelea kukubali kuwa mateka wa wahuni wachache hata kama wanaowatuma wanaweza kuwa na maulaji?
Maana haieleweki mafyatu wanyotolewe roho mchana kweupe na hakuna anayeshikwa. Je, lisrikal liko wapi? Je, nalo linahusika?
Kwa nini wanaotekwa na kunyatuliwa roho ni wa chata moja kati ya utitiri wa vyata vya upingaji? Je, huu ni mchezo mchafu wa siasa? Je, mafyatu wa kaya hii wakimbilie wapi? Kwa taarifa zilizopo ni kwamba kaya ishapoteza takriban mafyatu 80. Je, wafe wangapi ndo wahusika wastuke na kutenda haki hata kusitisha kadhia hii? Maswali ni mengi kuliko majibu.
Yeyote anayewatuma, sababu zozote zinazowasukuma, yeyote anayewalea anapaswa kujua kitu kimoja.
Wanaweza kumgeuka naye akajikuta kwenye waathirika sawa na wengine. Kabla ya kupinduliwa, Obote hakudhani kuwa uhuni lingekuwa tatizo lake wala jambo ambalo lingemfyatua na kumtemesha ulaji.
Hivyo, nasi, tunapaswa kuwa makini kama mafyatu wenye akili timamu na tunduizi wanaoisoma historia na kujifunza namna ya kutatua baadhi ya matatizo kama hili la utekaji wa kaya na mafyatu wake.
Haiwezekani mafyatu wafyatuliwe kila uchao halafu tunaambiwa mambo poa. Hivi hawa waathirika wa utekaji huu siku watakapokengeuka hali itakuwaje? Mafyatu si wanyama, wadudu wala mataahira.
Ni viumbe wanaobadilika na wasiotabirika. Hata hawa waliobadilikiana na kugeuziana kibao ni mafyatu kama hawa wanaofyatuliwa na hawa wahuni.
Kwa vile huwa nasikia kuwa rahis wetu ni msikivu, si vibaya kumpa ushauri wa bure kuwa hali hii isipokomeshwa, upo uwezekano wa kuwachochea mafyatu ambao wanajiona kama wahanga wasio na mtetezi wala pa kwenda, kuamua kufyatuka na kuwatafuta hao wanaowateka ili nao wawateke waonje ladha ya dawa yao.
Nadhani wanachosahau hawa watekaji, watesaji na wauaji ni kwamba wao ni mafyatu, tena wenye familia, ndugu, jamaa ambao wanaweza kujikuta katika ulipizaji visasi, mbali na kutaka kukomesha hii jinai na dhuluma.
Kwa nini tunaweza kupata ndata wa kuzuia maandamano au kukamata ng’ombe kwenye mbuga za wanyama, lakini hawapo wa kukamata watekaji au nao wametekwa bila kujijua?
Uadui, hata ugomvi wa kisiasa humalizwa kisiasa na si kihuni na kikatili hivi. Hii ni aibu kwa kaya yote.
Je, tumeishiwa kiasi hiki hadi tunatekwa na watekaji kiasi cha kugeuka mateka wa wawatekaji?
Tumalizie. Chondechonde, msiharibu sifa nzuri ya kaya yetu. Maulaji yana mwisho.
Na isitoshe, hakuna atakayeyafaidi wala kuishi milele.
Kuna haja ya kujirudi na kuachana na uhuni wakati huu ambapo mnaweza kuwapa sababu baadhi ya wahuni na maadui wasioitakia kaya yetu mema kuanzisha machafuko na vita uchwara kama kule Somaliya.
Tunafahamiana hapa? Hivi ni asubuhi au usiku?