Jitafakari kama uliyenaye ni rafiki wa kweli
Leo tukumbushane kidogo kuhusiana na marafiki tunaowachagua kwenye maisha yetu, ambao mara nyingi tunawaamini na kuwashirikisha kwenye mipango tunayopanga kwa asilimia kubwa.
Si kitu kibaya kuwa na marafiki wa kubadilishana nao mawazo kwenye harakati za kujitafuta, isipokuwa kuna haja ya kuwasoma vizuri ili kutambua uhalisia juu ya uwepo wao kwenye maisha yetu.
Si rahisi kuwatambua, lakini zipo ishara zitakazokuonyesha hilo.
Kuna ishara za kuwatambua marafiki wa kweli na feki, endapo tu kama umakini wa kuwasoma utatumika bila kupuuza ishara wanazozionyesha, katika vipindi tofauti vinavyotokea kwenye maisha.
Wakati mwingine watu hawatabiriki.
Kuna wengine ukiwa unajitafuta wanakuwa sambamba kukupa moyo wa kuamini ipo siku utafanikiwa, lakini ukianza kuonyesha matunda utaona utofauti wa kutopendezewa na hatua zako.
Hilo lisikutishe ni moja ya ishara ya kuwafahamu kile walichokuwa wamekificha ndani ya mioyo yao, kwamba hawakumaanisha maneno yao zaidi ya unafiki, ukiona hivyo utajifunza kupunguza kuanika mambo yako kwake.
Hapa unakuwa umeshajua rafiki yako huyo feki yupo kwenye kundi la wanaotaka ufanikiwe, lakini siyo kuwashinda wao.
Kuna kundi la watu wengine ambao wanakukatisha tamaa kwenye mwanzo wako, lakini baada ya kufanikiwa wanaanza kujisogeza na kuona unastahili kuwepo kwenye hiyo hatua.
Hawa hubadilika kabisa kadiri unavyofanikiwa na kuwa katika kundi la chawa.
Hapo sasa kazi yao kubwa itakuwa ni kukusifia tu na kukujaza ujinga, wakijua fika utalewa sifa na kupotea badala ya kuwa imara zaidi.
Ukiona uliyemuamini kuwa ni rafiki yako, nyakati za kujitafuta kwa machozi, jasho na damu aliingia mitini na sasa anarudi kwa staili ya uchawa, muogope sana anataka kukuzamisha.
Maana atakusifia kiasi cha kukutoa maana mbele ya macho ya jamii. Ninachotaka kusema ni kuwa jitafakari, jichunguze rafiki uliye naye ni sehemu ya maisha yako kama anavyokuaminisha?
Hii inatokana na kuwaamini marafiki tulionao na kuwaambia kila kitu, huku akikupaka ubaya mahali inakuwa rahisi kuaminiwa kwa sababu anakuwa na mifano hai ya namna anavyokufahamu.
Mfano mzuri ni kisa cha mwanamuziki wa Afrika Kusini, Rapa AKA aliyefariki kwa kupigwa risasi, huku taarifa zikiwahusisha marafiki zake kutoa mchongo wa kifo chake, tukio hilo lilitokea Februari mwaka huu.
Kuna rapa mwingine chipukizi kutoka nchini Nigeria, Ilerioluwa Oladimeji Aloba 'MohBad', kifo chake kina utata, huku marafiki zake wakihusishwa na tukio hilo na baadhi kukamatwa kwa uchunguzi zaidi.
Mifano hiyo inatufunza namna ya kuanza kuwachambua watu tunaostahili kufanya nao safari ya maisha yetu.
Tusichanganye marafiki na watu tunaokutana nao maishani.
Bora uwe na mzunguko wa watu wachache kuliko kuwa nao wengi wasiokutakia mema pembeni, huku wakikuchekea usoni.
Pamoja na marafiki wa aina hiyo, pia wapo wa kweli ambao huenda ndio wanaopuuzwa, kwani mara nyingi wanakuwa hawatumii nguvu kubwa ya kukuonyesha upendo wao wa dhati, zaidi ya matendo yaliyonyooka.
Hawa kuna wakati wakiwa sirini wanamuomba Mungu, hutuombea nasi kwa sababu wanatupenda na kutuchukulia kama sehemu ya maisha yao.
Kuna haja wakati unatumia muda wako kuwekeza kwenye vitu unavyoamini vinaweza kukutoa kimaisha, kipengele cha marafiki kikumbukwe kusoma ishara zao ili kuepuka usumbufu mbele ya safari.
Ishara nyingine ya kutambua rafiki wa kweli ni yule anayekuwepo na wewe kwenye nyakati ngumu na zenye furaha, hawezi kukaa mbali nawe wala kutoa aibu zako nje.
Ukiachana na marafiki, kuna ndugu na jamaa wanaoweza wakasababisha tufurahie maisha yetu ya mafanikio ama kuharibikiwa, pia unaweza ukawatambua kwa maneno na vitendo vyao.
Kuna kila sababu ya kuanza kuwachambua watu sahihi kwenye maisha yetu, hilo litafanya tuwe salama zaidi, kuliko kupuuza baadhi ya mambo ambayo yanaweza kutugharimu.
Tunapaswa kujifunza subira ya kutotoa kwa haraka mambo yetu mbele ya marafiki zetu, wakati mwingine ni vizuri kuwashangaza kwa kushtukia baadhi ya mafanikio yako.
Wingi wa marafiki ndio wingi wa aibu yako, itakapofika hatua ya wengi uliodhani ni marafiki wa kweli mkitofautiana mambo yako anayaanika hadharani, huyu pia achana naye, atakuingiza shimoni siku ukija kumueleza jambo la hatari.
Marafiki hawawezi kuharibu mambo ya uchumi pekee, wapo ambao wameharibu hadi mahusiano kwa kutumia udhaifu wako wa kukujua kiundani.
Visa vya marafiki kuchukuliana wenza vipo wazi na vimekuwa vikiripotiwa, wengi wakilia na watu wao wa karibu ambao waliwaamini, lakini mwisho wa siku waliwageuka na kuwa wasaliti.
Hivyo anayebahatika kupata rafiki wa kweli anakuwa amepata kitu cha thamani sana na mambo yake kuwa salama, kinyume chake ni kujitafutia matatizo na maumivu ya moyo bila sababu.