Kuchanganya maiti ni uzembe, uepukwe

Gazeti hili jana lilichapisha habari ya tukio la ndugu kupewa na kuzika maiti isiyo ya ndugu yao, likiwa ni tukio la pili ndani ya siku 10 kuripotiwa.

Katika tukio la jana, familia ya marehemu Gudluck Munuo (53), mkazi wa Kijiji cha Mese, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro imechukua maiti ya Eliudi Mbaga (68) iliyokuwa imehifadhiwa katika Hospitali ya Kibong'oto na kwenda kuzika.

Katika tukio hilo lililotokea Mei 26, mwaka huu, wanandugu hao bila kujua walichukua maiti ya mkazi huyo wa Kijiji cha Matadi na kuuzika na nduguze (Mbaga) walipokwenda kuufuata mwili huo, waligundua umeshachukuliwa, ndipo wakaanza kuufuatilia kwa kushirikiana na uongozi wa hospitali hiyo.

Mambo ni yaleyale, hata katika tukio lililotokea Mei 18 na kuripotiwa na gazeti hili Mei 20 katika Mkoa wa Morogoro, mwili wa mzee Melkior Ndambale (85) ulichukuliwa na wasiokuwa nduguze na kwenda kuuzika Kilosa.

Kama vile ilivyokuwa Siha, ndugu zake Ndambale walipokwenda kufuata mwili wa ndugu yao wakakuta umeshachukuliwa.

Baada ya uongozi wa ya Rufaa Mkoa wa Morogoro kufuatilia katika vitabu uligundua mwili huo ulichukuliwa na familia moja ambayo pia ilikuwa na imemhifadhi baba yao hapo na kwenda nao Kilosa kwa ajili ya mazishi (Ikaacha ya baba yao).

Katika matukio yote mawili, ambayo sisi hatuna maneno mengine zaidi ya kusema ni ya kizembe, ilibidi zifanyike taratibu za kisheria na kwenda kufukua miili hiyo na kuirejesha katika maeneo stahiki.

 Haya si matukio madogo katika mila na destuli, sheria umani zetu za dini. Ni masuala mazito na nyeti yanayoibua hisia za wananchi na kuingilia hata masuala ya imani.

Mathalan, katika tukio mojawapo, maiti iliyochukuliwa kimakosa ni ya mtu aliyekuwa na imani ya Kikristo lakini ilikutwa imeshazikwa kwa taratibu za maziko kwa Kiisilamu; kwa ujumla ni masuala ambayo yanaweza kuleta taharuki zisizo za msingi.

Kutokana na uzito wake ni masuala kama haya yanapaswa kuepukwa kwa viwango vyote kwa kuwekewa utaratibu wa kuhakiki kila hatua inayochukuliwa.

Kwa kawaida jibu linaloweza kutolewa kirahisi na hospitali husika au wahudumu wa mochari ni kwamba kitendo hicho kimetokea kwa bahati mbaya, lakini sisi tunasema hizo ni bahati mbaya zinazopaswa kuepukwa.

Ingawa inaelezwa kwamba mojawapo ya sababu za changamoto hiyo ni kwamba wanaopeleka maiti hospitali si wale naokwenda kuzifuata, jambo hilo linapaswa kuwekewa utaratibu, kwamba waende watu wanaomfahamu vizuri marehemu, hasa ndugu wa damu au wa karibu na inapowezekana wale walioupeleka ndiyo wauchukue.

Hii ni kwa sababu mbali na kuzua hisia na taharuki, matukio hayo yanasababisha usumbufu na gharama si tu kwa familia za marehemu bali pia kwa uongozi wa hospitali na mamlaka mbalimbali za Serikali katika kuhakikisha utulivu unakuwepo katika pande mbili zinazohusika.

Ili kuepuka yote hayo ni muhimu ukawekwa utaratibu ambao ni lazima ufuatwe kabla ya kuchukua mwili wowote wa marehemu na pale utaratibu huo unapokiukwa, mhusika awe anajua kuwa kuna adhabu kali inayomsubiri.

Ikiwa utaratibu huo upo, basi ujulikane, ufuatwe na kusimamiwa vizuri na wale waoukiuka wapewe haki yao ya kuwakumbusha kuuzingatia kwa kila hatua.

Kama kuna mianya katika utekelezaji izibwe ili matukio hayo yakomeshwe.