Maisha ni hadithi, je, simulizi ya maisha yako inasomeka?

Muktasari:

  • Kuna wakati mwingine tunadhani alama za kukumbukwa zinapaswa kuachwa na watu fulani wenye ngazi kubwa serikalini ama sekta binafsi, ila ukweli ni kwamba kila mtu anaweza akawa na alama ya kusimuliwa na kuigwa kwa nafasi yake.

Je, umewahi kujiuliza kuna alama gani hai za kukumbukwa kwenye maisha yako, iwe ngazi ya familia, mahala pa kazi utakayoiacha?

Ama  mahusiano yako na  watu wanaokuzunguka, kwenye ndoa au  uchumba unaamini yana alama yoyote? Kama hujui jiulize na kama unajua jiulize pia ni alama ipi utaacha duniani.

Kuna wakati mwingine tunadhani alama za kukumbukwa zinapaswa kuachwa na watu fulani wenye ngazi kubwa serikalini ama sekta binafsi, ila ukweli ni kwamba kila mtu anaweza akawa na alama ya kusimuliwa na kuigwa kwa nafasi yake.

Mfano linapotajwa jina la muasisi wa Taifa la Tanzania, hayati Mwalimu Nyerere wengi wetu kitu kikubwa kinachotujia kichwani  ni namna alivyopambana kuleta uhuru wa nchi hii. Pia alivyokomesha ukabila na mataba miongoni mwetu na kutujenga kuwa kitu kimoja.

Hata tunapopingana, kubishana huwa ni kwa hoja na si vihoja ndiyo maana mtu akifanya kitu tofauti huonekana wa ajabu.

Ndiyo tunaweza kusema alifanikiwa kufanya hayo kwa sababu ya nafasi yake ya uongozi, lakini kuna watu wa kawaida alishirikiana nao na sasa wanakumbukwa kwa hilo.

Mfano mwingine ni  mwanamama Oprah Winfrey mtangazaji na mmiliki wa mtandao wa Oprah.com ambaye amekuwa akifanya mahojiano na watu mbalimbali akiwamo Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama. Pia alifanya  na mwanamfalme wa Uingereza Prince Harry na mkewe Meghan, ambao waliamua kujitenga na jumba la mfalme na kwa mara ya kwanza walieleza sababu za kujiondoa kwenye jumba hilo na kuishtua dunia.

Historia ya Oprah, alizaliwa kwenye familia ya kimaskini na kulelewa na mama yake pekee, kama haitoshi aliishi maisha   ya mtaani ambapo alipata mimba akiwa na miaka 14, hilo halikumkatisha tamaa. Alipambana na sasa ni mfano wa kuigwa kwa wanawake wengi, wenye ndoto kubwa kuamini aibu ya leo inaweza ikawa baraka ya kesho.

Jambo kubwa la kujifunza ni nafasi yoyote uliyonayo iwe unafanya kazi za ndani, ofisini, mfanyabiashara ziwe ndogo ama kubwa hakikisha unaacha alama ya kusimuliwa na kuwa  mfano wa kuigwa na wengine.

Usiamini kuwa ukiwa kwenye nafasi kubwa ndiyo unaweza kufanya mambo yatakayoacha  alama, ndiyo maana siyo kila mwenye nafasi anaweza akaacha kumbukumbu nzuri.

Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi aliwahi kunukuliwa akisema “Maisha ni hadhithi, tujitahidi kuacha simulizi nzuri kwa wenzetu” mwisho wa kunukuu.

Hii ina maana popote ulipo katika safari yako ya maisha jitahidi uache hadithi nzuri kwa watakaoisikiliza.

Kuacha alama siyo lazima isimuliwe ukiwa haupo duniani, bali ni namna ambavyo unakuwa mkombozi kwa watu wanaokutazama kama mfano wa kuwatatulia changamoto zao ama kuwapa majibu ya maswali yao kulingana  na mazingira yanayowazunguka.

Labda tuulizane kwa wale wenye mahusiano baina ya mwanamke na mwanaume mnapokuwa wawili mnazungumza vitu gani vya kuacha kumbukumbu kwa mwenzi wako.

Kwa maoni yangu inawezekana ukaacha vitu vyenye afya ya akili ama maumivu ya moyo, na hivyo ndivyo wanavyofanya wengi kuyapa matatizo nafasi badala ya kufurahia angalau fursa ya kuwa pamoja.

Kutokana na changamoto za kimaisha na mahangaiko ya hapa na pale, mtu anapokutana na mwenzi wake anakuwa anatarajia asahau yaliyoumiza akili yake na aanzeni upya, lakini wengi wetu tunakosea na kudhani ni muda wa mashtaka, malalamiko hiyo ni moja ya sababu ya wengi wao kupunguza muda na wenza wao na kutafuta vitu vinavyowapa furaha.

Hapa napo ni pa kujiuliza, unadhani kwa kufanya hayo utakuwa umeacha alama yoyote kwenye uhusiano wenu utakapovunjika au mmoja kati yenu akitangulia mbele ya haki.

Basi tukijiuliza tunaweza tukawa na mwanzo mpya wa kuacha alama bora kwao  na kutumia fursa ya kuwa pamoja kwa kufurahia maisha.

Aliyewahi kuwa rais wa Marekani, Barack Obama aliwahi kusema kuwa mtu mzuri kwa mwenza wako anaweza akawa mchumba, mume ama mke, mtazamo wako imara unaweza ukamfanya akawa mtu fulani wa kuigwa duniani, hilo litafanyika tu kutokana na kumbukumbu nzuri anayoachiwa kwenye akili yake, itakayomfanya athamini uwepo wako na awapo mbali kukumbuka msaada wako wa kiakili.

Tujitahidi kwenye uhusiano pia tuache hadithi nzuri inayovutia kuisikiliza, badala ya migogoro isiyo na kikomo.

Pengine huko ni mbali sana  je,  vipi kuhusiana na familia unayotokea umeacha alama ya kukumbukwa uwepo wako unapokuwa haupo, ndugu zako wawe wanalitaja jina lako kwa uzuri na kukuhitaji zaidi usipokuwepo, au wanatamani ubaki huko huko ulipo.

 Bado hutujachelewa  kuanza kubadili mitazamo yetu na kuwa watu wenye nguvu ya manufaa kwa familia,  jamii, Taifa kwa kufanya vitu imara na vizuri ambavyo vitaacha alama kwa wale wanaotuamini  kwenye nafasi tulizopo.

Mifano mingine hai ni ile inayotunzunguka kila siku, kuna watu wanapofariki kwenye jamii zetu watu wanaumia na kupoteza matumaini kumpata mbadala wake, pia wapo ambao wakiondoka duniani inakuwa kheri kwa wanaobaki kutokana na aina ya maisha waliyochagua kuishi.

Hayo yote yanatukumbusha kuwa watu wema tunapokuwa mahali popote ili tuache alama ya kukumbukwa.