Maisha ya mtandaoni ni sehemu ndogo ya uhalisia

Maisha ya mtandaoni ni sehemu ndogo ya uhalisia

Muktasari:

  • Utafiti wa Statista 2021, shirika la Kijerumani la kuhifadhi matumizi ya data na masoko mtandaoni kwa nchi 170 duniani unaonyesha kuna watu bilioni 4.66 wanaotumia mitandao ya kijamii.

Utafiti wa Statista 2021, shirika la Kijerumani la kuhifadhi matumizi ya data na masoko mtandaoni kwa nchi 170 duniani unaonyesha kuna watu bilioni 4.66 wanaotumia mitandao ya kijamii.

Hii ina maana asilimia 59.5 ya watu wote duniani wanatumia mitandao ya kijamii. China, India na Marekani zinaongoza kwa matumizi ya intaneti. China pekee, zaidi ya watu milioni 854 wanatumia mitandao, India zaidi ya watu milioni 560 wanatumia mitandao.

Hii inaonyesha namna isivyo rahisi kukimbia mabadiliko ya kiteknolojia yaliyozalisha mitandao hii ambayo ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku.

Unapozungumzia mitandao ya kijamii unajumuisha Facebook, Instagram, Telegram, Wechat, Twitter na Whatsapp inayowakutanisha watu na kuwafanya wapate taarifa na kuisambaza. Urahisi wa mitandao ya kijamii upo katika kutumiana taarifa kwa haraka zaidi, tofauti na hali ilivyokuwa kabla ya kuwapo kwake.

Simu za kisasa zimechukua sehemu ya maisha ya watu wa karne ya 21, hivyo kuchangia uraibu wa mitandao ya kijamii kuwa mkubwa. Mtu akituma kitu basi anangoja maoni ya wengine na ‘likes’ zao.

Kutokana na shauku ya kujua maoni ya wengine kuhusu picha au ujumbe alioutuma mtandaoni, kurudirudi mtandaoni kumekuwa kukubwa, hivyo kuongeza matumizi ya mitandao hii.

Saikolojia ya kuwavutia watu kuirudia mitandao ya kijamii ni sayansi ya kemikali iitwayo dopamini ambayo hutoa furaha inayompa mtu kujisikia vizuri anapofanya kitu na kujisikia vizuri kunamfanya aitafute hali hiyo tena na tena. Hivyo kemikali hii inatoka zaidi pale mtu anapojisikia vizuri na hivyo inamhamasisha kukirudia kitu.

Hivi ndivyo mitandao ya kijamii ilivyofanywa katika kuwanasa watu watume picha, wasambaze kitu na wangoje watu watoe maoni yao. Hili humfanya mtu aendelee kuhamasika kutuma picha iwe ni Instagram au Whatsapp Status na kuona watu wangapi wataona. Kadri watu wanavyotoa maoni ndivyo anahamasika zaidi na zaidi kuwa mteja wa mtandao na kujenga matarajio ya wasomaji au wafuasi wa kile anachokituma.

Mitandao ya kijamii imeibua mtindo wa maisha wa watu kutuma upande mzuri tu wa maisha yao kwa kushirikisha picha za matukio au maisha wanavyoishi bila kujua wanachoshirikisha ni sehemu ndogo ya nyuma ya pazia ya maisha halisia.

Ukipita katika mitandao ya kijamii utaona matukio yanayotumwa na watu yenye kuonyesha maisha yao yanaendelea vizuri. Watu wengine huingia gharama kuigiza maisha mtandaoni ili waonekane ni wa hadhi fulani au wa maisha fulani kumbe kiuhalisia hayapo hivyo. Wanaoumia ni wale wafuasi wa watu wenye ushawishi fulani kufanya mambo kwa kuiga wasijue kinachooneshwa ni sehemu ndogo ya maisha halisi.

Ongezeko la watu kujisikia vibaya au huzuni limekuwa kubwa wanapoona wengine wanashirikisha matukio au picha na mambo yanawaendea vizuri huku kwao wanapitia maisha magumu na changamoto nyingi.

Utafiti unaonyesha mitandao ya kijamii imeongeza idadi ya watu wanaogua sonona, ugonjwa unaotokana na msongo wa mawazo wa kulinganisha maisha yako na ya watu wengine.

Wengi wanajihisi hawana maana ya maisha. Wanakata tamaa na wengine kujihatarishia maisha kwa sababu ya kufuatilia maisha ya watu waliofanikiwa kimaisha, wanaoamini wana utajiri hata kama kiuhalisia hawako hivyo.

Hutaona mtu anatuma uhalisia wa maisha yake au mchakato wa jambo husika, bali matokeo tu ya anachokifanya. Uhalisia unafichwa usionwe kwa wafuatiliaji wa ukurasa wake.

Mbali na kuficha uhalisia wa maisha, bado mitandao hii inatoa fursa zenye manufaa makubwa kwa zama tuishizo sasa. Watu wanatumia mitandao ya kijamii kutangaza biashara na kutafuta wateja, kukuza mtandao wa watu, kutafuta kazi na ajira, kusambaza habari na kusambaza maudhui ya kielimu na maarifa.

Ni muhimu kuwa makini na kuchuja taarifa na habari zinazosambazwa mitandaoni kwa kujihakikishia chanzo cha habari, maudhui kabla ya kuisambaza kwa wengine.


Mwandishi ni daktari wa binadamu jijini Mbeya. Kwa maoni na ushauri, anapatikana kwa namba 0676 559 211