Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matabaka ya walipa kodi hayajengi nchi

Muktasari:

Katika dunia ya sasa pamoja na mambo mengine, huwezi kupinga suala hili. Serikali yoyote duniani inaendeshwa kwa kodi.

Rais wa 37 wa Marekani Richard Nixon aliwahi kusema: “Hakikisha unalipa kodi, vinginevyo unaweza kujikuta katika matatizo makubwa.’’

Katika dunia ya sasa pamoja na mambo mengine, huwezi kupinga suala hili. Serikali yoyote duniani inaendeshwa kwa kodi.

Ndiyo maana alipoingia madarakani, Rais John Magufuli alifanya mabadiliko katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yenye jukumu la kukusanya kodi nchini.

Baada ya hapo alikutana na wafanyabiashara na wamiliki wa taasisi binafsi nchini kama wahusika wakubwa wa kodi, achilia mbali wafanyakazi na watumishi wengine wa Serikali ambao kodi zao ni nyepesi kupatikana kwani wengi hukatwa moja kwa moja katika mishahara yao.

Siku alipozungumza na wamiliki wa sekta binafsi na wafanyabiashara alikuwa na uso wa tabasamu ila alipofika katika kipengele cha kuwaasa walipe kodi, sura yale ilikuwa na mkazo zaidi.

Rais alisisitiza kulipa kodi na bado kila siku anazidi kuwaasa Watanzania kuwa na hulka ya kulipa kodi.

Chanzo kikuu cha mapato ya Serikali ni kodi na kwa kupitia mapato hayo ndiyo yanayotumika katika nyanja mbalimbali za maendeleo kama elimu, afya, miundombinu na nyinginezo. Bila kodi huduma hizi hazifiki kokote.

Katika taifa hili kuna watu kwa dhati kabisa na mioyo yao ya kiuzalendo wana tabia ya kulipa kodi, wengine kwa kushirikiana na watumishi wa Serikali wasiokuwa waaminifu hukwepa kodi jambo ambalo huleta kikwazo katika maendeleo ya taifa.

Hapo awali waligeuza nchi kijiwe cha kupiga ‘dili’ waliunganisha nguvu zao kutakatisha maovu na wale waliokuwa na mapenzi dhidi ya nchi yao, waligeuzwa mbuzi wa kafara.

Waadilifu na waaminifu, walichukiwa hadi kuitwa maadui wa nchi, ilifika wakati wema walionekana wabaya.

Sheria ni msumeno, ni vyema kila mtu akalipa kodi. Nchini Marekani, hata mshahara wa rais hukatwa kodi. Waziri Mkuu wa Uingereza analipa kodi kama raia mwingine.

Tena kwa wenzetu sifa mojawapo ya kuwa kiongozi ni historia ya kulipa kodi tofauti na hapa kwetu, viongozi wakiwamo wabunge ndiyo wanaoongoza kukwepa kodi, watapendekeza walipwe milungula ya fedha, lakini wasikatwe kodi.

Wabunge hawana budi kuwa mfano katika suala la kulipa kodi kupitia posho na mishahara yao. Hii itakuwa ishara na picha ya mioyo ya uwajibikaji kuwa wao ni viongozi wa mifano na wazalendo.

Isifike wakati tukasimamia katika nguzo kuwa mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe bila kushirikana na viongozi. Taifa litajengwa na Watanzania wote.

Katika mataifa yaliyoendelea suala la kukwepa kulipa kodi ni sawa na kosa la ubakaji hapa kwetu. Pia, hata suala la misamaha ya kodi halipo, kila mtu ana wajibu wa kulipa kodi.

Hapa kwetu mzigo mkubwa wa kodi ni kwa wananchi wa kawaida, huku viongozi ambao walipaswa kuwa mfano wakitembea vifua wazi kwa kutolipa kodi. Na wanajisikia fahari katika hili na likija pendekezo la wao kulipa kodi hulipinga kwa nguvu zote.

Katika kuijenga Tanzania ni lazima wote tushikamane, si vema taifa likawa na matabaka ya walipa kodi, wengine watwishwe mzigo huku wengine wakiwa na misamaha ya kodi chini ya miamvuli ya uongozi au nyadhifa fulani.

Tusiwatupie lawama wafanyabiashara kama wakwepa kodi, kumbe kuna wengine hawalipi kwa kisingizio cha uongozi. Kila mtu aliye katika ardhi ya Tanzania ajisikie fahari kulipa kodi.

Noel Shao ni mchambuzi wa masuala ya jamii na siasa nchini 0769735826

Kwa taarifa zaidi nunua gazeti lako la Mwananchi au soma mtandaoni kupitia www.epaper.mcl.co.tz