Mitishamba ya kuongeza uchungu hatari kwa wajawazito

Mitishamba ya kuongeza uchungu hatari kwa wajawazito

Muktasari:

  • Matumizi ya dawa za miti shamba yalikuwepo tangu enzi za mababu zetu, zilisaidia kutibu magonjwa mbalimbali.

Matumizi ya dawa za miti shamba yalikuwepo tangu enzi za mababu zetu, zilisaidia kutibu magonjwa mbalimbali.

Hata sasa kuna baadhi ya watu wanaendelea kutumia miti shamba kwa ajili ya kutibu magonjwa mbalimbali, ikiwemo homa, lakini kuna baadhi wanaofanya matumizi mabaya ya dawa hizo za asili.

Kwa mfano wajawazito wengi wanaoishi maeneo ya vijijini na hata pembezoni mwa miji, hawaendi katika vituo vya afya kwa ajili ya kupata huduma za mama na mtoto wakiamini kwamba wakitumia miti shamba wataweza kujifungua salama majumbani.

Baadhi ya wajawazito pia hutumia dawa hizo kutibu minyoo na kuongeza uchungu muda wa kujifungua ukifika, hivyo kusababisha vifo vya wanawake na wakati mwingine kwa watoto wao.

Kwa mujibu wa Mratibu wa mama na mtoto katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Caroline Maliseli dawa hizo ni kali na kuwa mjamzito anapozitumia kutibu minyoo husababisha kupasuka kwa mfuko wa uzazi na kufanya mtoto tumboni kunywa maji machafu na mwisho wa siku yanamsababishia kifo akiwa bado yuko tumboni hajazaliwa.

Alisema asilimia kubwa ya vifo vya wajawazito na watoto katika Manispaa ya Kahama vinatokana na uwepo wa matumizi ya dawa za miti shamba ambazo zimekuwa zikitumiwa na wajawazito.

Maliseli alisema kwa mwaka jana vifo vya watoto waliozaliwa wakiwa wamefariki na wengine kufariki ndani ya siku saba vilikuwa 266, huku vya wajawazito vikiwa saba.

Alisema vifo chini ya mwaka mmoja vilikuwa saba, zaidi ya mwaka mmoja 35 na vifo chini ya miaka mitano vilikuwa 115.

Alisema kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, vifo vya wajawazito vilikuwa viwili, vifo vya watoto ndani ya siku saba 12, vifo vya watoto wafu (wanaofia tumboni kwa mama zao) 54.

Mratibu huyo wa Mama na Mtoto alisema wamekuwa wakiwakamata wajawazito na dawa hizo wakitumia kwenye chai, maji ya kunywa na kwenye machupa ya kuhifadhia vinywaji.

“Hivi karibuni tulimpokea mjamzito aliyekuwa amepasuka mfuko wa uzazi na mtoto amefia tumboni, baada ya kumsaidia na kumhoji zaidi alidai alipewa dawa za miti shamba za kuongeza uchungu na mama mkwe wake na ilikuwa mimba ya kwanza,” alisema Maliseli.

Ili kuondoa tatizo hilo, elimu inahitajika kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa miji kwa kuwaeleza madhara makubwa yanayopatikana pale mjamzito anapotumia dawa za miti shamba kuongeza uchungu wakati wa kujifungua au kutibu minyoo.

Tatizo hili ni kubwa na limekuwa likijitokeza mara kwa mara kwa wajawazito hao na kuonyesha dawa hizo zinatumika wamekuwa wakifika nazo hospitali kwa kificho na kutumia kwenye chai ambapo mwisho wa siku uchungu kuongeza ambapo mama hujifungua mtoto huku mfuko wa uzazi umeshapasuka.

Wadau wa afya wafike maeneo ya vijijini waendelee kutoa elimu kwa wanawake kuhusu madhara ya matumizi ya miti shamba kuongeza uchungu kwa kuwa licha ya kuhatarisha maisha yao, wanahatarisha maisha ya watoto wao.

Pia wakati wa kipindi cha wajawazito kuhudhuria kliniki, wataalamu wa afya watumie kipindi hicho kutoa elimu kwa wajawazito kuachana na matumizi ya dawa hizo kwa kuwa kuna wengine hujifungulia njiani kwa sababu ya matumizi ya dawa hizo.

Masharika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi za kutoa huduma za afya ngazi za jamii, ikiwemo Shirika la Shdepha+ na Tulonge afya wahakikishe wanashirikiana na Serikali katika kupambana na uwepo wa matumizi ya dawa hizo zinazosababisha vifo kama wanavyotoa elimu ya kujikinga na ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) na Ukimwi.

Elimu hiyo itolewe kwa vijiji vyote vilivyopo nje hata ya Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Ushetu na Halmashauri ya Msalala kwa kuwaeleza wananchi dalili za hatari, maandalizi ya kujifungua na kuhudhuria kliniki kabla na baada ya kujifungua, ili kuendelea kuangalia maendeleo ya mtoto na mama.

Ushirikiano baina ya wananchi, wadau wa afya na Serikali unaweza kuokoa maisha ya mama na mtoto kwa kupinga vikali matumizi ya dawa za mitishamba zinazotumika kuongeza uchungu wakati wa kujifungua.