Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwaka 2024 unaondoka umejitafakari?

Kila tunapofikia tamati ya mwaka, imekuwa ni hulka ya wengi kutulia na kufanya tathmini juu ya hatima ya maisha yetu.

Ni ishara nzuri kufanya tafakuri yakinifu kuhusu changamoto zilizojitokeza, mafanikio yaliyopatikana katika malengo ya kibinafsi na kitaasisi ambayo yaliwekwa mwanzoni mwa mwaka.

Ni zaidi ya umuhimu, kuwa na utamaduni huo wa kujikagua mara kwa mara.

Naam, ni vigumu mno kujikabili wenyewe; hasa katika aibu zetu, vilema vyetu, kushindwa kwetu na sehemu ya historia zetu hasi.

Kuna maumivu ya kukubali kuwa wakati mwingine sisi wenyewe ndiyo tatizo kubwa, hivyo kufanya kazi hii ya kujitathmini iwe ngumu sana.

Mtu anahitaji ujasiri na ukomavu kujikabili na kujisaili nafsi na nafasi yake hapa duniani. Ukifaulu hofu ya kukikabili kivuli chako cha kuacha kuchukulia mrejesho hasi kama chuki, wivu na husda, na kutokuwa wepesi kuwageuzia kibao wale wanaoyaona matatizo yetu, hapo ndipo safari ya kujitambua inapoanza.

Baadhi ya maswali ya msingi ambayo hayakwepeki katika safari ya kutafiti lile lengo mahususi la uwepo wetu duniani ni kama; je, uwepo wangu duniani una maana na una lengo gani?

Je, nisingezaliwa ni ombwe gani ningesababisha? Je, siku nikifa, ni pigo na pengo gani nitaacha? Je, mchango wako ni upi na unajulikana kwa lipi?

Je, una ndoto fulani ya maisha au wewe ni bora liende tu? Ukipewa nafasi ya mwisho kuishi utarekebisha nini?

Huu mchakato pevu na endelevu wa kujifahamu mwenyewe ni tabia ya lazima na ndio ni kiini cha falsafa ya mwanafalasfa Sokrates.

Aliamini kuwa kabla ya kuutafiti ulimwengu, ni vyema binadamu ajitafiti mwenyewe kwanza.

Moja ya raha na mahaba ya binadamu ni kujinenea mazuri na kujitabiria siha njema juu ya maisha yake.

Aghalabu, tunakimbizana na upepo wa miadi, ahadi kemkem na kukutana na watu ili tusikike na kuthaminiwa, lakini pengine tunasahau, tunapuuza au kuogopa kukutana na nafsi zetu kwa sababu zinaanika vidonda na udhaifu wetu

Tupo ‘bize’ kutafuta riziki mpaka tunakosa muda wa faragha na mapumziko. Ni hatari, kukosa ule utulivu na kuogopa ukimya ili ujisikilize, ujikague na kuzama hadi kwenye fundo la moyo wako, kwenye kioo cha ndani.

 Upweke si ukiwa. Kuna nyakati huwezi kukutana na ‘wewe’ bila kuwa peke yako. Mwanasaikolojia wa Kiuswisi, Carl Jung aliwahi kusema kuwa matatizo mengi ya mwanadamu yanatokana na kushindwa kukaa kimya peke yake ajitafakari.

Laiti angelifaulu kukaa kimya, kujipata na kujipatanisha na nafsi yake kwanza, basi matatizo mengi yangeepukika.

Kwenye ukimya unajitazama upya na unajikosoa. Kwenye ukimya unajisahihisha na kujihuisha. Kwenye ukimya unajichaji, hatimaye unajipatia nguvu na ari zaidi.

Somo la kwanza ambalo elimu ya nafsi inatufunda ni juu ya umbumbumbu au uelewa wetu hafifu juu ya mambo fulani.

Kuna faida fulani ya kutojua kila kitu hasa kipindi hiki cha lundo la taarifa ambazo ubongo hauwezi kuzichakata sawasawa.Kwanza anayejifanya mjuaji wa kila kitu ni mtu hatari. Kuwa na udadisi,unyenyekevu na kuwa muwazi kujifunza ni muhimu sana.

Maisha ya mwanadamu, tofauti na viumbe wengine, ni kuitafuta maana, na hii ndiyo mada kuu.

Uhuru wa ndani na elimu ya nafsi inakupa mtazamo na msukumo chanya kuhusu maisha, kuchochea hamasa ya kuishi licha ya changamoto zake.

Mtazamo chanya wa maisha, kwa mujibu wa mshunuzi mbobezi Viktor E. Frankl (1905-1997), unasaidia kuona changamoto za maisha kama alama ya mkato na si nukta, ndiyo maana hata giza husaidia kuona nyota.

Katika safari ya maendeleo binafsi yaani “self-development” kwa Kimombo, unatakiwa ujitafakari kwa yakini na bila kukoma.

Vuta picha uko mahali, unakutana na ‘wewe’. Je, ungempenda? Ungependa kukaa na kuishi naye? Ungependa uwezo na ndoto zake?

Kwa unavyomfahamu ‘wewe’, angefaa awe nani kwako; rafiki, mwenza, mzazi, mtoto, jirani au? Ungechukuliaje upungufu na haiba yake?

Hebu jiulize, ukiondoa elimu, ujuzi, kazi, mali, cheo na watu uliowaweka karibu, utabaki na nini kinachoweza kubeba thamani yako? Wakati mwingine watu hawakuheshimu “wewe” bali huheshimu vile vinavyoambatana na wewe kama elimu, cheo au umaarufu wako. Wewe ni zaidi ya vitu hivyo vyote, je, wewe ni nani? Desturi ya kujitafiti na kukutana na ‘mimi’ ni suala la jadi na endelevu.