Naamini Rais Samia atatibu majeraha ya Taifa

Naamini Rais Samia atatibu majeraha ya Taifa

Muktasari:

  • Vifo na michezo ni miongoni mwa matukio yanayoelezwa kuwaunganisha watu na kusahau tofauti zao kwa wakati.

Vifo na michezo ni miongoni mwa matukio yanayoelezwa kuwaunganisha watu na kusahau tofauti zao kwa wakati.

Hii ni kwa kuwa kimsingi, matukio hayo yanabebwa na thamani ya utu na mapenzi au ushabiki ambao huwaweka pamoja watu wanaohasimiana.

Katika michezo mahasimu kama ilivyo kwa timu maarufu za Simba na Yanga, wachezaji hujikuta wakichezea timu moja ya Taifa na wakishinda ushindi huwa wao wote.

Nao mashabiki hujikuta wanaungana kushangilia timu yao ya Taifa kwa wakati huo, lakini baada ya mchezo ndipo hurudi kwenye tofauti zao za upenzi wa klabu.

Lakini kwa matukio ya ugonjwa na vifo, utu au ubinadamu hutawala na hivyo kututofautisha na viumbe wengine.

Ndiyo maana akigongwa mtu barabarani akapoteza maisha, mwili wake hauwezi kuozea barabarani, husitiriwa na hata wasiokuwa ndugu zake.

Lakini mnyama akigongwa hatolewi zaidi ya mwili wake kuendelea kukanyagwa, na utabaki hapo mpaka umalizike.

Hakuna anayejali hata kuondoa mabaki ya mwili wa mnyama anapogongwa barabarani.

Ikumbukwe katika kifo watu hawasambazi kadi kama ilivyo sherehe nyingine kama harusi, ubatizo, komunio na jubilei ambazo unaweza usishiriki kwa kuwa katika maisha yako unaweza usioe wala kubatizwa.

Hata hivyo, msibani watu huenda wenyewe bila kuangalia mipaka ya mitaa, kwa kuwa ni tukio linalogusa utu wa kila mmoja, akiamini asipokufa yeye iko siku atafiwa hivyo atahitaji huruma ya watu wengine.

Utamaduni wa watu kuhasimiana mpaka kuombeana vifo, kushangilia watu kufa au kupata majanga mabaya ambayo yanahatarisha uhai wa mtu, nimeanza kuuona katika miaka ya karibuni

Hii ni kinyume kabisa na misingi iliyowekwa na wasisi wetu ambao waliamini kuwa Afrika ni moja na binadamu wote ni sawa.

Waasisi hao waliunganisha makabila zaidi ya 120 kuwa kitu kimoja na kuwa na lugha moja ya kutuunganisha, kusoma na kutibiwa sehemu moja.

Watu walilima pamoja kwa njia ya ushirika, tatizo la mwingine lilichukuliwa lao wote; hayo yameanza kupotea hivi leo, lazima kuna sehemu tulipojikwaa.

Leo watu wanaombea wenzao waugue na kufa na kutoshiriki matukio ya misiba ya watu ambao wanatofautiana kwenye mrengo fulani

Hili halipaswi kuachwa likaendelea maana litakuwa linakinzana na kauli zilizozoeleza kuwa Tanzania ni nchi ya amani, umoja, upendo na utulivu.

Thamani ya utu wetu kama Taifa inazidi kupotea. Kwa wafuatiliaji wa mitandao ya kijamii watakuwa mashuhuda kuwa kama hatutaangalia tulipojikwaa, tuendako kunaweza kuwa kubaya sana.

Kama tumefikia hatua ya kuombea watu kufa au kushangilia watu kufa, hili linadhihirisha wazi kuwa kuna ufa mkubwa ambao tusipouziba sasa tutajenga ukuta kwa gharama kubwa.

Ukifuatilia salamu za rambirambi za viongozi wa vyama vya kisiasa vya upinzani walizotoa katika kifo cha Dk John Magufuli, mguso wa kifo waliueleza kwa kifupi, lakini kilichojaza mioyo yao walikieleza kwa kirefu na kuomba kufanyike mabadiliko ya haraka ili kutibu majeraha hayo.

Jambo ambalo linaleta tumaini ni kauli ya Rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan aliyoitoa siku ya kuapa kwake kuwa Rais.

Alisema si wakati wa kuangalia nyuma kwa maana yaliyopita, bali kuangalia mbele kwa maana ya kuboresha pale palipokuwa na dosari.

Alisema ni wakati wa kushikamana na kuziacha tofauti zilizopo na kuwa wamoja, kwani ndiyo njia pekee ya nchi kusonga mbele kwa haraka

Aliongeza kuwa huu ni wakati wa kufarijiana, kuonyeshana upendo, udugu wetu na utanzania, na si kuangalia mbele kwa mashaka bali matumaini na kujiamini.

Ingawa Rais Samia alikuwa kwenye kipindi kigumu cha majonzi na kupewa majukumu mazito huku mtu aliyekuwa kiongozi wake akiwa hajazikwa, bado ametoa kauli inayolenga kurejesha umoja, udugu, upendo na mshikamano wetu kama njia ya kumuenzi mwasisi wa Taifa hili.

Naamini kupitia hotuba yake, tunatakiwa kumuamini na kumpa ushirikiano mkubwa katika kufikia ndoto hiyo ambayo inalenga kutibu majeraha ndani ya mioyo ya baadhi ya watu.

Antony Mayunga ni mwandishi wa Mwananchi. 0783104341.