Namna ya kujiandaa na kustaafu kwa raha
Kuweka akiba kwa ajili ya uzeeni ni kitu ambacho kinatatiza watu wengi. Hii ni kwa sababu watu wengi wanaona kiasi wanachopata hakitoshi kwa matumizi na pia pengine uzee ni majaliwa.
Ni vizuri kuelewa kuwa binadamu anapitia vipindi tofauti tofauti na uzee ni kipindi ambacho nguvu zimeisha, uwezo wa kufanya kazi umepungua na hivyo unatakiwa kuwa na akiba ya kuwezesha kuishi maisha uliyokuwa unaishi wakati ukiwa na nguvu. Kuweka akiba kwa ajili ya uzeeni ni jambo muhimu sana ambalo linahitaji mipango madhubuti kuanzia miaka ya mwanzo kabisa ya ujana wako. Kanuni kadhaa zitakusaidia.
Mosi. Kanuni ya 50/30/20. Hii ni mbinu muhimu sana ambayo inaweza kukusaidia kupanga matumizi yako ya fedha. Kwa mujibu wa kanuni hii, unapaswa kugawanya mapato yako katika sehemu tatu: asilimia 50 kwa mahitaji ya msingi (kama vile kodi ya nyumba, usafiri, ada, chakula, na umeme), asilimia 30 kwa matumizi ya kawaida (kama vile burudani na mavazi), na asilimia 20 kwa ajili ya kuweka akiba na kuwekeza. Kama unafanya kazi na unaona huwezi kuwa na asilimia 20 kwa ajili ya akiba na kuwekeza, jitahidi kuongeza ujuzi, ufanisi au kutafuta kazi ya ziada ili kuongeza kipato chako.
Pili. Anza kujilipa mwenyewe kwanza kabla ya kulipa kwa ajili ya wengine. Ni kweli unapopata mshahara unalipwa. Jilipe tena kwa kuweka kando fedha za akiba kabla ya kuanza kutumia. Unaweza kufanya hivi kwa kutengeneza akaunti maalum ya akiba na kufanya uhamisho wa moja kwa moja wa fedha mara tu mshahara unapoingia. Kama unafanya biashara ndogo ndogo hakikisha unajilipa mshahara kutokana na hiyo biashara.
Tatu. Weka akiba ya dharura. Jitahidi kuweka akiba inayotosha kukuhudumia kwa miezi mitatu hadi sita bila kupata mapato mengine. Hii itakusaidia kukabiliana na changamoto zozote zisizotarajiwa bila kuharibu mpango wako wa kustaafu. Kwenye hili unaweza kuweka lengo ambalo utalifuata. Mathalani ukiweka akiba ya shilingi 100,000 kila mwezi utakuwa umejiwekea Sh1.2 milioni.
Nne. Usinunue kitu chenye matumizi makubwa kabla ya kushauriana na familia yako na hakikisha unatumia kanuni ya masaa 24 kabla ya kufanya manunuzi makubwa. Hii itakusaidia kuepuka kununua vitu visivyo vya lazima kwa msukumo wa ghafla. Chukua muda kufikiri kama kweli unahitaji kitu hicho na jinsi kitakavyoathiri mpango wako wa kuweka akiba. Watu wengi wananunua kitu kwa ghafla baada ya muda mchache wanakuta kitu hichohicho kinauzwa nusu ya bei kwa muuzaji mwingine jirani. Pia jaribu kuuliza bei kwa wauzaji angalau watatu kabla ya kununua chochote.
Tano. Ni muhimu kuongeza kiwango chako cha akiba kwa kadiri kipato chako kinavyokua na kwa namna mbalimbali. Kwa mfano, unaweza kuweka fedha zozote za ziada unazopata kama akiba yako. Hizi zinaweza kuwa bonasi kutoka kazini, fedha za mirathi, au zawadi za fedha taslimu. Badala ya kutumia fedha hizi kwa matumizi ya kawaida, zingatia kuziweka kama sehemu ya akiba yako ya uzeeni.
Safari ya kuweka akiba kwa ajili ya kustaafu ni ya muda mrefu na inahitaji nidhamu. Muhimu kwenye safari hii ni kuanza na kuendelea kwa utaratibu. Kustaafu kunawapata watu wote, uwe umeajiriwa au kujiajiri kwenye biashara ndogo. Uwe umeajiriwa sekta binafsi au serikalini. Hivyo panga kujiandaa kustaafu.