Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIKWAMBIE MAMA: Viongozi wasikariri kanuni, wawe wabunifu

Rais Samia Suluhu Hassan

Katika maagizo unayowapa viongozi wetu kila siku, siwezi kuisahau ile unayowataka kuwa wabunifu. Kiongozi mbunifu huweza kutatua changamoto mpya na zile zilizokosa utatuzi hapo mwanzo. Tumeshuhudia viini vya maradhi vikijibadilisha kutoka hatua moja hadi nyingine na kuwachanganya watafiti wa tiba. Kwa mfano wakati wa janga la korona tuliona mdudu akibadilika kukwepa dawa na tafiti zilizokuwa zikiendelea, kadhalika mdudu wa ebola, M-Pox na kadhalika.

Mwalimu wangu wa sayansi alinifundisha kitu kutoka kwa mdudu amoeba. Huyu mdudu alipoingia kwenye maji ya kunywa, alisababisha yasiwe salama na mnywaji kuwa hatarini. Ikagundulika kuwa maji yakichemshwa na kuhifadhiwa vizuri mdudu hufa na maji yanarudi kuwa salama. Lakini baada ya mdudu huyu kugundua kuwa watu sasa wanachemsha maji ili afe, akawa akivaa gamba la kukinga maji yanayochemshwa yasimdhuru.

Jambo hili linanifanya kuamini kuwa maadui wote wakishaijua njia yako ya kujihami, huacha kuitumia njia hiyo na kubuni njia mpya. Wakati fulani askari wa barabarani wasio waaminifu walikuwa wakipigwa picha wakati wanapokea milungula kutoka kwa madereva wazembe. Walipogundua hilo, askari wabovu na madereva wazembe wakabuni mbinu mpya za kupeana milungula yao. Mlungula ukawekwa ndani ya gazeti ambalo dereva alimletea askari.

Mapambano ya rushwa, ukatili wa kijinsia, umasikini na changamoto nyingine yalianza zamani sana. Zikatungwa sheria za kupambana na matatizo hayo lakini hazikufua dafu. Changamoto zinazidi kuongezeka kadiri zinavyopigiwa kelele. Mfano hai ni huu wa juzi tu hapa. Baada ya kupigia kelele vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia, wahalifu wametujibu na tukio la Dodoma baada ya kuwalawiti mama na bintiye, kisha kuwaua kwa silaha. Katika hali hii hatuna budi kuwa wabunifu ili kuyakomesha majanga haya.

Kwa tafsiri nyepesi, ubunifu ni ugunduzi wa matumizi ya njia bora zaidi zinazotatua changamoto mpya, changamoto ambazo tayari zipo lakini hazijapatiwa ufumbuzi, na changamoto sugu zilizopo kwenye jamii kwa kipindi husika. Dhana hii hutimilika pale ambapo bidhaa, huduma, teknolojia, mpangilio wa biashara au njia nyingine yoyote inayoweza kutatua changamoto husika katika jamii ni adimu kuipata katika masoko ya kiuchumi, Serikali au jamii yenyewe.

Chanzo cha ubunifu ni Mungu, maana ndiye aliyeanzisha vitu vyote na kuachilia mawazo ndani ya watu. Hii inatafsiri kuwa kabla ulimwengu haujaumbwa hakukuwa na kitu chochote. Baada ya Mungu kuumba ulimwengu, ndipo tulipotayarishiwa anga, maji, hewa na vyote tulivyovikuta. Na baada ya Mungu kutupa uwezo wa kubuni ndipo tukajiongeza kwa majengo, magari, madaraja na kadhalika. Kabla havijabuniwa, vyote hivyo havikuwapo.

Ili ubunifu uweze kuonekana ni lazima wabunifu waaminiwe, wapewe kipaumbele, ikiwezekana pia wapewe mitaji na kuendeleza elimu za ubunifu wao. Wakati mwingine mbunifu hukutana na visiki vya sheria. Ataambiwa jambo lake haliwezekani kwani hakuna kifungu cha sheria kinacholisimamia. Lakini bila uthubutu wa kuwaamini wabunifu hawa, hakuna kitakachowezekana, na pengine wabunifu hao wanaweza kuonekana wanakwenda nje ya dira.

Ni ukweli watakuwa nje ya dira, lakini wanayaona ni yale ambayo hayajaonekana kwenye dira iliyopo. Haya yaliwahi kumtokea mshauri wa masuala ya sayansi kwenye uongozi wa Rais John F. Kennedy wa Marekani. Alipingwa kabla hajawasilisha maono yake ya kupeleka watu mwezini kwenye miaka ya sitini. Hata Kennedy mwenyewe alilichukua wazo hilo kama msalaba, lingefeli naye angechukuliwa kuwa chizi wa hatari kuliko yule wa Msanga.

Kwa ujasiri mkubwa Kennedy akamwamini mbunifu na akaubeba msalaba huo. Aliliomba bunge kuidhinisha bajeti ya karibu dola bilioni kumi kwa ajili ya mchakato huo. Iwapo mpango huo ungefanikiwa, Warekani wangelinda heshima ya ubaba wa dunia baada ya kuwa wameshaanza kufeli kwenye vita baridi dhidi ya Warusi. Urusi walishatuma chombo chao kwenye anga za juu kabla ya Marekani. Kennedy alipoukubali mpango huo alipingwa mpaka na watoto wa shule. Sheria ilimtaka abwage manyanga na pengine kujiuzulu, lakini akakaza na hatimaye kufanikisha azma yake Julai 20, 1969.

Nasisitiza kuwa sheria zote zimebuniwa na wanadamu kuzikabili changamoto. Ina maana kabla hazijabuniwa hakukuwepo na sheria. Tungekuta tumeshawekewa sheria zinazotusimamia, hadi leo tusingelikuwa na seria tulizonazo. Namaanisha iwapo tungejikuta tunafugwa na viumbe wengine, tungewekewa sheria zao kama sisi tunavyowawekea kuku na mbwa. Tusingeliweza kubuni sheria zetu wenyewe.

Hivyo, inawezekana kwa mbunifu kuziweka sheria pembeni wakati akiendelea na ubunifu wake. Pia, inawezekana hata kuziepuka, kwani sheria sio rungu la kuzima mawazo mapya. Wakati mwingine sheria tulizonazo kwenye vyama na hata Serikalini zinatubana kuingia kwenye wigo mpana wa kutatua matatizo yetu. Kiongozi anaogopa kubuni ili asionekane kuwa mpinzani wa mawazo ya wakubwa. Na haiwezekani kuondoa ombwe ulilo ndani yake.

Wakati huu tunapoelekea uchaguzi kutoka mtaani mpaka Serikali kuu, tutathmini viongozi wabunifu badala ya wanaokariri kanuni. Baada ya mbinu zote kushindwa kutufikisha kwenye tija, kiongozi atakayetufaa ni yule mwenye uwezo wa kubuni michakato mipya inayoweza kutuvusha. Wapo vijana mahiri na wazee wastaafu ambao wakipata nafasi za uongozi, bila shaka wataliweza hilo.