Ruzuku itolewe kuchochea matumizi ya gesi majumbani

Matumizi ya nishati safi ya kupikia majumbani nchini Oman ni somo lililoeleweka kwa raia wake ambapo asilimia 100 mjini na vijijini wanatumia huduma hiyo ambayo ni salama na gharama nafuu.
Oman ni nchi ya Kifalme yenye utajiri wa gesi na mafuta, matumizi ya nishati safi ya kupikia majumbani ni kila nyumba. Mji mkuu wa Mascat mtungi wa gesi wa kilo 15 unauzwa kwa riale 3, sawa na Sh21,000 na mtungi wa kilo 6 unauzwa kwa riale moja na nusu, sawa na Sh10,500 za Tanzania.
Tanzania inatajwa kuwa kinara barani Afrika wa kampeni ya matumizi nishati safi ya kupikia majumbani, viongozi wake wamekuwa wakinadi katika majukwaa na makongamano ya ndani na ya kimataifa.
Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa ziara yake mkoani Tanga, Februari 27, 2025 alisema Serikali itaendelea kutunga sera rafiki zitakazowezesha ushiriki wa sekta binafsi katika kuwezesha nishati safi ya kupikia kupatikana kwa gharama nafuu.
Matamanio ya wengi ni kuona bei ya gesi inapungua ili kumwezesha mwananchi kuipata nishati hiyo safi ya kupikia majumbani chini ya bei ya soko, na kuwavutia wengi na kuachana na nishati chafu ya kuni na mkaa.
Juni 21, 2024, jijini Dar es Salaam lilifanyika kongamano la uhamasishaji matumizi ya nishati safi ya kupikia majumbani na kutolewa pendekezo la ushirikishwaji wa viongozi wa dini na kimila kutoa elimu kwa wananchi.
Kongamano hilo liliandaliwa na UNCDF kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) na viongozi wa mataifa kutoa michango na malengo yao ambapo Serikali ya Tanzania iliazimia ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania watakuwa wanatumia nishati safi ya kupikia majumbani.
Kwa mnasaba wa kongamano hilo kuelekea mwaka 2034, Watanzania asilimia 80 wawe wanatumia nishati safi, ni vema Serikali kukaa na waagizaji wa gesi, lengo ni kumwezesha mwananchi kunufaika na nishati hiyo, ikiwemo kupunguza gharama ya kununua mtungi na kujaza gesi.
Imekuwa ada kuwaona viongozi kugawa mitungi ya gesi bure katika maeneo mbalimbali, yakiwemo majimboni, jambo ambalo ni la kupongezwa, lakini nionavyo, kampeni hiyo haiwezi kumtoa mwananchi kutoka katika matumizi ya nishati chafu ya kupikia bila kumuwekea mazingira mazuri na elimu.
Kwanza, ni vyema Serikali ikaondoa kodi kwa bidhaa zinazohusiana na nishati hiyo, hatua ambayo itatoa hamasa kwa Watanzania kuhamasika kuachana na nishati chafu, sambamba na kupiga marufuku ukataji miti kwa ajili ya mkaa.
Ni vema kuwepo ukomo wa matumizi ya kuni na mkaa kama ilivyokuwa kwa mifuko ya plastiki, kwani inaweza kuwa vigumu kumtoa mwananchi katika matumizi hayo ambayo si salama kiafya na pia yenye gharama kiuchumi.
Ili dhamira itimie, ni vema Serikali itoe ruzuku kwa wanaochakata gesi kuwa nishati na kuweka mazingira rafiki yatakayochochea ushiriki wa sekta binafsi kwenye shughuli hiyo itakayorahisisha asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi kabla ya mwaka 2034.
Viongozi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji pamoja na viongozi wa dini mkoa, wilaya na nyumba za ibada washirikishwe katika kampeni hii ambayo kwa upande wao wana mchango mkubwa, hasa ikiwa wako karibu na jamii.
Kada hii ikishirikishwa ipasavyo wakati Serikali inaweka mazingira mazuri kwa wananchi juu ya kumudu gharama za matumizi ya nishati safi ya kupikia majumbani, uwezekano wa kutofika mwaka huo wa 2034 Watanzania wote watakuwa tayari wanatumia nishati hiyo.
Kwa sasa mjini Tanga, kujaza gesi mtungi wa kilo 15 ni kati ya Sh55,000 hadi Sh58,000 ambapo wa kilo sita hujazwa kwa Sh23,000 hadi Sh25,000 kutegemea na kampuni.
Kama ndio unaanza kutumia, bei ya mtungi wa kilo 15 ni kati ya Sh90,000 hadi Sh100,000 na ule wa kilo 6 ni Sh45,000 hadi Sh50,000 kutegemea na kampuni inayouza gesi.
Dhamira ya dhati ya Serikali kuwatoa Watanzania katika matumizi ya nishati chafu ya kupikia inapaswa kuungwa mkono kama kongamano la Juni 21, 2024 jijini Dar es Salaam lilivyoazimia kwa kutambua kuwa matumizi ya mkaa na kuni si salama kiafya.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yanayosababishwa na moshi husababisha vifo vya watu milioni 4.3 kila mwaka ulimwenguni na kupiku ugonjwa wa malaria na kifua kikuu.
Salim Mohammed, ni mdau wa mazingira - 0655902929.