Serikali, makandarasi timizeni wajibu wenu
Sekta ya ujenzi nchini Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa, zikiwemo ucheleweshaji wa malipo na kutokamilika kwa wakati miradi ya maendeleo.
Makandarasi wazawa na wa nje ya nchi wamekuwa wakilalamika kuhusu kucheleweshewa malipo, hali inayosababisha miradi mingi kuendelea kuchelewa kukamilika.
Serikali, kwa upande wake, inalalamikia miradi inayocheleweshwa au kutotekelezwa kwa viwango vinavyokubalika, jambo linaloathiri maendeleo ya miundombinu.
Kwa sasa, Serikali inakabiliwa na shinikizo la kuhakikisha malipo ya makandarasi na wahandisi washauri yanalipwa kwa wakati.
Hali ya malimbikizo ya madeni, hasa katika miradi ya barabara imekuwa changamoto kubwa, ambapo mahitaji makubwa ya rasilimali fedha hayakidhi mahitaji halisi ya miradi hiyo.
Serikali imeweka mkakati wa kulipa madeni ya makandarasi kwa kiwango cha shilingi bilioni 70 kila mwezi, ambapo bilioni 50 zinawalenga makandarasi wazawa.
Hata hivyo, kasi ya ulipaji wa madeni bado haikidhi ukubwa wa madeni yenyewe.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu shughuli ilizozifanya kwa mwaka 2023, ilibainisha kuwa miongoni mwa changamoto zinazoikabili Tanroads ni uchelewashaji wa ulipaji wa madeni ya makandarasi na wahandisi washauri hali iliyosababisha kuongezeka kwa gharama.
Kwa mfano, taarifa ilibainisha kuwa Desemba 2023, miradi iliyokamilika ilikuwa 94 na makandarasi husika walikuwa wanaidai Serikali Sh386.36 bilioni huku miradi ya barabara inayoendelea kujengwa ikiwa 69, yenye deni la makandarasi Sh392.6 bilioni na hivyo kufanya jumla ya deni lote liwe Sh778.96 bilioni.
Tunaungana na kamati hiyo iliyoitaka Serikali ilipe madeni ya makandarasi na waandisi washauri kwa wakati ili kuondoa ongezeko la gharama zinazosabishwa na riba.
Katikati ya mjadala wa deni hilo, ndipo Serikali imekuja na onyo kwa makampuni ambayo hayatekelezi majukumu yao kwa viwango vinavyotarajiwa, hasa kampuni zinazotelekeza miradi.
Pamoja na umuhimu wa onyo hili, sisi tunalitazama hili kama suala la wajibu wa kila upande – Serikali kulipa malimbikizo na kuwawezesha makandarasi kukamilisha miradi, na wale waliokwishalipwa kukamilisha miradi husika.
Pamoja na juhudi hizi, bado kuna changamoto zinazosababishwa na matumizi mabaya ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi na hivyo kufanya kazi chini ya kiwango.
Hapa wanatajwa makandarasi wazawa, kuwa licha ya kupewa fursa kubwa na Serikali, mara nyingi wanashindwa kutumia ipasavyo fedha zilizotengwa kwa miradi ya ujenzi, na badala yake wanazitumia kwa matumizi binafsi na kuchelewesha miradi.
Suala hili linaweza kuchangiwa na kutokuwepo kwa taratibu madhubuti za ufuatiliaji na udhibiti wa fedha za miradi kunakofanya iwe vigumu kuhakikisha fedha zinaelekezwa katika matumizi yaliyokusudiwa.
Ili kutatua tatizo hili, kuna haja ya Serikali kuweka mifumo madhubuti ya usimamizi wa malipo ambayo itahakikisha kuwa makandarasi wanapokea fedha kwa wakati kulingana na mikataba waliyoisaini.
Serikali inapaswa pia kuhakikisha wahandisi na wataalamu wa ukaguzi wa miradi wanahusishwa kikamilifu ili kubaini changamoto zilizopo na kutatua matatizo kwa haraka.
Hii itasaidia kuondoa malimbikizo ya madeni na kuzuia ucheleweshaji wa miradi kwa wakati mmoja, pia itaondoa suala la kipa upande kuulalamikia mwingine.
Kwa upande wa makandarasi, ni muhimu kuchukua hatua thabiti za kuboresha usimamizi wa rasilimali fedha na kuhakikisha zinaelekezwa katika maeneo muhimu ya miradi.
Pia, makandarasi wanapaswa kufuata taratibu na mikataba ya malipo kwa uadilifu na kufanya kazi kwa welezi na viwango ili kuepuka kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya kuilipua.