Shida matumizi ya nishati safi, ni gharama

Muktasari:

Makala haya yanashauri Serikali kuweka mazingira rafiki na rahisi ili kuvutia Watanzania wengi kutumia nishati safi.

Dar es Salaam. Nazitazama jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan,  akitaka Watanzania kugeukia matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kama kiongozi wa nchi mara kadhaa amenukuliwa akihanikiza wananchi kuacha kutumia mkaa na kuni.

Hata msimamo wa Serikali yake unaonyesha dhamira ya dhati ya kutaka kuona mkaa na kuni vinakuwa historia.

Serikali yake  imeshatamka rasmi kuwa kwenye maeneo ya watu wengi kuanzia 100 na kuendelea kama vile magerezani, kambini na kwenye taasisi za elimu, wahusika lazima watumie nishati mbadala.Ni kwa  namna gani hilo linatekelezwa, ni mada ya kujadili siku nyingine.

Majuzi hapa Rais Samia alikuwa nchini Ufaransa akihudhuria mkutano wa kimataifa kuhusu nishati safi. Katika mkutano huo Samia alikuwa mwenyekiti mwenza.

Nakumbuka miongoni mwa aliyosema ni pamoja na kutaja changamoto tatu zinazozuia wakazi wa barani  Afrika kutotumia nishati safi ya kupikia.

Changamoto hizo ni pamoja na gharama kubwa ya vyanzo vya nishati safi ikiwamo nishati ya gesi, umeme na nyinginezo.

Kwa Tanzania sio siri kuwa nishati safi hasa gesi bado ni kibarua kigumu. Watanzaniaa  wengi wanaendelea kutumia mkaa na kuni,  nishati inayoelezwa kuwa na madhara kwa afya na mazingira kwa jumla.

Majanga tunayoyashuhudia sasa ya yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi, ni kwa sababu binadamu tumeshitadi pamoja na mambo mengineyo kukata miti kwa ajili ya mkaa, kuni au mbao.

Hata hivyo, kilichopo kwa Watanzania sio kama wanaamini  kuwa mkaa  na kuni ndio nishati pekee.

Watanzania ni wasikivu na wana utayari wa kubadilika wakijengewa mazingra ya kufanya ‘muhamo wa ruwaza’.

Hawaoni tatizo kuingia kwenye zama mpya za matumizi ya nishati safi kama inavyopigiwa chapuo na Serikali na wadau watetezi wengine wa mazingira.

Tatizo  linalowarudisha nyuma ni gharama ya kumudu nishat hizo. Kwa mfano, nishati kama  gesi asilia, bei yake haishikiki kulinganisha na mkaa au kuni.

Hata matumizi ya umeme, sio tu haujawafikia Watanzania wote kila kona ya nchi, lakini bei yake nayo ni kikwazo.

Upande wa gesi, leo kama huna Sh22,000 na kuendelea hupati ule mtungi wa chini kabisa wa kilo sita.

Ninavyo wawekezaji  katika nishati hiyo, wanaitumia hiyo kama fursa ya kuvuna, kumbe wanawakimbiza Watanzania.

Sielewi  sababu ya gesi kuwa kubwa ilhali tunaelezwa nchi ina utajiri mwingi wa nishati hiyo.

kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA),  tangu nchi ianze  uzalishaji wa gesi  Julai 2004 hadi Januari 2024, kiasi kilichotumika ni futi za ujazo bilioni 700 kati ya trilioni 57 zilizogundulika.

Hicho ni kiwango cha gesi kilichogundulika, achana na ambacho bado hakijagundulika ambacho naamini maeneo mengi ya nchi yetu yana utajiri huo.

Ajabu ni kuwa katikati ya utajiri huu, bei ya gesi haijawa nafuu. Si kwa gesi ya majumbani, lakini hata inayotumika kwenye magari kama mbadala wa mafuta.

Kwa wingi wa gesi pengine kiasi kilichopaswa kutozwa kwa wenye magari kwa kila kilo moja ya gesi, kingekuwa chini ya Sh1000. Hapo tungeona namna Watanzania wanavyochangamkia nishati hiyo na kuachana na mafuta ambayo ni pasua kichwa.

Nimezungumzia bei ya kujaziwa gesi, sijataja mamilioni anayotakiwa kuwa nayo mtu akitakaa kuwekewa mfumo wa gesi!


Ukitazama kwa undani hizi ni gharama kubwa ndio maana ni watu wachache wanaojitokeza kutumia gesi kwenye magari yao.

Niliwahi kusoma tangazo la kampuni moja ikitangaza kuweka mfumo wa gesi kwenye bajaji. Niliachwa mdomo wazi kuona hata bajaji kuwekewa mfumo, mhusika anatakiwa awe na sio chini ya Sh1milioni!Serikali isipoamka na kuweka mazingira rafiki  na nafuu kwa wawekezaji na wafanyabiashara wa nishati safi,  Watanzania wataendelea kutumia nishati hatarishi walizozioea kwa miaka nenda rudi.

Nimezungumzi gesi kwa kirefu kwa kuwa ndio aina ya nishati safi ambayo kwa sasa inaonekana kuja juu. Natambua kuwapo kwa  aina anuai za nishati safi.

Hata hivyo, kama ilivyo kwa gesi,  hata  nishati hizi nazo hazihitaji lelemama; wananchi wanapaswa kujifunga kibwebw kumudu gharama zake. 


Dawa ni moja tu, gharama zipunguzwe.  Tukifanya hivyo, wengi watakimbilia kwenye nishati safi. Vinginevyo tusahau matumizi ya nishati hiyo.

Tutabaki kusema Watanzania hawataki kubadilika, tatizo sio mtazamo hasi bali wanakimbizwa na  gharama kubwa ya matumizi ya nishati safi.

Abeid Poyo ni mwandishi wa Mwananchi