SIMANZI YA KUACHIKA YAWEZA KUKUPA UGONJWA WA MOYO

Muktasari:

Broken heart syndrome au Takostubo ni tatizo la moyo linalosababishwa na mtu kupata simanzi au huzuni kali baada ya kutengana au kuachika na mwenza au mpenzi.

Broken heart syndrome au Takostubo ni tatizo la moyo linalosababishwa na mtu kupata simanzi au huzuni kali baada ya kutengana au kuachika na mwenza au mpenzi.

Tatizo hili linalosababishwa na kudhoofika ghafla kwa misuli ya moyo kwa kipindi kifupi huitwa Takastubo kutokana na mgunduzi wa ugonjwa huu ambaye ni Mjapani.

Wataalamu wa magonjwa ya moyo wanalitofautisha tatizo hili na yale ya kukosekana kwa damu ya kutosha katika misuli ya moyo.

Takostubo inajitokeza zaidi pale watu wa karibu au wenza ambao wana mgusa moja kwa moja muathirika wanapofariki ghafla, wanaachwa na kuwa na hofu au wasiwasi kwa muda mrefu.

Jumuia ya wataalamu wa moyo duniani wanakubaliana kuwa tatizo hili huweza kusababisha kushindwa kufanya kazi kwa moyo ghafla na kudunda bila mpangilio.

Huwa na dalili mbalimbali ikiwamo maumivu makali ya kifua, uchovu, kuweweseka kupumua au kuhema kwa taabu na kuhisi kizunguzungu.

Tatizo hili huweza kuonekana zaidi pale mtu anapopokea taarifa ya kufiwa, kuibiwa mali au pesa zenye thamani kubwa, kugundulika ana magonjwa sugu kama vile Ukimwi na saratani, kutakiwa kuongea katika hadhara na kushtukizwa jambo.

Vilevile watu wenye hatari ya kupata tatizo hili ni kama wale wenye magonjwa kama pumu, maambukizi hatari, kupata ajali mbaya au kufanyiwa upasuaji mkubwa mwilini.

Vipimo vya msingi ambavyo ni muhimu kufanyika haraka ni pamoja na kipimo cha kuchunguza mwenendo wa moyo ECG, picha ya xray ya kifua, kipimo cha Echocardiogram, picha ya MRI, kipimo cha CAG.

Vipimo vingine ni pamoja kutazama taswira nzima ya damu na chembe chembe zake, kipimo cha kuangalia vimeng’enya vya moyo na vingine kubaini magonjwa sugu ikiwamo VVU.

Vipimo hivi ni muhimu ili kumwezesha daktari kutofautisha ugonjwa huu na shambulizi la moyo (heart attack)

Hakuna tiba ya madawa iliyo maalumu kwa ajili ya kutibu tatizo hili pekee. Matibabu yake yanaweza kufanana na ya shambulio la moyo, na mgonjwa anaweza kuhitaji kulazwa hospitali kwa muda tu.

Daktari akishathibitisha kuwa chanzo cha dalili ni broken heart syndrome na wala si shambulio la moyo anaweza kukupatia dawa kama vile zilizo katika makundi mawili.

Dawa hizo husaidia kupunguza mzigo katika moyo na pia kuzuia usipate shambulio jipya. Kwa kawaida wagonjwa wengi hupata nafuu baada ya muda wa mwezi mmoja au miwili.

Kuna uwezekano mkubwa sana wa hali hii kujirudia tena mara baada ya shambulio la kwanza.

Mpaka sasa hakuna dawa zilizothibitishwa zinazoweza kusaidia kuzuia hali hii isijitokeze tena, ingawa baadhi ya madaktari wanashauri matumizi ya muda mrefu ya dawa za kundi la beta blockers au dawa zenye kuzuia uzalishaji wa homoni zenye kuchochea shinikizo katika moyo.

Pamoja na matumizi ya dawa, ushauri nasaha pamoja na kubadili mfumo wa maisha ni mambo ya muhimu kusaidia kukukinga na tatizo hili.

Vilevile tatizo hili huweza kupelekea moyo kushindwa kufanya kazi ghafla, kupiga kwa kasi isiyo ya kawaida.

Imeandikwa na DK Shitta