Simba isibweteke na matokeo ya Kaizer

Muktasari:

  • Baada ya Jumamosi iliyopita kumalizana na watani zao Yanga, Jumamosi ijayo Simba itakuwa na kibarua kingine cha kuanza kusaka tiketi ya kucheza nusu fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika.

Baada ya Jumamosi iliyopita kumalizana na watani zao Yanga, Jumamosi ijayo Simba itakuwa na kibarua kingine cha kuanza kusaka tiketi ya kucheza nusu fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika.

Wawakilishi hao Watanzania wataanzia ugenini kwenye uwanja wa FNB au Soccer City huko Johannesburg, kuwakabiri wenyeji, Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini katika mchezo wa kwanza wa robo fainali.

Wiki moja baadae timu hizo zitarudiana jijini Dar es Salaam kwenye uwanja wa Mkapa, kama Simba itashinda mechi zote mbili, itafuzu kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa, rekodi ambayo mashabiki wa Simba wanaisubiri kwa shauku.

Simba itaikabili Kaizer Chiefs ambayo inapambana kwenye Ligi ya kwao ambako haina mwenendo mzuri.

Rekodi zinaonyesha katika mechi tano za hivi karibuni kwenye ligi yao, Kaizer Chiefs imefungwa mara tatu, imetoka sare mara moja na kushinda mchezo mmoja.

Katika mechi hizo, Kaizer Chiefs imefungwa mabao 2-1 na Cape Town na kipigo kama hicho dhidi ya TTM na bao 1-0 dhidi ya Chippa United.

Imetoka sare ya mabao 2-2 na Bloemfontein Celtic na kuichapa Mamelodi Sundowns mabao 2-1.

Ukiiangalia Kaizer Chiefs kwenye mechi hizo, imefunga mabao sita na kufungwa mabao manane.

Kabla ya kuikabiri Simba, Kaizer Chiefs itavaana na Swallows kwenye ligi yao, ingawa Simba pia itacheza mechi kadhaa za Ligi baada ya ile ya Jumamosi iliyopita na watani zao Yanga.

Japo Simba itacheza robo fainali ya Ligi ya mabingwa ikiwa na rekodi nzuri kwenye mechi zake tano za karibuni za Ligi, bado haitoshi timu hiyo kujiaminisha kwamba tayari imefuzu nusu fainali.

Ni dhahiri kwamba kabla ya mechi iliyopita na Yanga, Simba ilikuwa imeshinda mechi zote tano zilizopita za Ligi.

Iliichapa 5-0 Mtibwa, 1-0 dhidi ya Mwadui, 2-0 dhidi ya Kagera Sugar, bao 1-0 na Gwambina na mabao 3-1 na Dodoma Jiji, kabla ya mechi ya juzi na Yanga.

Katika mechi hizo imefunga mabao 12 na kufungwa bao moja pekee, lakini hiyo isiwe kigezo cha Simba kuichukulia poa Kaizer Chiefs na kuamini tayari wameshashinda kabla hata ya mechi.

Matokeo yasiyoridhisha ya timu hiyo haimaanishi yatajirudia kwenye mashindano ya kimataifa.

Simba ijiandae kikamilifu kuikabili Kaizer Chiefs ugenini na nyumbani, imani ya kwamba Kaizer Chiefs sasa ni mbovu kutokana na kipindi wanachopitia kwenye ligi yao hivi karibuni waiondoe.


Hayo ni mashindano ya kimataifa, lolote linaweza kutokea, kama hawatajipanga na kuichukulia Kaizer Chiefs kuwa ni timu bora, wakidanganywa na matokeo ya karibuni ya timu hiyo, wasijejikutana wanapata matokeo ya kushangaza na kushindwa kutimiza ndoto zao msimu huu.

Mechi ya Mei Mei 15 ni ya kimataifa, narudia tena, lolote linaweza kutokea, tunafahamu Simba inapiga hesabu ya kucheza nusu fainali, vivyo hivyo Kaizer Chiefs pia wanapiga hesabu hiyo.

Hivyo ni jukumu la wachezaji, benchi la ufundi na kila Mwanasimba kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake katika mchezo huo wa kimataifa, wasibweteke na kipindi wanachopitia Kaizer Chiefs sasa.

Kama ambavyo kocha Didier Gomes alisema awali, kuwa atatumia mechi dhidi ya Kagera Sugar na Yanga (zilizopita) kuwa ni maandalizi ya kuangalia namna ya jinsi gani ya kuifunga miamba hiyo ya Afrika Kusini, bila shaka aliona kuna kitu cha kuongeza.

Bila shaka itakuwa imepata kipimo kizuri kwa ajili ya kuhakikisha kuwa inaisaka nusu fainali ya mashindano hayo kwa mara nyingine ikiwa na kiwango cha juu cha uchezaji msimu huu.

Hilo linabaki kwa wachezaji, benchi la ufundi na uongozi kuangalia umuhimu wa mchezo ujao bila kuangalia wapinzani wao wanapata matokeo gani katika ligi yao, kwani wanacheza na timu ambazo kila msimu inacheza nazo.

Lakini kucheza na timu ambayo inatoka katika nchi nyingine na hakuna mechi zilizowahi kuwakutanisha, hilo linaweza kuleta utofauti mkubwa katika uchezaji wa timu hizo.

Kwa mtazamo wa kile ambacho kimetokea kwa Simba msimu huu, ni wazi kuwa wana nafasi kubwa ya kucheza kwa ubora mbele ya Kaizer Chiefs, ambayo imetajwa kuwa na kiwango kisichoridhisha katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Kama nilivyotanguliza kusema, kunahitajika kuwa na mazoezi na maandalizi ya msingi bila kujali matokeo ya sasa ya wapinzani wao katika ligi ya kwao.

Ni maandalizi pekee kama waliyofanya awali yatakayowasaidia.