Simba mnaweza kucheza nusu fainali

Muktasari:

Mabingwa wa soka nchini, Simba wamewasili nchini juzi jioni baada ya kutoka katika mchezo wao wa mwisho wa Kundi A wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, uliofanyika nchini Misri.

Mabingwa wa soka nchini, Simba wamewasili nchini juzi jioni baada ya kutoka katika mchezo wao wa mwisho wa Kundi A wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, uliofanyika nchini Misri.

Simba imepoteza mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kwa kipigo cha bao 1-0 ikiwa ugenini, lakini imefuzu kwa kuwa kinara wa kundi lake na kwenda hatua ya robo fainali ya mashindano hayo makubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Matokeo yake ya msimu huu yameshitua timu nyingi kongwe za Afrika, huku makocha na wachambuzi wa soka wakiitabiria makubwa katika mashindano hayo kwa msimu huu.

Hilo limetokana na mipango na dhamira ya dhati ya kutaka kuwa bora katika soka. Pia mipango waliyonayo katika michezo ya kimataifa ilionekana tangu mapema kwamba, wanahitaji kufanya makubwa.

Tangu ilipoibuka na ushindi wa bao 1-0 nchini DR Congo ilipocheza ugenini na wenyeji wao AS Vita Club, mchezo ambao misimu miwili iliyopita ungeweza kusikia habari ya kichapo cha mabao mengi.

Al Ahly nayo ikatulizwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa bao 1-0, jambo ambalo lilimshitua kocha Pitso Mosimane wa miamba hiyo ya soka Afrika, ambao walitoka kupata sare na Al Merrikh.

Sare dhidi ya Al Merrikh ugenini ni kama iliwaongezea hasira Simba, ambao walitulia na kushinda katika mchezo wa nyumbani dhidi ya miamba hiyo ya Sudan, kabla ya ushindi mwingine muhimu dhidi ya AS Vita Club kwenye ardhi ya nyumbani.

Matokeo hayo yote kwa ujumla yalionyesha ni jinsi gani miamba hiyo ya soka nchini ilidhamiria kufanya makubwa msimu huu katika mashindano ya kimataifa kwa kujipanga zaidi.

Na sasa, Simba inajiandaa kukutana na timu iliyoshika nafasi ya pili katika makundi mengine matatu ya mashindano hayo msimu huu, jambo ambalo linaweza kuwa faidi zaidi kwa timu hiyo.

Imefanikiwa kupenya mbele ya vigogo AS Vita Club na Al Ahly ambao ndiyo mabingwa watetezi wa mashindano hayo msimu huu, ni wazi kuwa Simba haina cha kuogopa katika hatua inayofuaya.

Inaweza kukutana na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini , au MC Alger ya Algeria katika hatua inayofuata, timu ambazo zimeshika nafasi ya pili katika timu zao.

Pia, CR Belouizdad ya Algeria nayo ilipata nafasi ya pili katika kundi lake, hivyo kuwa katika hatari ya kukutana na mabingwa wa soka nchini.

Kwa aina ya timu zilizopita katika makundi hayo, ni wazi kuwa Simba ina kila sababu ya kucheza hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo msimu huu, kama itachanga karata zake vizuri.

Simba, ambayo itaanzia ugenini katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kati ya Mei 14 na 15, inaweza kutafuta ushindi ama sare ugenini mbele ya timu hizo na kumaliza kazi nyumbani.

Kwa rekodi iliyonayo Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, tunaamini kuwa hilo hata wapinzani wao watakuwa wanajua kuwa wanakutana na timu isiyofungika katika ardhi ya Tanzania.

Tunaamini kuwa uongozi na benchi la ufundi la Simba lina kila sababu ya kujipanga upya huku wakiendelea kujipongeza kwa hatua ambayo timu imefika.

Mipango yao ya msimu imekamilika, wana viporo katika ligi ya nyumbani, ambavyo wakituliza akili pia bado wana kila sababu ya kutwaa tena ubingwa wa Ligi Kuu.

Kinachotakiwa kwao sasa ni kutuliza aili na kuamini kuwa kila kiti kinawezekana katika mashindano ya kimataifa.