Simba, Yanga tuonyesheni ukubwa wenu

Simba, Yanga tuonyesheni ukubwa wenu

Muktasari:

  • Mtanange wa mahasimu wa Ligi Kuu Tanzania bara, mahasimu wa jiji moja ya Dar es Salaam – Simba na Yanga unatarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Jumamosi hii.

Mtanange wa mahasimu wa Ligi Kuu Tanzania bara, mahasimu wa jiji moja ya Dar es Salaam – Simba na Yanga unatarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Jumamosi hii.

Ni mchezo mkubwa kwa soka la Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla, kwani upinzani wa timu hizi umekuwa maarufu kwa sasa katika nchi nyingi za Afrika.

Ni takribani mchezo mkubwa wa nne katika michezo mikubwa inayotambulika Afrika, ikitanguliwa na michezo mikubwa kama ule wa Afrika Kusini kati ya Orlando Pirates na Mamelodi Sundowns, wakati pia Misri kukiwa na Al Ahly na Zamalek, Kenya pia kuna FC Leopard na Go Mahia.

Ndivyo ilivyo kwa Simba na Yanga hapa nchini, mchezo ambao unapewa heshima kubwa kuanzia kwa mashabiki, viongozi wa timu, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wadau wengine kutokana na ukubwa wake.

Mara nyingi mchezo huu umekuwa na mihemko ya wiki nzima kabla, zamani watu wakiingia katika Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) kuanzia saa 4 asubuhi kwa ajili ya kusubiri mchezo, ambao utachezwa saa 10 jioni.

Hii yote ni kutokana na ukubwa wa mchezo wenyewe na shauku ya kuwaona mahasimu hao, ambao wanaongoza kwa kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara mara nyingi zaidi kuliko timu nyingine.

Lakini mara nyingi kuelekea katika mchezo huu, kuna mambo mengi huibuka na makocha au wachezaji wameshawahi kuwa waathirika wakubwa wa mechi za aina hii.

Makocha wameshawahi kufukuzwa kwa mechi moja pekee ya Simba na Yanga, lakini pia wachezaji wengi wa vikosi hiki mara nyingi wamekuwa wakiingia lawamani pale wanapokuwa na siku mbaya kazini.

Ni suala ambalo ukilitazama kwa haraka unaweza kugundua kuwa ni ile hasira ya kufungwa, lakini maisha ya uaminifu kwa mchezaji husika yanaweza kuishia hapo na kukosa hata mechi nyingine kwa kosa moja.

Ukiachana na matatizo hayo kwa makocha na wachezaji, katika miaka ya hivi karibuni, mchezo wa watani umekosa ubunifu na utamu kama ambavyo utaangalia mchezo kati ya Ruvu Shooting na Yanga, au JKT Tanzania na Simba, lakini unaweza kuona kuwa mchezo kati ya Kagera Sugar na Azam FC ukawa mzuri zaidi ya Simba na Yanga.

Hili limeshatokea mara nyingi na linasababishwa na akili kuelekezwa katika mchezo mmoja kati ya michezo 33 ya Ligi Kuu msimu huu kwa kila timu.

Mechi ya Simba na Yanga zimekosa kuwa na ubunifu kutokana na timu zote kuangalia matokeo zaidi, na kuna wengine pia wanakwenda uwanjani na matokeo yao kwa kuangalia ubora wa kikosi.

Na mambo yanapoanza kuwa magumu ndani ya dakika 45 za kwanza, hapo ndipo balaa zaidi linapokuja kwa wachezaji kushindwa kuendana na mipango ama maelekezo ya kocha na kuwazia zaidi bao badala ya njia sahihi na bora katika kufunga.

Tunaamini kuwa wachezaji na mabenchi ya ufundi ya timu zote yamekaa na wachezaji vizuri na kuwafanya kuuona mchezo huu kama michezo mingine ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo wameshaicheza.

Wakilisimamia hilo, mchezo wa Simba na Yanga utarudi katika hadhi yake, badala ya kuwaza tu matokeo, ambayo bila shaka ndiyo kiu ya kila timu katika kusaka ubingwa, lakini ushindi unapatikana kwa njia sahihi na bora uwanjani.

Tunaamini kuwa mchezo utakuwa kama mingine ya Ligi Kuu iliyopita kwa timu zote kuonyesha ukubwa wao kwa soka safi badala ya lawama kwa waamuzi na wasimamizi wa mchezo husika.