Taasisi za dini zifuate sheria ufungishaji ndoa
Ndoa ni moja ya taasisi muhimu inayojenga misingi ya familia na jamii kwa jumla. Licha ya kuwa na umuhimu wa kiimani, ndoa pia ina muktadha wa kisheria unaopaswa kuheshimiwa na kudumishwa.
Katika hilo, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) una jukumu la kuhakikisha ndoa zinazofungwa zinafuata taratibu zinazohitajika ili zitambulike kisheria
Kwa mujibu wa Rita, cheti cha ndoa cha dini hakiwezi kutoa uhalali wa kisheria kwa wanandoa kama hazijafuata taratibu, ikiwamo kusajiliwa na wakala huo ili kupata cheti cha ndoa cha Serikali.
Upo ushahidi wa kutosha kuwa kutosajiliwa kwa ndoa kumekuwa kukiwakwamisha baadhi ya wanandoa pale wanapohitaji hati zinazotambulika kisheria. Hawa ni wake ambao wamefungishwa ndoa na viongozi wa dini ambao hawana leseni za Rita. Hii inaonyesha umuhimu wa wanandoa kuhakikisha kuwa kiongozi anayefungisha ndoa ana leseni na kibali cha Rita.
Ndoa inayofungwa na kiongozi wa dini ambaye hana leseni ya kufungisha ndoa inakuwa batili kisheria na cheti kinachotolewa kwa misingi hiyo hakiwezi kutumika kama uthibitisho wa ndoa halali katika masuala ya kisheria kama vile urithi, haki za mali, uhamisho na stahiki nyingine zinazotokana na ndoa.
Kwa mujibu wa Rita, ni lazima kiongozi wa dini anayefungisha ndoa awe na leseni ya kisheria kutoka serikalini. Leseni hii haipatikani katika taasisi husika za dini, bali ni kwa mtu mmoja mmoja, mfano mchungaji, sheikh au kadhi. Wote hao lazima wawe na kibali hicho ili kuepuka misukosuko ya kisheria kwa wanandoa siku zijazo.
Kadhalika, wanandoa wanapaswa kushirikiana na viongozi wa dini kuhakikisha kuwa ndoa zao zinajumuisha uhalali wa kisheria.
Ndoa ikisajiliwa na Rita inahakikisha wanandoa wanapata kinga ya kisheria na haki zao zinatambuliwa.
Hili linasisitizwa na Sheikh Ramadhani Kitogo, kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, kuwa kwa mujibu wa dini ya Kiislamu, walii wa binti anaweza kufungisha ndoa kwa misingi ya dini, lakini anatakiwa kufuata taratibu za kisheria kwa kusajili ndoa hiyo Rita. Hatua hii ni muhimu ili kuhakikisha ndoa za Kiislamu zinatambulika kisheria, ingawa watu wengi wamekuwa wakipuuza hatua hiyo.
Vilevile, Askofu Msaidizi mstaafu wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini, naye anasisitiza jambo hilo, kuwa kiongozi wa Kikristo lazima awe na leseni ya Rita ili ndoa anayofungisha iwe na uhalali wa kisheria. Anasema kama hana leseni, ndoa hiyo itakuwa batili na haitatambulika kisheria. Hii inaonyesha kuwa viongozi wa dini wanapaswa kuzingatia taratibu za kisheria ili kulinda haki za wanandoa na kuzuia matatizo yoyote ya kisheria yanayoweza kujitokeza baadaye.
Kwa ujumla, taasisi za dini zinapaswa kuhakikisha zinatoa elimu kwa waumini wao kuhusu umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria katika ufungaji wa ndoa.
Hili litasaidia kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza baadaye na kuhakikisha ndoa zinakuwa na heshima, haki na utulivu ndani ya jamii.
Wanandoa pia wana jukumu la kuhakikisha ndoa zao zinatambulika kisheria ili kulinda haki na masilahi yao katika nyanja mbalimbali za maisha.