Tahadhari mvua za El-Nino ifanyiwe kazi

Julai 19 mwaka huu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa tahadhari ya mvua za El-Nino msimu wa vuli kati ya Oktoba na Desemba huku ikitaja mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara na Tanga kuathirika.

Katika tahadhari hiyo mvua hizo zitakazonyesha hadi mwanzoni mwa Januari 2024, wanaoishi mabondeni wameshauriwa kuhama makazi yao.
Mara nyingi baadhi ya watu hasa wanaoishi mabondeni hupuuza tahadhari na yanapokuja maafa huilaumu Serikali kwa kuchelewa kuwapa msaada.
Kumbukumbu za mvua za El-Nino ilikuwa mwaka 1998 watu kadhaa walipoteza maisha na wengine waliachwa bila makazi.
Tanga ni moja kati ya mikoa iliyoathirika wa mvua za El-Nino za mwaka huo katika maeneo la Sahare, Donge na Magaoni, nyumba zilisombwa na maji na mifugo kufa.
Licha ya jitihada kubwa iliyofanywa na Serikali kwa kuchimba mifereji mikubwa ya kupitisha maji na miundombinu mengine, lakini iko haja ya watu kuchukua tahadhari hasa wale ambao wako mabondeni na maeneo hatarishi nyakati za mvua.
Tumekuwa tukishuhudia katika baadhi ya maeneo mvua za wastani tu, lakini watu wamekuwa na taharuki kwa nyumba zao kutuama maji kutokana na mvua hizo.
Kisiwa cha Unguja eneo la Ziwa Maboga na Mwanakwerekwe ni maeneo ya waathirika wa mvua za El- Nino mwaka 1998 licha ya jitihada zilizofanywa na Serikali kwa kuchimba mifereji na maji kupata uelekeo kwenda baharini, lakini upo umuhimu kwa watu wanaoishi maeneo hayo kuchukua tahadhari mapema.
Eneo la Ziwa Maboga ambalo liko Wilaya ya Mjini Magharibi (B) bado changamoto zipo kwa kuwa imekuwa ikishuhudiwa mvua za kawaida zinaponyesha maji hujaa na kutishia kuingia katika makazi ya watu.
Vile kwa Dar es Salaam watu wanaoishi Mto Msimbazi na Kigogo, wanapaswa kuchukua tahadhari mapema za ujio wa mvua hizo kama utabiri wa TMA, unavyoeleza.
Kama nilivyosema mikoa iliyotajwa na TMA za uwepo wa mvua hizo ni vyema wenye mamlaka katika mikoa hiyo kuchukua tahadhari mapema ikiwamo kuwaondoa wote wanaoishi maeneo hatarishi, busara ikishindikana, watolewe kwa kulazimishwa kuepusha maafa.
Tahadhari hii pia iwe kwa mikoa ambayo haikutajwa kuathiriwa na mvua hizo zinazotarajiwa kunyesha kwa kuwa tumekuwa tukishuhudia baadhi ya maeneo mvua za kawaida zimekuwa zikileta taharuki na hofu huku maji yakituama katika maeneo yao ya kuingia ndani ya nyumba.
Kwa tahadhari hiyo ya wataalamu wa hali ya hewa, iwe ukumbusho katika mitaa ambayo haina mifereji kwa kuwa, nyakati za mvua maji yanakosa njia.
Ni vyema mifereji ichimbwe mapema kuwezesha maji kuwa na uelekeo si ujio wa mvua za El-Nino tu, bali hata nyakati za misimu ya kawaida za mvua.
Tanga yapo maeneo ikiwamo Usagara Makaburini, nyakati za mvua maji hutuama na barabara kufunikwa.
Hali hiyo husababisha njia kufungwa kwa siku kadhaa na hii ni kutokana na kukosa mfereji wa uchepushaji maji kwenda baharini na maeneo mengine ya kutega maji ya mvua kwa matumizi mbalimbali yakiwamo ya kilimo cha umwagiliaji na unyweshaji maji mifugo.
Eneo hili la Barabara ya Usagara Makaburini mwaka 2017 wakati mvua inanyesha usiku, mtu mmoja alisombwa na maji wakati akiendesha gari.
Mamlaka na halmashauri za majiji na miji ni vyema kipindi hiki cha kuelekea mvua hizo za El-Nino kama watabiri wa hali ya hewa wanavyosema wajiandae kutoa elimu ya mvua hizo na madhara yake kama kuzuka magonjwa ya milipuko. Kumbukumbu zinaonyesha kuwa wakati wa mvua za El-Nino mwaka 1998 miundombinu mingi iliharibika zikiwamo barabara na madaraja kusombwa na maji, hivyo sasa ni muda muafaka wa utoaji wa elimu kwa jamii kwa kuzishirikisha asasi za kiraia.
Mashirika haya yakishirikishwa yanaweza kufikisha elimu kwa jamii juu ya kujikinga na majanga wakati wa mvua yakiwamo magonjwa ya milipuko.
Ujio wa mvua hizi uwazindue Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) kwa kuyakarabati madaraja.
Na yale ambayo yako katika ujenzi yakamilishwe mapema ili kuepuka kusombwa na maji wakati wa mvua hizo zinazotajwa kuwa za muda mrefu kwa baadhi ya maeneo.
Ni muhimu kufanyike ukaguzi mapema wa miundombinu ya barabara za lami na za vumbi mjini na vijijini zikiwamo zenye milima na kona kama za Lushoto, Bumbuli, milima ya Bungu wilayani Korogwe, Amani wilayani Muheza na nyinginezo za Tanga.
Katika milima hii nyakati za mvua kubwa magari hukwama na ndio maeneo muhimu ya utoaji wa vyakula, mbogamboga na matunda kwenda mjini.
Hivyo wenye mamlaka wazikagua mapema ikiwamo kuweka vifusi na mawe ili kuweza zipitike nyakati za mvua.