Tamko la Rais Samia fursa mpya kuvutia uwekezaji nchini

Tamko la Rais Samia fursa mpya kuvutia uwekezaji nchini

Muktasari:

  • Kila enzi na kitabu chake, nadhani hii ndiyo lugha nyepesi unayoweza kusema kwa sasa katika Taifa la Tanzania.

Kila enzi na kitabu chake, nadhani hii ndiyo lugha nyepesi unayoweza kusema kwa sasa katika Taifa la Tanzania.

Baada ya kifo cha Rais wa tano wa Tanzania, John Magufuli na baadaye kupatikana Rais mpya kwa mujibu wa Katiba, Rais Samia Suluhu Hassan, baadhi ya mambo sasa yameanza kupata suluhu.

Hakika kuna mambo yalikuwa hayawezi kujadiliwa kwa upana wake siku za nyuma, lakini sasa yanajadiliwa tena kwa kuanzishwa na Rais mwenyewe kwa maono yake.

Kauli ya Rais Samia wakati akiapisha mawaziri hivi karibuni kuwa mwenendo unaoendelea wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni kuua walipa kodi na wafanyabashara kutokana kutumika nguvu zaidi kuliko akili na maarifa kupata kodi, imerejesha amani kwa wafanyabiashara na wawekezaji walio wengi.

Rais alikwenda mbali zaidi na kuitaka TRA kupanua wigo wa walipa kodi, kwani wafanyabiashara wanaokamuliwa na kuchukuliwa vifaa vyao vya kazi na kufungwa akaunti zao, kisha kuchukuliwa fedha kwenye akaunti kisa sheria inawaruhusu, inasababisha wafanyabiasha kufunga biashara na kwenda nchi nyingine na hivyo kupunguza walipa kodi nchini.

Kauli hii si tu imepokelewa kwa faraja na wafanyabiashara na wawekezaji, lakini pia imetangaza fursa mpya kwa wawekezaji wa ndani na nje kurejesha mitaji yao nchini.

Siku za nyuma hakuna aliyeweza kuhoji ukokotoaji wa kodi ambao uliokuwa unafanywa na kikosi kazi maalumu ambacho kilikusanya mabilioni ya fedha, nyingi zikitumika katika miradi mikubwa inayoendelea hapa nchini.

Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara za lami nchini, kuanzisha mradi wa treni ya umeme (SGR), kuanzisha mradi wa kufua umeme katika bwawa la Mwalimu Nyerere, kujenga barabara za juu jijini Dar es Salaam, Serikali kuhamia Makao Makuu ya nchi Dodoma, ujenzi wa viwanja vya ndege na ununuzi wa ndege.

Pia sehemu ya fedha nina imani zilitumika katika ununuzi wa vivuko na ujenzi wa madaraja maeneo mbalimbali nchini, lakini hata hivyo, vilio vilisikika vya wafanyabiashara na wawekezaji kufunga biashara na wengine kupunguza wafanyakazi.

Naamini hakuna anayepinga kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara na wawekezaji waliokuwa wakikwepa kodi na kuikosesha Serikali mapato, lakini hatua zilizokuwa zikichukuliwa kukusanya kodi ilikuwa ni adhabu kubwa kwa wengi.

Walioathirika si wafanyabiashara na wawekezaji tu, bali hata wamiliki wa shule binafsi na za taasisi za dini, mawakala wa utalii baadhi wamepunguza uwekezaji na wafanyakazi na wakulima wa maua na mbogamboga baadhi wamesitisha kilimo.

Tayari Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba pia ametoa wito kwa wafanyabiashara walioanza kuweka fedha majumbani badala ya benki, kuzirejesha benki fedha bila kuwa na hofu yoyote.

Kauli hii pia ni kujenga imani kwa wafanyabiashara kuwa kuna enzi mpya, warejeshe fedha zao katika mifumo rasmi na kufanya biashara halali bila hofu ya kuchukuliwa fedha zao benki.

Lakini pia wapo waliokwenda mbali zaidi kutokana na Rais Samia na Waziri wa Fedha kuitaka Serikali kupeleka bungeni muswada wa maboresho ya sheria za TRA, kuwazuia kuchukua fedha kwenye akaunti za wafanyabiashara ama wawekezaji bila uamuzi wa Mahakama, kwani bado wana mwanya wa kuendelea kuchukua fedha benki.

Hili ni jambo jema, kwani chombo pekee kinachotambuliwa na Katiba ya nchi kinachotafsiri sheria na kutoa haki ni Mahakama, hivyo ndiyo ina wajibu wa kutoa ruhusa ya wakwepa kodi fedha zao kuchukuliwa kwenye akaunti zao.

Hivyo itoshe kusema fursa nyingine imefunguliwa na Serikali ya Rais Samia, sasa wafanyabiashara na wawekezaji wenye dhamira njema warejeshe mitaji yao nchini bila hofu.

Utulivu na amani iliyopo nchini ni fursa nyingine kwa wawekezaji na wafanyabiashara kurejesha mitaji yao nchini, kwani wana uhakika wa kupata faida ya muda mrefu katika uwekezaji wao. Hivyo itoshe kumpongeza Rais Samia kwa kuleta suluhu katika manung’uniko ya wafanyabiashara na wawekezaji nchini, lakini hii sasa iwe fursa kwao kupanua biashara, uwekezaji na kulipa kodi stahili kwa wakati.


Mussa Juma ni Mkuu wa gazeti la Mwananchi Mkoa wa Arusha, anapatikana 0754296503.