Tatizo la maji linahitaji ufumbuzi wa kudumu
Ukosefu wa majisafi na salama ni changamoto inayozikumba sehemu mbalimbali nchini na kusababisha madhara ya afya kwa maisha ya wananchi.
Miji, maeneo ya vijijini pamoja na mikoa kama Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mbeya, imekuwa ikikumbwa na tatizo la maji.
Wakati mwingine wananchi wanalazimika kufanya maandamano, kama ilivyoshuhudiwa huko Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam, na Msaranga, Kilimanjaro, wakilalamikia ukosefu wa maji.
Hata hivyo, licha ya juhudi zinazochukuliwa na Serikali kupitia mamlaka za maji, bado tatizo hili linajitokeza na kusababisha malalamiko kutoka kwa wananchi.
Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, imechukua hatua kadhaa kushughulikia changamoto hii, ikiwa ni pamoja na kusimamia miradi ya maji na kuwasimamisha watendaji wa mamlaka za maji pale inapobainika kutokuwepo kwa utendaji mzuri. Hata hivyo, matatizo yanayoendelea kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo yanaonyesha kuwa, licha ya juhudi hizi, bado kuna vikwazo vikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maji.
Kwa mfano, wananchi wa Mbezi Msakuzi wanalalamikia ukosefu wa maji licha ya ahadi zilizotolewa na mamlaka ya maji.
Wengi wao wanakiri kutumia maji machafu kutoka kwenye mabonde, huku wakihofia kuambukizwa magonjwa kama ya mfumo wa njia ya mkojo (UTI) na matatizo ya tumbo.
Hiyo inaashiria kwamba changamoto ya maji ni kubwa na inahitaji mikakati ya kudumu, badala ya ahadi zisizotekelezwa.
Ingawa Serikali kupitia Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) imeanzisha miradi ya maji, baadhi ya maeneo bado yanakosa huduma, huku wananchi wakipata shida katika kuhakikisha wanapata majisafi na salama kwa matumizi yao ya kila siku.
Kwa mfano, Mhandisi Edson Robert, Meneja wa Dawasa Ukanda wa Kimara, alieleza kwamba mradi wa maji wa Mbezi Msakuzi ulianza kutekelezwa mwaka wa fedha wa 2023/24, lakini bado haujakamilika.
Kwa mujibu wa Robert, chanzo cha maji cha Mshikamano kimekamilika na kazi ya ugawaji maji inaendelea, lakini haijafikia wananchi wa Msakuzi kwa wakati.
Hii ni changamoto kubwa, wananchi wanapokosa maji, wanashindwa kufanya shughuli zao za kila siku, zikiwamo za kiuchumi.
Serikali inapaswa kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa kwa wakati na kwa ufanisi. Vilevile, ni muhimu kwa mamlaka husika kutoa taarifa mapema kuhusu ukosefu wa maji, ili wananchi wajiandae na kupanga shughuli zao, badala ya kupata mshtuko wa ghafla wa kukosa huduma ya maji.
Tunafahamu hapa nchini miji inakua na idadi ya watu inaongezeka, hivyo kunahitajika mipango ya kudumu na endelevu katika kutatua changamoto za maji.
Serikali inapaswa kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya maji, kama vile kuchimba visima vya maji, kujenga mabwawa na kuboresha mtandao wa usambazaji wa maji.
Pia, kuhitajika kuwepo na usimamizi mzuri wa rasilimali za maji ili kuhakikisha maji yanapatikana kwa usawa kwa kila mwananchi, bila kujali hali yake ya kijamii au kiuchumi.