TB Joshua aliishi vizuri kijamii

TB Joshua aliishi vizuri kijamii

Muktasari:

  • TB Joshua, alikuwa mtu wa majina mengi. Wapo waliomwita “Man of God” – “Mtu wa Mungu”, wengine walimtambua kama “Man of People” – “Mtu wa Watu”.

TB Joshua, alikuwa mtu wa majina mengi. Wapo waliomwita “Man of God” – “Mtu wa Mungu”, wengine walimtambua kama “Man of People” – “Mtu wa Watu”.

Waumini wake walisema TB Joshua alikuwa na uwezo wa kuiona kesho. Ni kwa sababu ya uwezo wake wa kutabiri yajayo na kutokea.

Kuna waliomtaja kama mtu mwenye macho ya kuona giza. Sifa hii ilitokana na jinsi TB Joshua alivyojitengeneza kwa waumini wake, katika Kanisa la The Synagogue Church Of All Nations (SCOAN).

Waumini wake waliamini kuwa hakuna nguvu ya giza iliyobaki salama baada ya kupita kwenye mikono yake.

Alipozaliwa, wazazi wake walimpa jina la Tamitope. Kwa ukamilifu anaitwa, Tamitope Balogun Joshua. Kisha, Tamitope Balogun, yakafupishwa kuwa TB. Ukiongeza na Joshua, unapata ukamilisho wa TB Joshua. Jina ambalo likitajwa, halihitaji utambulisho mrefu kwa watu wa jumuiya ya Kristo, hususan madhehebu ya kilokole.

Juni 12, 1963, ndipo TB Joshua alizaliwa. Jimbo la Ondo, Nigeria, ndio mahali alimulikwa na mwanga wa jua kwa mara ya kwanza. Juni 5, mwaka huu, ikiwa ni siku saba kabla hajatimiza umri wa miaka 58, TB Joshua, alipokea wito wa lazima kutoka kwa Muumba wa mbingu, ardhi na vyote vilivyomo, Kifo.

Kwa kifupi, miaka 58 kasoro siku saba, ambayo TB Joshua aliishi duniani, inaweza kuwa alama kubwa kwenye maisha ya wengi. Uwe uliamini mafundisho yake au hukuamini, ukweli ni kuwa TB Joshua, aliweza kuingia ndani ya maisha ya wengi, hususan kwa jinsi ambavyo alivyoihudumia jamii.

Binafsi, kabla sijamfahamu TB Joshua, niliijua Televisheni ya Emmanuel, ya nchini Nigeria. Nikawa nafuatilia namna ilivyokuwa inafanya kazi za kuhudumia jamii.

Inawatembelea wagonjwa na kuwasaidia kupata huduma za matibabu. Inawafikia wanaoishi kwenye mazingira magumu na kuboresha kiwango chao cha kuishi.

Baada ya kuvutiwa mno na huduma za Emmanuel TV, nikabaini mmiliki wake ni TB Joshua, nikawa natazama mahubiri yake. Hapa niweke wazi kwamba mimi ni Muislamu, lakini huvutiwa na watu ambao hujitoa kusaidia jamii bila kuangalia imani zao. TB Joshua akanivutia.

Ni kwa sababau hiyo, baada ya TB Joshua kutangulia mbele za haki, unaweza kuitazama nguvu yake nje ya Kanisa na kuiona ni kubwa. Alikuwa kiongozi wa kidini aliyekuwa na misimamo ya wazi kwenye jamii katika nyanja mbalimbali. Alipoingia kwenye siasa, alikuwa mpatanishi.

Uchaguzi Mkuu 2015 nchini Tanzania, TB Joshua alihusika moja kwa moja. Alikuwa baba wa kiroho wa wagombea urais wawili wakubwa, Edward Lowassa, aliyekuwa anagombea kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), vilevile Dk John Magufuli, aliyewania kiti cha urais kwa leseni ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kipindi ulipoibuka mvutano wa matokeo, Dk Magufuli alipotangazwa mshindi na Lowassa kupinga, akidai ni yeye aliyeshinda, TB Joshua alisafiri kwa ndege yake binafsi kutoka Nigeria hadi Tanzania, akafanya kazi ya usuluhishia, kwa gharama zake.

Zingatia, yeye ni mtumishi wa kiroho, hakuwa na mapato ya moja kwa moja aliyoyategemea kutoka kwa mshindi yeyote. Alitambua dhima yake kama baba wa kiroho wa wagombea hao.

Zilivuja picha zilizomuonesha TB Joshua akimuombea Magufuli na familia yake, vilevile akiwa na Lowassa na baadhi ya viongozi wa vyama vilivyokuwa vikiunda uliokuwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambavyo vilimsimamisha Lowassa kuwania urais, wakizungumza.

Inaaminika kuwa baada ya kikao hicho, Lowassa alitulia na kuridhia nchi iongozwe na Magufuli, lakini kabla ya hapo kulikuwa na hali tete juu ya matokeo yaliyompa ushindi hayati Magufuli.

Wapo baadhi ya mashabiki na wanachama wa vyama vya upinzani waliokuwa wakitaka waingie mitaani kupinga matokeo hayo. Walitaka idhini au kauli za viongozi wao tu, haikuwa hivyo maana busara ilitumika.

Hivyo vikao vya TB Joshua na pande hizo mbili ni kipimo cha jinsi kiongozi huyo wa dini alivyoamua kuishi kwa kuweka alama.

Inawezekana hata asingekuja nchini baada ya Uchaguzi Mkuu 2015, bado hakuna baya lolote lingetokea.

Hata hivyo, vema kutambua na kuthamini kujitoa kwake kwa ajili ya kuifanya amani ya nchi iendelee kutamalaki. Kwa msisitizo kabisa, zingatia alisafiri kwa ndege yake binafsi na kwa gharama zake.