Teknolojia haikwepeki, tuzidi kuiimarisha

Wiki iliyopita, Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam liliitaka Serikali kushirikiana nalo kudhibiti ukahaba, biashara inayozidi kuota mizizi ndani ya mipaka yake.

Si Kinondoni pekee ambako vitendo vya ukahaba vinaonekana dhahiri, ni biashara haramu inayosambaa nchi nzima kwa sasa na kutishia maadili ya Mtanzania.

Pamoja na kuwa biashara hii, kama ilivyo kwa mapenzi ya jinsia moja, imeharamishwa kupitia Kanuni ya Adhabu (Penal Code) iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019, vilevile inakwenda mbali zaidi kwa kuharibu mila, utu na utamaduni wa Mtanzania.

Matendo haya mawili, ukahaba na ushoga, ambayo nayaona ni ya kishetani, hivi sasa yanafanyika waziwazi, tena katikati ya makazi ya watu mpaka unajiuliza hivi mamlaka hazioni hatari inayolinyemelea Taifa? Lakini majibu huyapati.

Baba wa Taifa, Julius Nyerere aliwahi kusema hatuwezi kuwa na matumaini ya kutatua matatizo yetu kwa kujifanya hayapo, suala la kukithiri kwa ukahaba na ushoga ni tishio ambalo si jipya, bali haliendani na mila, desturi na tamaduni zetu.

Nimemsikiliza Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge na madiwani wake wakisema biashara ya ukahaba inashika kasi jijini Dar es Salaam kiasi kwamba sasa mtu anakata chumba ili viwe vitatu na kuvigeuza danguro kwa ajili ya ufuska huo. Sauti za wahusika hao wakiwa vyumbani na wateja wao, zinawaharibu watoto wa kizazi hiki cha ‘dotcom’ na kuwapa wakati mgumu wazazi kujibu maswali yao.

Kulingana na maelezo yao, baadhi ya madanguro hayo yapo katikati ya makazi ya watu, hasa maeneo ya Msasani, Mwanyamala na Makumbusho na pia ukifuatilia katika baadhi ya barabara mashuhuri, dadapoa nao hujipanga huko.

Hali ikiwa hivyo jijini Dar es Salaam, katika miji mikubwa kama Arusha, Moshi na Mwanza nako biashara ya ukahaba inaonekana waziwazi, hasa usiku kwa dada hao kujiuza nje ya kumbi za starehe wanakokesha.

Katika baadhi ya maeneo, hususan Moshi, baadhi ya walinzi wameyageuza majengo wanayoyalinda kama kitegauchumi chao kwa kuruhusu dadapoa na wateja wao kutumia magodoro wanayoyalalia ili ‘kumalizana’ na kuwalipa chochote kitu walinzi hao. Mapenzi ya jinsia moja nayo yanakuja kwa kasi mno yakihusisha vijana wadogo wanaofikia hatua ya kugombea wanaume baa na katika nyumba za starehe.

Kifungu cha 146 cha sheria niliyoitaja kinasema wazi kwamba ni kosa la jinai kwa mwanamke kuishi kwa ujumla au kwa sehemu, akitegemea kipato kinachotokana na umalaya, lakini usimamizi wa sheria hiyo ukoje?

Kifungu cha 148 nacho kimeeleza wazi kuwa mtu yeyote anayemiliki nyumba, chumba au kutengeneza chumba au vyumba au kuandaa eneo kwa ajili ya kufanyia ukahaba anatenda kosa la jinai.

Na kifungu cha 154(1)(c) kinasema mtu yeyote atakayemruhusu mwanaume mwenzake kumwingilia kinyume cha maumbile au kumwingilia mwanamke, anatenda kosa la jinai na akipatikana na hatia, adhabu yake haipungui miaka 30 jela.

Katika baadhi ya mataifa, hasa ya magharibi vitendo hivyo vimehalalishwa kisheria, lakini hapa ni Tanzania na tuna mila, desturi na tamaduni pamoja na sheria zetu ambazo ni lazima kila aliyepo aziheshimu na kuzifuata.

Ninafahamu wapo ambao suala la ushoga ni la kibaolojia, lakini hawa vijana wadogo tunaowaona huku mitaani ni waliofundishwa au kujifunza wakiwa shuleni au kufanyiwa hivyo na watu wasio wema na kuendelea na mchezo huo.

Ninamshukuru na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan ambaye hivi karibuni alizungumza na wanafunzi wa vyuo vikuu na kuwataka waache kuiga vya nje, akiwasisitiza waishi kwa maadili, mila na desturi na kuachana na mila za kuletewa kutoka nje.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni wiki iliyopita alisaini sheria inayoharamisha vitendo vya ushoga nchini humo ambapo kama ni kosa lake la kwanza atafungwa miaka 14, ila akiendelea ni kifungo cha maisha.

Sheria hiyo haikuishia hapo, inasema kama unamfahamu mtu anayejihusisha na ushoga au kuhamasisha ushoga nawe unatenda kosa. Ndiyo maana nasema kama sheria imesema jambo fulani ni haramu, tunasitasita nini kuchukua hatua?

Mjema ni mwandishi wa gazeti hili mkoani Kilimanjaro. Kwa maoni na ushauri anapatikana kwa namba 0656 600 900.