TFF acheni kufanya ligi kuwa bonanza

TFF acheni kufanya ligi kuwa bonanza

Muktasari:

  • Mtanange wa mahasimu wa Ligi Kuu Tanzania bara, mahasimu wa jiji moja ya Dar es Salaam, Simba na Yanga umeshindwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, juzi usiku.

Mtanange wa mahasimu wa Ligi Kuu Tanzania bara, mahasimu wa jiji moja ya Dar es Salaam, Simba na Yanga umeshindwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, juzi usiku.

Ni mchezo mkubwa kwa soka la Tanzania na Afrika Mashariki kwa jumla, kwa kuwa upinzani wa timu hizi umekuwa maarufu kwa sasa katika nchi nyingi za Afrika.

Ni takribani mchezo mkubwa wa nne katika michezo mikubwa inayotambulika Afrika.

Awali, mchezo huu ulitakiwa kuanza saa 11 jioni ya Jumamosi, wakati mashabiki wa timu zote mbili wakianza kuingia uwanjani mapema majira ya saa nne asubuhi, kusubiri muda wa mchezo.

Lakini kwa mshituko, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TTF) ilitoa taarifa baada ya uvumi wa muda kuwa mchezo huo unatakiwa kuanza saa moja usiku, badala ya 11 jioni, muda uliokuwa umepangwa awali kufanyika.

Kwa mujibu wa taarifa ya TFF, mchezo huo ulisogezwa mbele kutokana na kupokea maelekezo mabadiliko ya muda wa kuanza kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Ni taarifa iliyozua taharuki kwa mashabiki hasa wa Yanga, waliokuwa wakiamini mchezo huo utaanza mapema na kupata muda wa kufuturu kwa waumini wa dini ya Kiislamu.

Wakati tukio hilo linaendelea, uongozi wa Yanga ulitoa taarifa yake iliyosainiwa na katibu wake mkuu ikionyesha kusikitishwa kwao na mabadiliko ya muda yaliyotangazwa na TFF.

Katika taarifa hiyo, Yanga ililaani mabadiliko hayo yaliyosababisha taharuki na kueleza kuwa ni batili kwa mujibu wa kanuni za soka, zinazotaka mabadiliko yote yatakayofanyika kuwa zaidi ya saa 24.

Yanga ilinukuu kipengele cha kanuni ya 15 (10) cha Ligi Kuu Tanzania Bara kinachosema ‘mabadiliko yoyote ya muda wa kuanza mchezo yatajulishwa ipasavyo kwa pande zote husika za mchezo angalau saa 24 kabla ya muda wa awali.’

Inawezekana kukawa na mabadiliko ya msingi yaliyotakiwa kufanyika kama awali, wakati mashabiki na wadau walipolalamikia muda wa kuanza kwa mchezo, lakini hili la juzi limeshusha hadhi ya ligi.

Kuna watu walipanga mambo tofauti kwa ajili ya muda wa awali, kama kuangalia mapema na watoto na kurudi nyumbani kabla ya saa 2 usiku, wengine waliokuwa wakisafiri wakidhani wangeweza kwanza kuangalia mchezo mapema.

Lakini kilichotokea ni kama Ligi Kuu kuwa bonanza kwa kuwa na maelezo yalioyoshindwa kufuta sintofahamu kwa mashabiki bila kuwa na sababu za msingi.

Kitendo cha kuitaja wizara kubadili muda wakati maelekezo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (Fifa) yanakataza serikali kuingilia michezo, hili linakuwa jambo la kufikirisha mno.

Tujifunze kwa hili na tuache kushusha thamani ya ligi yetu kwa mambo ambayo yanaweza kuepukika.

TFF kama ilikuwa na nia ya kusogeza muda mbele wa mchezo huu, ilitakiwa kuweka taarifa hiyo katika kikao kabla ya mechi (Pre match meeting), ambacho hufanywa asubuhi ya mchezo, angalau ingesaidia kwa wakata tiketi kujua muda sahihi wa kwenda uwanjani na kuamua kama unawafaa au vinginevyo.

Tunaamini kuwa TFF ina viongozi waadilifu, lakini suala hili nadhani hadi sasa lingekuwa limechukua sura mpya kwa kiongozi kujiuzulu kupisha aibu hii.

Ni suala la ajabu kutokea katika soka letu na hakuna mpenda soka aliyekuwa na wazo la mchezo ule kutofanyika kwa sababu ambazo hazisimuliki.