THBUB iwezeshwe kusaidia wananchi
Ibara ya 8 (1)(a) ya Katiba inasema: “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii.”
Hata hivyo, kumekuwa na uvunjifu wa haki za binadamu na mbaya zaidi malalamiko yanaelekezwa kwa mamlaka za Serikali.
Matokeo yake, badala ya Serikali kupata madaraka kutoka kwa wananchi, imekuwa kinyume, wananchi ndio wanaomba mamlaka kwa Serikali.
Kumekuwa na malalamiko ya watu kukamatwa bila kufuata utaratibu wa kisheria na matokeo yake wengine wamedaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
Kumekuwa na malalamiko ya wananchi kunyimwa dhamana wanapokamatwa na wengine wanazilalamikia mahakama kwa kuchelewesha mashauri yao.
Magerezani, kumekuwa na malalamiko ya watu walioko rumande na waliofungwa kuteswa, kudhalilishwa na wengine kuuawa kwa vipigo.
Kutokana na malalamiko hayo, mwaka 2023 Rais Samia Suluhu Hassan aliunda Tume ya Haki za Jinai iliyochungumza mamlaka za utoaji za haki zikiwamo Mahakama, Jeshi la Polisi, Magereza na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), kisha ikatoa ripoti yake.
Mbali na mamlaka nyingine, THBUB ilipewa mapendekezo sita ambayo ni pamoja na kuongeza rasilimali watu na fedha, kuanzisha divisheni maalum itakayopokea malalamiko ya wananchi, kupitia muundo wa tume hiyo, kuboresha upatikanaji wa taarifa, kutumia kifungu cha 6 cha sheria yetu kinachotaka kushitaki mamlaka inaposhindwa kutekeleza mapendekezo yake na kutoa elimu kwa umma.
Ieleweke kwamba tume hiyo imeanzishwa kwa mujibu wa Katiba ili kufuatilia utekelezaji wa haki za binadamu.
Hata hivyo, imeelezwa kwamba bado inakabiliwa na changamoto zikiwamo za upungufu wa watumishi na bajeti.
Licha ya mikakati ya Serikali kuwezesha tume hiyo kutekeleza majukumu yake, nadhani bado inapaswa kuwezeshwa zaidi ili iwe na nguvu ya kudhibiti mamlaka za Serikali zinazotajwa kuvunja haki za binadamu.
Hata hivyo, THBUB inaweza kutumia mamlaka yake kikatiba kuongeza makali ili kudhibiti uvunjifu wa haki za binadamu.Kwa kuwa tayari kumekuwa na malalamiko ya wananchi kwa vyombo vya Dola, ni wakati wa tume nayo kufanya kazi yake, kwa mfano kulidhibiti Jeshi la Polisi.
Baada ya Tume ya Haki Jinai kutoa mapendekezo yake, tusingetarajia kuendelea kusikia malalamiko yale yale yakiendelea, watu wanaendelea kulalamika kunyimwa dhamana, wengine wanadai kutekwa na vyombo vya Dola. Uko wapi udhibiti wa THBUB?
Mbali na THBUB, watendaji wa vyombo vya utoaji haki nao wanapaswa kubadilika kitabia na kuwa na jicho la ubinadamu.
Kama tayari Rais Samia ameonyesha dhamira ya kuleta mabadiliko katika mfumo wa haki jinai, kwa nini watendaji bado wana kiguigumizi?
Iweje mtu apotee na polisi wamtafute, halafu baada ya mwezi mzima, polisi hao hao waseme wanamshikilia? Hiki ni kigugumizi na kiburi ambacho hakitegemewi kutokea katika nchi inayofuata utawala wa sheria, tena baada ya Tume ya Haki Jinai kutoa mapendekezo yake.
Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) inaeleza waziwazi jinsi vyombo husika vinavyotakiwa kukamata mtu, lakini utashangaa watu wanavyokamatwa, kwanza utambulisho wa wahusika haueleweki na wala mtu haelezwi kosa lake.
Inawezekana kuna wahalifu wanatumia mwanya huo huo kutekeleza uhalifu, lakini utawatofautishaje na wengine?
Haya yote yanapaswa kufanyiwa kazi na THBUB, ikiwa pamoja na kutoa elimu ya sheria kwa wananchi ili wajue haki na wajibu wao.
Pia tume itumie sheria yake na izishitaki mamlaka zinazokataa kutekeleza mapendekezo yake ili kuleta nidhamu na heshima kwa haki za watu.
Serikali nayo ina wajibu wa kuiwezesha THBUB na kuhakikisha inaheshimiwa. Ripoti ya Tume ya Haki Jinai itolewe kwa umma ikiwezekana mitandaoni ili watu waisome.
Kumekuwa na tume nyingi zinazoundwa na marais kwa nyakati tofauti, lakini utekelezaji wa mapendekezo yake nao umekuwa ni changamoto.
Tume hizi zinagharimu fedha nyingi za Serikali na zinakuja na mapendekezo mazuri, lakini mengi huwa hayatekelezwi na kusababisha turudi kwenye malalamiko yale yale ya wananchi miaka nenda miaka rudi.