Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tuchangamkie fursa na 'maokoto' halali

Mwamko wa kuchangamkia fursa za biashara, uzalishaji na kujiajiri umekuwa mkubwa katika jamii zetu, hususan katika zama hizi za mitandao ya kijamii. Wito wa kutafuta “maokoto” umekuwa kama wimbo unaocheza kwa sauti kubwa bila kusimama katika akili na masikio ya vijana wengi. Hata hivyo, kuna umuhimu mkubwa kwa mtu binafsi kujizoesha kujitafutia kipato kinachotokana na shughuli halali.

Neno “halali,” kwa maana rahisi, ni “inayokubalika.” Linaweza kuwa na tafsiri kadhaa kulingana na mitazamo tofauti. Kwa mfano, sheria za nchi zinaweza kukataza shughuli fulani kuwa si halali, hata kama shughuli hizo zinaweza kuleta fedha nyingi kwa haraka, lakini si halali kisheria.

Kwa kuwa mwanadamu haishi hewani, uhalali katika shughuli zake anazozifanya unaweza kubeba tafsiri inayotokana na imani za kidini au mitazamo ya kijamii. Kinachoonekana kuwa halali kwa mtu binafsi kinaweza kuwa tofauti kulingana na mitazamo hiyo. Mathalan, biashara ya ukahaba inaweza kuwa halali kisheria katika baadhi ya nchi, lakini ni fedheha, si halali kwa desturi za jamii, au ni dhambi kwa tafsiri za kidini.

Kujihusisha na shughuli za kuzalisha kipato ambazo si halali si tu kunakiuka sheria, bali pia kunapinga kanuni za kimaadili. Shughuli hizi zinaweza kukupa fedha nyingi, lakini pia zinaacha athari isiyoweza kurekebishwa, na nyingine zinaacha janga kwa maisha ya binadamu.

Kwa mfano, biashara kama usafirishaji wa watu kwa ajili ya kuwatumikisha katika shughuli za ngono, kazi za kulazimishwa, au kuuza viungo vya binadamu inatengeneza pesa nyingi.

Taarifa ya Idara ya Usalama wa Ndani ya Marekani (Counter Human Trafficking, US Department of Homeland Security, 2020/2021) iliwahi kutaja kuwa biashara hiyo duniani ina thamani ya Dola bilioni 150 mwaka 2020. Kiwango hicho ni zaidi ya mara mbili ya Pato la Taifa la nchi yetu. Lakini, shughuli hiyo inawanyonya watu wasio na uwezo kwa faida ya kifedha, kuwaacha vilema maisha yao yote, na wengine kupoteza uhai.

Vilevile, uhalifu wa kimtandao kwa sasa umekuwa changamoto inayokua. Japokuwa unaweza kuvuna faida kubwa ya kupata mabilioni kwa haraka ukifanikiwa, ni wizi; umeibia watu fedha zao na kusababisha hasara kwa watu na biashara zao. Si sawa ikiwa unaendesha gari kubwa la kifahari kwa pesa zinazotokana na jasho la wengine.

Mathalani, biashara ya uuzaji wa dawa za kulevya inaonekana kuleta faida kubwa kwa haraka, lakini athari zake mbaya ni kubwa mno. Biashara hii inachochea uhalifu na kuharibu maisha ya vijana wengi ambao wanakuwa watumwa wa uraibu. Kuna sifa gani katika kuwa bilionea kwa kusababisha uharibifu wa maisha ya wengine? Faida ya haraka haifai kwa gharama ya kuangamiza jamii.

Kwa sasa, kamari na michezo ya bahati nasibu vimekuwa vikiwavutia wengi kama njia ya mkato ya kujipatia kipato. Wakati kuna wachache wanaoweza kufanikiwa kupitia michezo hii, vijana wengi wanatumia muda mwingi wakicheza kamari badala ya kufanya kazi au kujishughulisha na shughuli za maendeleo. Matokeo yake, ari ya kufanya kazi inapungua.

Ikiwa mwamko huu utaendelea kuongezeka, athari zake kwa jamii zitakuwa kubwa. Kwanza, kamari inaweza kupelekea utumwa wa kifedha, ambapo watu wanajikuta wakitumia pesa zote kwenye michezo hii, wakitumai kupata “bahati.”

Pia, wengine wanapokuwa na madeni au wanaposhindwa kupata fedha za kucheza kamari, wanaweza kugeukia njia nyingine zisizo halali za “chapchap” kupata pesa, na kuibuka kwa vitendo viovu.

Ni taifa gani duniani limejengwa kwa kucheza kamari? Hakuna. Maendeleo ya taifa yanategemea ubunifu, uvumilivu, na shughuli halali. Bahati nasibu haziwezi kuwa msingi wa maendeleo ya kijamii au kiuchumi.